Home Habari za michezo JEMBE LA NABI LAMKOSHA GAMONDI, MWAMBA AREJEA KUNDINI

JEMBE LA NABI LAMKOSHA GAMONDI, MWAMBA AREJEA KUNDINI

KOCHA Mkuu wa Yanga, Muargentina, Miguel Gamondi, amesema anafurahia aina ya uchezaji wa beki wa kati wa timu hiyo, Dickson Job, huku akimuhakikishia nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza.

Beki huyo hakuchezeshwa katika michezo miwili ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na Simba, huku akianzishwa Ibrahim Bacca, ambaye katika mchezo wa hatua ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika alitupwa benchi.

Job alikuwa kipenzi cha aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi ambaye hivi sasa anaifundisha FAR Rabat ya Morocco.

Akizungumza na Spoti Xtra, Gamondi alisema hakumtumia Job katika michezo hiyo miwili ya Ngao ya Jamii kwa sababu za kiufundi na kubwa mazingira ya uwanja ambao usingemfanya acheze vile ambavyo anataka.

Gamondi alisema Job ni mzuri katika kucheza mipira tofauti na Bacca ambaye uzuri wake upo katika mipira ya juu ambayo timu zote za Simba na Azam FC ziliingia kwa mbinu ya kucheza mipira ya juu kutokana na hali ya uwanja.

Aliongeza kuwa kutokana na aina yake hiyo ya uchezaji ya Job ya kupiga pasi za uhakika, amepanga kumtumia katika kila mchezo utakaomuhitaji wakiwa wanaanzisha mashambulizi kuanzia chini golini kwao kwenda kwa wapinzani.

“Unajua watu hawajui sababu za kutomtumia Job kule Tanga katika michezo miwili ya Ngao ya Jamii, ukiangalia yeye ni mzuri kwenye kucheza mipira ya chini tofauti na Bacca ambaye ni mzuri kwenye mipira ya juu.

“Ukiangalia Uwanja wa Mkwakwani utaona ulikuwa haumfanyi awe huru kutokana na aina yake ya kucheza mpira wa chini na pasi, ila mmeona pale Azam Complex namna ambavyo amecheza.

“Ni mchezaji ambaye nitakuwa namtumia kila mechi ninayohitaji kucheza sana mpira maana ana uwezo huo wa kutoa pasi za uhakika hivyo itakuwa vizuri tukicheza kuanzia kwake pale nyuma,” alisema Gamondi.

SOMA NA HII  AHMED ALLY: HATUKUPATA TULICHOTAKA KWA YANGA...TUNAHASIRA NA SARE...