Home Habari za michezo CAF KUAMUA HATMA YA USAJILI SIMBA NA YANGA….MASTAA HAWA HATARINI KUFYEKWA….

CAF KUAMUA HATMA YA USAJILI SIMBA NA YANGA….MASTAA HAWA HATARINI KUFYEKWA….

Habari za Michezo

USAJILI wa dirisha dogo ni kama umezitega Simba na Yanga, kwani unazilazimisha kushinda michezo yao inayofuata ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba na Yanga kwa mara ya kwanza zipo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ina pointi mbili tu kati ya sita, baada ya kutoka suluhu dhidi ya Jwaneng Galaxy na sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec Mimosas, huku Yanga ikiambulia pointi moja kati ya sita baada ya kufungwa na Belouizdad mabao 3-0 na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly.

Wikiendi ijayo zote zipo ugenini zikitafuta ushindi kwenye michezo yao muhimu ambayo itawaweka kwenye wakati mzuri wa kufuzu hatua ya robo fainali, Simba watavaana na Wydad Casablanca ya Morocco Jumamosi, huku Yanga wakikipiga na Medeama Ijumaa.

Hata hivyo, pamoja na kwamba vikosi vya timu zote mbili vimeonekana kuwa na upungufu, lakini usajili wao bora kwenye dirisha hili umeshikiliwa na michezo miwili inayofuata Simba mmoja na Yanga mmoja, bila hiyo watasajili kumalizia msimu wa ndani.

YANGA STRAIKA, KIUNGO:

Imepata wakati mgumu kimataifa msimu huu baada ya kukosa mshambuliaji wa uhakika kutoka na Hafidhi Konkoni, Kennedy Musonda na Clement Mzize kushindwa kumshawishi kocha Miguel Gamondi, sasa ni rasmi kuwa kocha huyo atasajili mshambuliaji kwenye dirisha hili.

Ranga Chivaviro wa Kaizer Chief anatajwa kumalizana na Yanga. Timu hiyo itahaha kumpata mshambuliaji mkubwa kutoka kwenye timu nyingine ambazo hazijashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kuwa kanuni haimruhusu mchezaji kuzichezea timu mbili kwenye michuano hiyo, endapo tu itakuwa na uhakika wa kwenda robo fainali.

Hivyo wakati usajili unafunguliwa Desemba 16, tayari Yanga itakuwa imeshavaana na Medeama Desemba 8, mchezo huu utaipa picha halisi ya kama ina nafasi ya kusonga mbele au hapana.

Endapo Yanga itashinda mchezo huu, itafikisha pointi nne na kubakiza michezo mitatu ambayo ina pointi 9, lakini miwili kati ya hiyo itakuwa nyumbani.

Hivyo ili Yanga isajili mshambuliaji mkubwa inatakiwa kushinda mchezo huu hali ambayo itamfanya kocha wa timu hiyo atafute staa ambaye anaweza kuwavusha kwenye michezo mitatu inayofuata, dhidi ya Medeama Desemba 20, Belaouzdad Februari 23 pamoja na ule dhidi ya Al Ahly Machi 1.

Hata hivyo, hali inaweza kuwa tofauti kwa Yanga, endapo watapoteza mchezo dhidi ya Medeama kwa kuwa matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali yatafifia, hivyo timu hiyo itapunguza kasi ya mshambuliaji mkubwa ikiamini kuwa inaweza kumpata yule aliye bora zaidi kwenye dirisha kubwa la Julai na waliopo wanaweza kusaidia kwenye ligi.

Hii ni kwa kuwa wachezaji wengi wakubwa huwa sokoni kwenye dirisha kubwa kuliko dirisha dogo ambalo timu nyingi huwa kwenye mipango nao na hata bei za mastaa hao huwa juu.

Mbali na eneo hilo, Yanga inalazimika pia kumsajili beki mmoja wa kati baada ya Gift Fred ambaye alisajiliwa kwenye kipindi kilichopita kushindwa kuonyesha makali yake, huku pia ikionekana inaweza kuongeza kiungo mkabaji atakayesaidiana na Khalid Aucho ambaye amekosa mbadala sahihi.

SIMBA KUNDI KUBWA:

Hali ilivyo kwa Yanga haina tofauti kubwa na Simba ambayo kwenye michezo miwili imekusanya pointi mbili hadi sasa na itapata kitita cha dola 700,000, sawa na bilioni 1.7 kutokana na kutinga hatua ya makundi.

Simba inacheza na timu yenye rekodi kubwa kwenye michuano hii, Wydad mchezo utakaopigwa Jumamosi ijayo, siku saba kabla dirisha halijafunguliwa.

Salim Abdallah ‘Try Again’ ameweka wazi kwamba safari hii wanaingia sokoni kwa nguvu ingawa hakuweka wazi bajeti yao. Simba inatajwa kuwa timu ambayo itafanya usajili mkubwa kwenye kipindi cha Januari na dirisha kubwa, lakini mtego wa timu hiyo pamoja na kelele nyingi hauna tofauti kubwa na Yanga.

Simba inatakiwa kuhakikisha angalau inapata pointi tatu au moja dhidi ya Wydad ili kuwa na matumaini ya kufuzu robo, hali ambayo itawalazimu kuingia sokoni kupata mastaa ambao watakuwa tayari kwa ajili ya michezo mitatu iliyobaki, lakini endapo haitapata pointi maneno yatakuwa tumalize msimu, tusajili dirisha kubwa.

Simba ikipata japo pointi moja kwa Wydad, itatakiwa kushinda michezo yake miwili ya hapa nyumbani na kufikisha pointi tisa ambazo zinaweza kuwabeba ingawa wakipata 10 wanakuwa salama zaidi.

Ikipata tatu itakuwa na tano ambazo zitawalazimu kufanya usajili wa mastaa watakaowasaidia kutafuta pointi tano kati ya tisa na kufuzu moja kwa moja.

Simba chini ya Benchikha inalazimika kusajili karibu maeneo yote ya uwanja, eneo la ulinzi wa kati, pembeni kote, kiungo mkabaji, winga zote pamoja na mshambuliaji, lakini pia hali ya kipa Aishi Manula inaweza kuwalazimisha kuingia sokoni kutafuta kipa atakayesaidiana na Ayoub Lakred ambaye sasa ni uhakika kwamba atabaki.

Hata hivyo, kupata wachezaji wote kwenye dirisha la Januari ni jambo gumu kwa kuwa unaotakiwa kusajili ni lazima wawe hawajacheza Ligi ya Mabingwa msimu huu, au usajili ambaye huwezi kumtumia kwenye michuano hiyo jambo ambalo siyo sahihi kwa Simba kama watakuwa wamepata pointi kwa Medeama Desemba 8.

CREDIT:- MWANASPOTI

SOMA NA HII  HUYU HAPA KIUNGO MKATA UMEME ANAYETAJWA KUTUA SIMBA...ANAKIPIGA TIMU YA TAIFA YA NIGERIA...ANABALAA HUYOOO...