Home Habari za michezo YANGA WABORESHA KIKOSI KAZI, WAMBA WATATU HAWA HAPA KUTUA JANGWANI

YANGA WABORESHA KIKOSI KAZI, WAMBA WATATU HAWA HAPA KUTUA JANGWANI

Kikosi cha Yanga kimerejea jijini Dar es Salaam kutoka Kumasi, Ghana ilipoenda kucheza mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Medeama na kutosha nguvu kwa kufungana bao 1-1, lakini mabosi wa klabu hiyo wameamua kufumua usajili mpya wa timu hiyo tofauti na ule waliokuwa wameupanga.

Uamuzi wa mabosi wa Yanga kupitia benchi la ufundi awali lilipanga kusajili mashine kama mbili tu katika dirisha dogo litakalofunguliwa wiki ijayo, lakini dakika 90 za mechi ya nyumbani dhidi ya Al Ahly imewabadilisha kila mmoja.

Mechi hiyo iliyopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliisha kwa sare ya 1-1 kwa mabao ya jioni, Pacome Zouzoua akiisawazisha Yanga na mara baada ya mchezo huo mabosi wa Yanga waliamua kurudi mezani na kufumua hesabu za usajili kibabe ili kuweka mizani sawa kwa kila idara ya timu hiyo.

Hesabu za awali ilikuwa ni Yanga kushusha mashine mpya mbili tu hivi akiwemo mshambuliaji mmoja wa kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni aliyeshindwa kuziba vyema pengo la Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri pamoja na winga mwenye kasi lakini Al Ahly ikawazindua mabosi hao na kupiga hesabu upya.

Habari kutoka ndani ya Yanga ni kwamba hesabu mpya za sasa ni mabosi wa klabu hiyo wameongeza idadi zaidi ya wachezaji hadi kufikia wanne, wakiwamo washambuliaji wawili baada ya mmoja kama walivyokuwa wamepanga awali.

Mbali na washambuliaji wawili, pia Yanga inataka winga na kiungo wa kati anayeweza kumudu ukabaji na hata ushambuliaji kwa nia ya kuongeza wigo mpana kwenye eneo hilo ambalo kwa sasa lina vichwa kadhaa wakiongozwa na Khalid Aucho.

Yanga iko tayari kukata watu wanne wa kigeni kwenye kikosi cha sasa ili kuweza kupata nafasi za maingizo hayo mapya ambayo wanayaona yanahitajika.

“Unajua ile mechi ya Al Ahly kila kitu kilionekana, kuna muda tuliona Stephane Aziz KI amechoka na hata Maxi Nzengeli lakini ukiangalia nje hupati jibu sawasawa la nani aingie na hapo kuna wachezaji wa kigeni unao wako hapo,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga aliyeongeza;

“Unajua unapokuwa na wachezaji wa kigeni wanatakiwa kukusaidia nyakati kama hizo, kwa hiyo tumeona hiyo changamoto na sasa tunahangaika kutafuta watu bora zaidi ambao watawapa makocha wetu afya ya kuamua haraka wanapoona waliopo uwanjani wameshindwa kucheza kwa ubora.

“Tulishasema hii sio timu ya kumsubiri mtu ambaye ameshindwa kuonyesha makali kama tutaona kuna watu wanashindwa kwenda na kasi yetu tutatafuta wengine kwa haraka.”

Kwenye mchezo huo wa Ahly ulioisha kwa sare ya 1-1 Yanga haikuwatumia wachezaji wanne wa kigeni beki Gift Fred, mshambulaiji Hafiz Konkoni, winga Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ huku winga mwingine Jesus Moloko akiwa juu jukwaani akidaiwa ni majeruhi.

Timu hiyo juzi usiku ilikuwa ugenini mjini Kumasi kucheza na Medeama na kutoka pia sare ya 1-1, huku Yanga ikisawazisha kupitia Pacome Zouzoua aliyetimiza mabao mawili kwenye michuano hiyo ambayo mabingwa hao wa Tanzania wanaburuza mkia kundini ikiwa na pointi mbili baada ya kucheza mechi tatu hadi sasa.

SOMA NA HII  WYDAD WAJIPANGA KUISHAMBULIA SIMBA KWA KASI...KOCHA ACHEZE NA PLAN B