Home Habari za michezo AL AHLY WASHIKILIA HESHIMA YA YANGA…. UONGOZI WAFUNGUKA HAYA

AL AHLY WASHIKILIA HESHIMA YA YANGA…. UONGOZI WAFUNGUKA HAYA

Habari za Yanga

Klabu ya Yanga imesema mechi ya Jumamosi dhidi ya Al Ahly imeshikilia heshima yao kwani kama ikiibuka na ushindi itapata sifa kubwa barani Afrika na pia itarudisha matumaini yao na malengo ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Akizungumza Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema walikuwa Unguja kwa ajili ya kupata baraka kutoka kwa wazee, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa ajili ya mechi ya Jumamosi itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Tulikuwa Zanzibar kwa ajili ya kupata baraka, kuelekea katika mechi yetu dhidi ya Al Ahly, ni mchezo mkubwa ambao umeshikilia heshima yetu barani Afrika, ni mpinzani mkubwa, hivi karibuni anakwenda kucheza Klabu Bingwa Dunia, atakwenda kucheza na klabu kubwa barani Ulaya kama Manchester City na nyinginezo, maana yake huyu ni mpinzani sahihi kwetu na ataiheshimisha klabu yetu kama tukipata matokeo mazuri,” alisema Kamwe.

Itakuwa ni mechi ya pili ya Yanga kwenye Kundi D, baada ya ile ya awali iliyopita kupokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad nchini Algeria na inahitaji ushindi ili irudi kwenye reli ya kuelekea hatua ya robo fainali. Al Ahly, ikiwa nyumbani Jumamosi iliyopita nayo iliichakaza Medeama ya Ghana mabao 3-0.

Mabingwa hao watetezi, Al Ahly, wapo juu kileleni mwa msimamo wa kundi hilo kialfabeti tu, wakiwa sawa kwa kila kitu na CR Belouizdad iliyo kwenye nafasi ya pili, huku Yanga nayo ikiburuza mkia kialfabeti pia kwani iko sawa kila kitu na Medeama iliyokaa nafasi ya tatu.

Wakati huo huo, Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi Said, amesema Klabu ya Yanga ni ya watu wote Bara na Visiwani, hivyo hafurahishwi na wale wanaoiita Dar es Salaam Young African, badala yake anataka iitwe Young African au Yanga.

Akizungumza wakati akifungua Tawi la Yanga, Taveta Mjini Unguja, Hersi alisema kitendo cha kuiita Yanga kwa jina la Dar es Salaam Young African, kunakuwa na dhana kwamba ni ya watu wa Dar tu.

“Hii inaitwa Young African, kwa kifupi ni Yanga na siyo Dar es Salaam Young African kama inavyoitwa na baadhi ya wanachama, mashabiki, wadau wa michezo na hata vyombo vya habari.

“Nini maana yake, ni kwamba hii klabu ya kwetu wote na wala si ya watu wa Dar es Salaam tu na pia kila tawi hapa nchini lina nafasi sawa na matawi yote Tanzania,” alisema.

SOMA NA HII  SIMBA IMESHAKUWA JANGA MO DEWJI AOGOPA KUFA KWA PRESHA