Home Habari za michezo HAPA SIMBA WAVUNJE TU BENKI MAANA SIO KWA DAU HILI

HAPA SIMBA WAVUNJE TU BENKI MAANA SIO KWA DAU HILI

Tetesi za Usajili Simba

Mabosi wa Simba wanaendelea kukuna kichwa juu ya kumalizana na kocha Abdelhak Benchikha ambaye ndiye pekee aliyepenya kwenye mchujo uliofanyika, ili wamlete kuchukua nafasi ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyefutwa kazi baada ya kufungwa 5-1 na Yanga, hata hivyo ni lazima wavunje benki ili kumleta nchini.

Simba italazimika kuvunja benki ili kutoa mkwanja mnene zaidi wa kumleta kikosini na hilo linaelezwa limeanza kuwatia ubaridi mabosi hao kwa kushindwa kujua nani atakayemlipa wakati klabu haina pesa.

Uzoefu wa Benchikha katika soka la Afrika kwa zaidi ya miaka 20, akitwaa mataji mengi tofauti ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita alipoifunga Yanga katika fainali akiwa na USM Alger kisha kubeba CAF Super Cup ilipoichapa Al Ahly kabla ya kujiuzulu, ni miongoni mwa sifa zilizoifanya Simba kuvutiwa naye na kutaka kumpa kazi lakini pesa anayohitaji kocha huyo huenda ikawa kikwazo kwake kutua.

Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba kwamba, kocha huyo ili atue kikosini anahitaji kulipwa si chini ya Euro 220,000 ( zaidi ya Sh597 milioni) kwa mwaka ambazo ukigawa kwa miezi 12 ni zaidi ya Sh49 milioni kwa mwezi.

Rekodi zinaonyesha SImba haijawaku kuwa na kocha wa kumlipa kiasi hicho cha fedha na hicho ndicho kinachowafanya mabosi wake kuanza kukuna vichwa, licha ya kila mmoja kutamani kumleta ili aifundishe timu hiyo inayoshika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu na inayoshiriki makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, mmoja wa vigogo hao wa Simba amesema kwa sasa wanaendelea kufanya majadiliano na kocha huyo na kama kila kitu kitaenda sawa anaweza kutua Msimbazi.

“Hiyo ni pesa nyingi kwa utaratibu wetu, lakini hadi sasa hatujafika mwafaka. Kama tutaamua kwenda na huyo mtajua na kama tutabadili mtajua pia ila nasisitiza hatujaamua kuachana au kuendelea naye,” alisema kigogo huyo jina tunalo.

Pamoja na uongozi wa Simba kutotoa taarifa kamili kuhusu hatima ya kocha huyo, Mwanaspoti linajua huenda viongozi wa timu hiyo wakalipiga chini jina la Benchikha na kuangalia kocha mwingine kwani kuna zaidi ya makocha 30 kutoka ndani na nje ya Afrika wametuma wasifu wao wakiomba kazi.

Hata hivyo, waliamua kukaushia kupitia CV hizo kwa vile mezani mwao walikuwa na majina matatu ya haraka, Nasreddine Nabi na Sven Vandenbroeck aliyewahi kuinoa kabla ya kutimika Morocco.

Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliendelea kuwataka mashabiki wa Simba kuwa na subira katika kipindi hiki kwani uongozi unafanya tathimini ya makocha waliotuma wasifu na baada ya kumpata mmoja wao watamtangaza hivi karibuni.

“Tunaomba muwe wavumilivu. Kwa sasa ligi na mashindano mengine yanaendelea, hatutaki kocha wa kuja na kuanza kubabaisha, tunataka mwalimu atakayekuja na kuendana moja kwa moja na kasi ya michuano tunayoshiriki. Viongozi wetu wako makini juu ya hilo na wanalifanyia kazi, siku si nyingi kuanzia leo (jana), tutawatangazia kocha wetu mpya,” alisema Ahmed.

Simba kwa sasa ipo chini ya kocha wa makipa Mhispanyola Dani Cadena mwenye sifa zote za kuwa kocha mkuu, huku akisaidiwa na nguli wa timu hiyo aliyewahi kucheza na kufundisha hapo kwa mafanikio, Seleman Matola ikiendelea kujifua kwenye uwanja wake wa mazoezi wa Mo Simba Arena, Bunju.

Mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast utapigwa Novemba 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na jana Ahmed alitangaza kuanza kuuzwa kwa tiketi pamoja na bei za viingilio vya mechi hiyo kubwa.

SOMA NA HII  SABABU ZA SIMBA KUACHANA NA KIPA WAO MBRAZILI ZAWEKWA WAZI