Home Habari za michezo BENCHIKHA AWATULIZA WANASIMBA AFUNGUKA HAYA

BENCHIKHA AWATULIZA WANASIMBA AFUNGUKA HAYA

Habari za Simba

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amewatuliza wanachama na mashabiki wa klabu hiyo akisema nafasi ya kwenda robo fainali kutoka Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ipo hasa kwa mabadiliko ndani ya kikosi hicho yakitokana na ubora wa mbinu anazowapa nyota wake.

Benchikha ameiongoza Simba katika mechi nne tofauti zikiwamo tatu za CAF na moja ya Ligi Kuu Bara akishinda mbili, kupoteza moja na sare moja aliyoanza nayo ugenini dhidi ya Jwaneng Galax ya Botswana.

Mechi ya pili kwake na aliyopoteza ni ile ya ugenini Morocco dhidi ya Wydad Casablanca, kisha kushinda dhidi ya Kagera Sugar katika Ligi Kuu na juzi kuifumua Wydad kwenye mechi ya marudiano ya CAF kwa mabao 2-0 na kupagawisha mashabiki na wapenzi wa Simba waliokuwa wanyonge tangu timu hiyo ifungwe mabao 5-1 na Yanga.

Ushindi wa juzi umeifanya Simba kufufua matumaini ya kutinga robo fainali na Benchikha aliliambia Mwanaspoti kuwa hakuna miujiza anayofanya kwa sasa kwani timu ni ileile iliyoachwa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ila alichoongeza ni mbinu zilizoanza kuzaa matunda.

“Sijafanya kazi kubwa kuibadilisha kilichobadilika ni mbinu na uelewa wa wachezaji ninaofanya nao kazi. Nafurahi kuona wadau wa soka wameona utofauti nitaendelea pale nilipoishia lengo ni kufikia malengo na niwatoe hofu kwamba robo fainali inatuhusu tukiendelea hivi,” alisema.

“Wachezaji ni wale wale kila mmoja ana umuhimu wake kutokana na aina ya timu tunayokutana nayo. Mfano leo (juzi) tumekutana na timu yenye uzoefu mkubwa na imeshatwaa mataji ya kimataifa walikuja na mbinu ngumu baada ya kufanikiwa kutegua mtego wao na kupata matokeo nasi tukaingia na mbinu kabambe zilizotubeba.”

Benchikha amesema kutokana na aina ya kikosi alichonacho mbinu zaidi ndio zitambeba na kumpa mafanikio hii ni baada ya kumsaidia kwa muda mfupi aliokaa na timu hiyo ambayo amekiri kuhitaji kuwekeza nguvu ili aweze kufikia malengo.

“Tumefanikiwa kuvuka hatua chache na nimeanza kuona picha ya nini kiendelee kufanyika zaidi ili kuweza kuwa bora na washindani nafurahi kuona matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali yamekuwa makubwa,” alisema. Simba inarejea Ligi Kuu ikitarajiwa kucheza na KMC wikiendi kabla ya kuifuata Mashujaa wiki ijayo na kumalizana na Tabora United kabla ya kwenda Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na Februari 24 itacheza mechi ya CAF ugenini dhidi ya vinara wa Kundi B, Asec Mimosas wenye pointi 10 kisha kumaliza kwa kuvaana na Jwaneng Galaxy ya tatu ikiwa na pointi nne.

SOMA NA HII  SAKATA LA KURUDISHWA YANGA NA TFF...UPANDE WA FEI TOTO WAIBUKA NA HILI JIPYA...