Home Habari za michezo BAADA YA WANANCHI KUSHINDWA KUTAMBA….. HAYA LEO NI MTOKO WA WENYE NCHI

BAADA YA WANANCHI KUSHINDWA KUTAMBA….. HAYA LEO NI MTOKO WA WENYE NCHI

Habari za Simba

INGEKUWA ni kadi ya mnuso, ingesomeka; “Mashabiki bora wa AFL leo wanalialika Taifa kwenye Mtoko wa Kimataifa utakaofanyika saa 10 Jioni kwenye Uwanja wa Mkapa. Usikose.”

Ni dakika 90 muhimu kwenye historia ya Simba dhidi ya Asec. Zinaweza kuijenga au kuivuruga Simba dhidi ya timu hiyo ya Ivory Coast kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wenye jukumu zito la kuhakikisha Wanasimba na Taifa linatoka na nyuso za furaha leo ni benchi la ufundi linaloongozwa na kaimu kocha mkuu Daniel Cadena na msaidizi wake Selemani Matola pamoja na wachezaji wa timu hiyo kwa kuipigania ivune pointi tatu muhimu leo.

ALSO READ
Kweli zinatisha ila zinafungika
Soka 35 min ago

Simba, Yanga ni heshima na rekodi Ligi ya Mabingwa
Soka 55 min ago

Cadena ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Akili za wachezaji ukiangalia kuanzia kwenye maandalizi ziko tofauti sana, hawaangalii mambo yaliyopita. Nguvu yao kubwa ipo kwenye mchezo huu na ninaamini tutapata matokeo mazuri kama wakitekeleza kwa vitendo kile ninachokiona kambini na mazoezini.”

Che Malone, beki wa kutumainiwa na kipenzi cha mashabiki wa Simba amesisitiza kwamba; “Tunataka ushindi muhimu na pointi tatu dhidi ya Asec tuwe na mwanzo mzuri.”

SIMBA MASTRAIKA, ASEC UKUTA

Katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti Simba imepata ushindi mara moja tu huku ikitoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja ambapo imefunga mabao saba na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Asec Mimosas wenyewe katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti, wameshinda miwili, sare mbili na wamepoteza mmoja huku wakifunga mabao matatu na wenyewe wamefungwa mabao mawili.

Kumbukumbu ya mechi 10 zilizopita za mashindano tofauti ya kimataifa ambazo Simba ilikuwa nyumbani, inaonyesha kuwa iliibuka na ushindi mara saba, kutoka sare kwenye mechi mbili na kupoteza mchezo mmoja huku ikifunga mabao 19 na yenyewe imeruhusi mabao matano tu.

Wageni wao Asec Mimosas wanaonekana sio wanyonge ugenini ingawa hawajapata ushindi mara nyingi ambapo katika mechi 10 zilizopita za kimataifa walizocheza nje ya nyumbani, wameshinda tatu, kutoka sare tatu na kufungwa michezo minne, wamefunga mabao sita na nyavu zao zimetikiswa mara 11.

MBINU, KIKOSI

Simba inapaswa kuwa makini zaidi na safu ya kiungo ya Asec Mimosas ambayo kwa muda mrefu imekuwa ndio uti wa mgongo wa timu hiyo katika kujenga mashambulizi na kuilinda safu ya kiungo na iwapo ikifanikiwa hapo, inaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kupata ushindi leo.

Safu ya ushambuliaji ya Simba itaendelea kuwa tegemeo kubwa la Cadena na benchi lake la ufundi kutokana na makali ya kufumania nyavu ambayo imeyaonyesha msimu huu.

Wenyeji hata hivyo wanatakiwa kuepuka ufanyaji wa makosa ya mara kwa mara katika eneo la ulinzi ambayo yameonekana kuigharimu msimu huu kwa kuruhusu bao/mabao katika idadi kubwa ya mechi msimu huu.

Kikosi cha Simba leo kinaweza kuundwa na Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Che Fondoh Malone, Enock Inonga, Sadio Kanoute, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Jean Baleke, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

UGOMVI WA KIHISTORIA

Kihistoria, Simba na Asec zimekutana mara sita kwenye mashindano ya Klabu Afrika na hii itakuwa ni mara ya saba kwa timu hizo mbili kuumana ambapo Asec ameonekana kutamba kwa kupata ushindi katika mechi nne huku Simba ikipata ushindi mara mbili, matokeo ambayo yanamaanisha kuwa sare huwa ni ngumu kupatikana pindi zinapocheza.

Katika mechi hizo sita zilizopita baina yao, Asec ilifumania nyavu mara 12 wakati Simba yenyewe imefunga mabao tisa tu.

Mechi ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni Machi 20, 2022 ambapo Simba ilipoteza ugenini dhidi ya Asec Mimosas kwa mabao 3-0 katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa L’Amitié uliopo Benin.

REFA WA MECHI

Refa asiye na mzaha kwa wacheza rafu na wachezaji watovu wa nidhamu, Mohamed Maarouf Eid Mansour kutoka Misri ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo baina ya Simba na Asec Mimosas.

Maarouf mwenye umri wa miaka 37, katika mechi 11 tu za mashindano ya klabu Afrika ambazo amechezesha, ameonyesha idadi ya kadi 46 ikiwa ni wastani wa kadi nne (4) kwa mchezo ambapo kati ya hizo, 43 ni za njano na tatu ni nyekundu.

Simba wana kumbukumbu nzuri na refa Maarouf kwani alikuwa mezani wakati walipoichapa Horoya kwa mabao 7-0 katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita wakati Asec Mimosas wana historia mbaya naye kwani amewachezesha mechi moja tu ambayo walichapwa bao 1-0 nyumbani na Raja Casablanca kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Julai 18, 2018 katika mchezo ambao nyota wao mmoja alionyeshwa kadi nyekundu.

Mwamuzi huyo atasaidiwa na Samir Saad na Youssef Elbosaty na mwamuzi wa mezani Mahmoudy Mosa wote kutoka Misri.

Kamishna wa mchezo huo ni Francis Oliele na mtathmini wa marefa ni Sylvester Kirwa wote kutoka Kenya.

SOMA NA HII  MMH HII SASA KUFURU...MABOSI WA SIMBA WAINGIA KAMBINI NA TIMU