Home Habari za michezo JE JUMAPILI NI SIKU YA SIMBA!? DABI HII KUAMUA KILA KITU

JE JUMAPILI NI SIKU YA SIMBA!? DABI HII KUAMUA KILA KITU

Habari za Simba SC

ZIMEBAKI siku tatu kabla ya mechi kubwa nchini Simba vs Yanga, lakini kwa takwimu za kiufundi zilivyo gemu itakuwa ya ufundi mwingi na itafia kwenye maeneo kadhaa. Mechi hiyo itapigwa Jumapili saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Hii ni Dabi kubwa zaidi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki. Yanga inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa wageni wa Simba, lakini ina deni kubwa kwa kuwa msimu uliopita ilimaliza bila kuibuka na ushindi dhidi ya watani wao hao kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na kwamba mwisho walitwaa ubingwa mchezo kwa kwanza walitoka sare ya 1-1, lakini mchezo wa pili Yanga wakalala kwa mabao 2-0, hivyo wana deni kubwa kwa mtani wao.

Timu zote kwenye ligi msimu huu hadi sasa zimeshaonyesha makali yake, Yanga ipo kileleni kwa pointi 18 baada ya kucheza michezo saba, imepoteza mmoja, imeshinda sita haina sare.

Simba inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa imecheza michezo sita, mmoja nyuma ya Yanga, imeshinda sita, haijapoteza, haina sare ipo nyuma ya Yanga kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Pamoja na mafanikio yao kwenye mechi ya ligi hadi sasa, lakini kila moja ina ubora na udhaifu wake kwenye mchezo huu na kama wakitumia vibaya madhaifu yao yatawakuta makubwa.

Yanga isipoteze…

Pamoja na ukubwa wa Dabi lakini Yanga inaonekana kuwa haitakiwi kupoteza kwa kuwa hali hiyo inaweza kuwatoa kwenye reli, kama Simba ikishinda mchezo huo na kiporo ilichonacho itakuwa tofauti ya pointi sita na watani wao.

Katikati Yanga ina watu…

Kwa hali ilivyo kwenye ligi hadi sasa , ili timu yoyote iweze kupambana na Yanga inatakiwa kuhakikisha viungo wake, Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua hawapati nafasi mbili muhimu, moja kutengeneza nafasi na ya pili kufunga mabao.

Hawa ndiyo wamekuwa ngome ya Yanga msimu huu na wamekuwa wakifunika tatizo la ukosefu wa mshambuliaji kwenye uwezo wa juu la timu hiyo.

Aziz Ki ndiye anaongoza kwa mabao hadi sasa akiwa amefunga sita, akitokeo eneo la kiungo akifutiwa na Maxi Nzegeli mwenye matano, matatu anayo kiungo mwingine, Pacome Zouzou.

Moja ya sehemu ambayo Simba wanatakiwa kuhakikisha wanaidhibiti ni eneo hili ambalo limekuwa likifanya kazi kubwa sana kwenye michezo yote.

Lakini kama watawazuia kufunga basi wawazuie na kutengeneza kwani Maxi mwenye mabao matano tayari ana pasi mbili za mabao hiyo kuwafanya Yanga ambao wameshafunga mabao 20 yeye mwenyewe kuhusika kwenye mabao saba.

Kwa upande wa Simba, eneo lao la kiungo siyo hatari, lakini lina watu ambao wanafanya kazi kubwa ya ulinzi kutokana na kucheza wenyewe muda mrefu lakini wakiwa na uzoefu zaidi wa mechi hizi, suluhu kwao kwenye mchezo huu ni kuwatumia watu wawili wa kuzuia, sana Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute ambao wameonekana kuwa na mhimili nzuri kwenye michezo waliyocheza ukiwemo ule wa pili dhidi ya Al Ahly kwenye African Football League.

Eneo hili kwa Simba linatabirika zaidi lakini kwa Yanga limekuwa halitabiriki kwani linabadilika kutokana na jinsi ambavyo kocha wao atakuwa ameamka.

Diarra kinara clean sheet, Salim….

Hili ni eneo lingine ambalo linaweza kuamua mchezo huu, mara nyingi uwezo wa kipa bora umekuwa ukisaidia timu kuibuka na ushindi.

Hakuna shaka kubwa Yanga wanaonekana kuwa kwenye njia nzuri zaidi kuliko Simba kwenye eneo hili.

Uwezo wa Djigui Diarra umekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Yanga, huyu ndiye anaongoza kwa makipa wenye ‘clean sheet’ nyingi akiwa amecheza michezo minne bila lango lake kuruhusu bao.

Kwa upande wa Simba mambo yamekuwa tofauti, Salim ambaye pia alionyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga baada ya kuokoa penalti tatu na kuipa timu yake Ngao amekuwa na makosa mengi msimu huu kwenye michezo ya dakika 90.

Aina yake ya kutema mipira ndani ya eneo la boksi imekuwa ikiigharimu timu hiyo kwenye michezo mingi ukiwemo ule wa kwanza wa African Football League dhidi ya Ahly.

Hata hivyo, faida nyingine kwa Yanga hapa ni kipa wao kuzungumza mara kwa mara kuwapanga mabeki wake lakini kupiga mipira mirefu, tofauti na Salim ambaye muda mwingine amekuwa mpole zaidi langoni.

Ushambuliaji ni Simba…

Yanga hawana jambo la kuzungumzia sana kwenye eneo lao la ushambuliaji, usajili wa Hafidhi Konkon umeonekana kutolipa na hadi sasa hana nafasi ya uhakika, lakini pia Kennedy Musonda ameshindwa kuziba viatu vya Fiston Mayele, lakini Simba hapa ni moto zaidi.

Eneo la ushambuliaji la Simba limekuwa na makali kutokana na uwepo wa Jean Baleke ambaye tayari ana mabao sita kwenye ligi hiyo akiwa sawa na Ki wa Yanga.

Lakini eneo hili pia Simba wana Moses Phiri ambaye ameshafunga mabao matatu pamoja na kucheza muda mchache msimu huu, hivyo kwenye mabao 16 washambuliaji wamefunga mabao 9, likiwa ndiyo eneo tegemeo zaidi kwa mabao ya Simba msimu huu.

Yao 4, Tshabalala na Kapombe 4…

Moja ya eneo ambalo linabadilika kila siku kwenye soka duniani ni mabeki wa pembeni, awali hawa kazi yao ilikuwa kulinda, lakini sasa soka limewabadilisha na wanafanya kazi ya kulinda na kutengeneza mabao.

Misimu miwili iliyopita Simba wamekuwa wakizalisha mabao mengi kupitia kwa Shomary Kapombe na Mohammed Hussein Tshabalala, lakini Yanga wamelipa msimu huu kwa kumshusha Yao Kouassi ambaye kwa sasa ndiye kinara wa pasi za mabao kwenye Ligi Kuu Bara akiwa nazo nne.

Huyu amekuwa beki mahiri kwenye eneo hilo, lakini uwezo wake wa kupiga krosi na wakati mwingine pasi za karibu zinawafanya Simba wawe makini eneo la pembeni, wakati yeye ana nne, Simba kazi hiyo ameonekana kuifanya Luis Misquissone ambaye ana pasi tatu, hivyo kama atapata nafasi kwenye mchezo huu anaweza kuwa madhara.

Aina ya Yao kucheza inafanana na Tshabalala na Kapombe ambao kila mmoja ana pasi mbili, wamekuwa wachezaji wanaopanda zaidi, moja, makocha wawape mawinga wanaoweza kuwasaidia kulinda wakiondoka kwenye eneo lao kwenye mchezo huu, au wawe na uwezo mkubwa wa kurudi kwa haraka kwenye eneo lao baada ya mpira kupotea.

Faulo, chunga Aziz KI….

Simba moja ya jambo ambalo wanatakiwa kuwa nalo makini kwenye mchezo huu ni kutegeneza faulo kwenye eneo lao la hatari kama Aziz Ki atakuwa uwanjani Jumapili, staa huyo amekuwa bora kwenye mapigo hayo akiwa kwenye mabao yake msimu huu ameshafunga mara tatu kwenye faulo.

Hata hivyo, kuna kumbukumbu ya bao ambalo aliwahi kufunga kwenye dabi kama hii wakati Simba ilipocheza na Yanga msimu uliopita na mchezo kumalizika kwa sare.

Simba wana Clatous Chama, Saido lakini kwa siku za hivi karibuni makali yao yamepungua.

Robertinho vs Gamondi

Staili ya kucheza na kocha wa Yanga, Miguel Gamondi inamvutia shabiki yeyote ambaye anataka kutazama soka safi, amekuwa akiitengeneza timu yake kucheza mchezo wa kuvutia kwenye kila mechi, pasi nyingi, kosa kosa nyingi na zaidi mpira wa burudani.

Hii ni staili bora ambayo mashabiki wanaipenda na amekuwa na uwezo wa kubadilika kwenye kila mchezo kwenye eneo la ushambuliaji, kiungo na hata mabeki kutokana na kikosi chake kuwa na watu wengi.

Siyo jambo la ajabu kucheza bila mshambuliaji kwenye mechi zake, siyo ajabu kumuona Mzize akianza na siyo ajabu kumuona akiwatumia mabeki watatu badala ya wanne kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Azam.

Robertinho, amekuwa tofauti na Gamondi msimu huu timu yake haijacheza mechi hata moja ikivutia, lakini ni timu ambayo ni ngumu kupoteza mchezo kwenye dakika tisini pamoja na kwamba imekuwa ikiruhusu mabao mengi kwenye timu yake.

Robertinho amekuwa akibadili kikosi chake kila kila kinachopata bao au kinaporuhusu bao kwenye mchezo wowote, ni kocha ambaye analinda alichonacho, huku Gamondi akiendelea kutafuta kitu kipya hata baada ya kupata, akifunga bao moja anatafuta la pili, Robertinho akifunga moja analilinda hilohilo.

Jumapili ya Simba?

Simba imekuwa ikijitapa kuwa Jumapili ni siku yake, huku Yanga mara nyingi ikitaka michezo yake ipigwa Jumamosi, katika michezo 36 ya ligi waliyokutana Jumapili tangu ligi hiyo imeanzishwa mwaka 1965, Simba imeshinda mara 10, Yanga mara saba na michezo 19 ni sare.

SOMA NA HII  GAMONDI AIPA TANO SIMBA, BAADA YA KIPIGO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here