Home Habari za michezo HAPA SIMBA,PALE YANGA, HUKU HESHIMA PALE REKODI SIO POA HUKO LIGI YA...

HAPA SIMBA,PALE YANGA, HUKU HESHIMA PALE REKODI SIO POA HUKO LIGI YA MABINGWA

KWA mara ya kwanza kwenye soka la Tanzania, klabu za Simba na Yanga zinatengeneza historia kwa kucheza kwa pamoja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku mmoja akianzia ugenini na mwingine nyumbani.

Tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika upande wa CAF haijwahi kushuhudiwa watani hao wa jadi wakicheza kwa pamoja hatua ya makundi ambayo imeanza kutimua vumbi wikiendi hii.

Yanga usiku wa jana ilikuwa Algeria ilikotupa karata yake ya kwanza katika Kundi D kwa kuvaana na CR Belouizdad, ilihali Simba yenyewe itakuwa nyumbani jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kucheza na miamba ya Ivory Coast, ASEC Mimosas.

ALSO READ
Kweli zinatisha ila zinafungika
Soka 25 min ago

Macho na masikio ya wadau wa soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla vimeelekezwa kwenye michezo hiyo mikubwa ambayo inafungua milango ya kibarua walichonacho watani hao wa jadi ambao msimu uliopita walifanya vizuri kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Msimu uliopita tulishuhudia Simba ikifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Yanga yenyewe ikionyesha ubabe kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako ilipoteza kwa kanuni ya mabao mengi zaidi ya ugenini mbele ya USM Alger. Je! baada ya kile kilichotokea jana usiku, wataendelea pale walipoishia msimu uliopita? Hicho ndio kitendawili kilichopo kwa viongozi wa klabu hizo mbili.

Hizi ni rekodi ambazo wababe hao wa soka la Tanzania watakuwa wakizifukuzia katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo bingwa wake ni mtetezi ni Al Ahly ambaye yupo kundi D pamoja na Yanga.

POINTI NYINGI

Simba ndio klabu ya Tanzania iliyokusanya pointi nyingi zaidi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilifanya hivyo msimu wa 2020/21 tena ikiwa kundi moja (A) na Al Ahly, Mnyama alimaliza akiwa kinara wa kundi hilo huku akiwa na pointi 13 kibindoni.

Licha ya kuishia katika hatua ya robo fainali, Simba iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania katika michuano hiyo kukusanya pointi nyingi zaidi, ilishinda mechi nne, sare moja na kupoteza mara moja tu.

Hivyo msimu huu, wawakilishi hao wa Tanzania wana kibarua cha kuvunja rekodi hiyo.

BILA KUPOTEZA

Haijawahi kutokea kwa klabu ya Tanzania kumaliza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika bila ya kupoteza mchezo (unbeaten).

Msimu uliopita tulishuhudia Simba ambayo ilikuwa kundi C ikipoteza mara tatu ambapo ilikuwa dhidi ya Horoya ya Guinea ikiwa ugenini kwa bao 1-0, Wydad Casablanca mara mbili yani nyumbani (3-0) na ugenini (3-1).

MCHEZAJI BORA

Haijawahi kutokea klabu yoyote ya Tanzania kutoa mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika yote hiyo imechangiwa kutofanya vizuri kwa klabu zake kwani ili utoe mchezaji bora ni wazi timu yako inatakiwa kucheza fainali.

Anaweza kupatikana mfungaji bora katika hatua ya makundi lakini sio mchezaji bora hivyo hiki nacho kinaweza kuwa kitendawili ambacho Simba na Yanga wanatakiwa kukitegua msimu huu kulingana na ubora wa wachezaji walionao kwenye vikosi vyao.

NUSU FAINALI

Timu ya Tanzania iliyofanya vizuri zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa miaka ya hivi karibuni ni Simba tu ambayo ilifika hatua ya robo fainali mara tatu kwenye msimu wa 2022/23, 2020/21 na 2018/19.

Yanga haijawahi kuvuka hatua ya makundi, historia yake upande huu sio kubwa angalau mara kadhaa iliwahi kuibuka na kufanya vizuri upande wa Shirikisho lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo kwao kutokana na kile ambacho walifanya msimu uliopita, walionyesha kuwa hakuna ambacho kinashindikana.

Simba na Yanga zitakuwa na kibarua cha kusaka hatua ya nusu fainali na hata fainali ya michuano hiyo ambayo imekuwa na heshima ya aina yake.

USHINDI MNONO

Simba ndio klabu inayoshikilia rekodi ya kuibuka na ushindi mnono zaidi kwenye mchezo mmoja wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilifanya hivyo msimu uliopita kwa kuitandika Horoya ya Guinea mabao 7-0.

Clatous Chama aliweka kambani mabao matatu kwenye mchezo huo huku Jean Baleke na Sadio Kanoute kila mmoja akitupia mabao mawili, ilikuwa mvua ya mabao iliyokuwa ikinyesha kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Je! Ni Simba tena au Yanga itaibuka na kuvunja rekodi hiyo na nyinginezo? Ni suala la muda tu ndio ambao unaweza kuamua juu ya rekodi hizo ambazo zinaweza kuvunjwa msimu huu wa michuano hiyo ya kimataifa kwa vigogo hao wa soka

SOMA NA HII  JEMBE LA KAZI LINALOKUJA YANGA HILI HAPA