Home Habari za michezo GAMONDI : HAO CR BELOUIZDAD DAWA YAO TAYARI IMECHEMKA WAJE TU

GAMONDI : HAO CR BELOUIZDAD DAWA YAO TAYARI IMECHEMKA WAJE TU

Habari za Yanga SC

Wakati uongozi wa Yanga ukianza kuandaa mikakati ya namna ya kuvuna alama zote tisa kwenye mechi zake za nyumbani za hatua ya makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameanika kinachompa jeuri ya kutoona sababu ya kuwa na mshambuliaji asilia katika kikosi chake.

Yanga hadi sasa imecheza mechi tisa ikitikisa nyavu mara 26 na kuruhusu mabao matono, Stephen Aziz Ki na Max Nzengeli wakiwa vinara wa kufunga ndani ya timu hiyo kila mmoja akicheka na nyavu mara saba na manne yakifungwa na Pacome Zouzoua

Washambuliaji Hafiz Konkoni na Clement Mzize kila mmoja amefunga mabao mawili huku kiungo mkabaji Mudathir Yahya na beki wa kati, Dickson Job kila mmoja akifunga moja.

Akizungumza na Nipashe, Kocha huyo alisema mipango yake katika kufundisha anawapa uhuru wachezaji wake hasa mwenye uwezo wa kutumia nafasi anaweza kufunga na si lazima mshambuliaji.

Alisema wachezaji wote wana kazi ya kupambania timu uwanjani ili kutafuta ushindi, na lazima kila mmoja kuwa makini kutumia vizuri nafasi zinazopatikana bila kujali anacheza nafasi gani.

“Mipango yangu kila mchezaji anatakiwa kutumia nafasi zinazopatikana akiwa sehemu nzuri kufunga, anatakiwa kufanya jukumu hilo, kila mtu yupo huru kupambania timu kupata matokeo chanya.

Ukiangalia mabao tuliyofunga mengi yamefungwa na viungo, washambuliaji hawajafunga mabao mengi, hii ni jinsi gani ninavyotaka kwa wachezaji wangu hasa katika kushirikiana kutimiza majukumu,” alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa viungo wanafunga mabao mengi na mabeki watafanya hivyo kwa kuwa anawapa uhuru wa kufunga ili kuipa timu matokeo mazuri na kufikia malengo yao.

Gamondi alisisitiza kuwa anahitaji kuona matokeo mazuri katika kila mechi jambo ambalo wachezaji wake wanatambua na kila mmoja kuhakikisha anatimiza majukumu anayopewa siku ya mechi.

Kuhusu maandalizi ya mchezo ujao wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad, Algeria, alisema mazoezi yanaendelea kwa wachezaji ambao hawako kwenye majukumu ya timu za taifa.

“Tumefanikiwa kuwaangalia wapinzani wetu baadhi ya mechi zao na kuona ubora wao kikubwa ni maandalizi yetu kuelekea mchezo huo ni muhimu kupata matokeo mazuri ugenini,” alisema Gamondi.

Katika hatua nyingine uongozi wa klabu hiyo, umesema kwa sasa inandaa mikakati ya kuhakikisha inashinda mechi zake zote tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika itakazocheza nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikiamini ndizo zitakazoivusha kwenda hatua ya robo fainali.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema mkakati huo utajumuisha viongozi, benchi la ufundi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambapo kila mmoja atakuwa na jukumu la kuhakikisha timu hiyo inasonga mbele na kufikia hatua ya robo fainali kwa pointi tisa za nyumbani.

“Tupo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini asikudanganye mtu, ukifika hatua hii ili usonge mbele na kufika robo fainali ni lazima uchukue pointi tisa za nyumbani, na sisi kama Yanga mchezo wetu wa kwanza nyumbani tutacheza na Al Ahly ya Misri Desemba 2, ukiacha wa kwanza wa ugenini Novemba 24 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

“Wanachana na mashabiki wa Yanga tuna kazi moja tu Desemba 2, tutakuwa na mchezo mgumu sana dhidi ya Al Ahly, lakini kutokana na umoja tulionao hakuna mchezo mgumu kwa Yanga, na niseme tu msimu uliopita tulifika fainali kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, msimu huu kuna jambo letu lingine tunalolitafuta,” alisema.

Akifafanua hilo, Kamwe alisema wanachama na mashabiki wao watakuwa na kazi moja tu ya kuja uwanjani na kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuwashangaza wageni, ambapo benchi la ufundi kazi yake itakuwa ni kuwasuka, kuwatengeneza na kuwapa mbinu na ujanja wachezaji.

SOMA NA HII  HUKO AZAM SIO POA UNAAMBIWA MASTAA HAWAMTAKI KOCHA.......HUKU MABOSI NAO WAZIBA MASIKIO