Home Habari za michezo GAMONDI AJA NA MBINU HIZI KUELEKEA ROBO FAINALI

GAMONDI AJA NA MBINU HIZI KUELEKEA ROBO FAINALI

Habari za Yanga

Wakati Kocha Mkuu wa Yanga, akianika mikakati yake kuelekea mechi mbili za nyumbani za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama FC na CR Belouizdad, wachezaji wa timu hiyo wamesema nao wamepania kupambana hadi tone la mwisho la hatua hiyo ya makundi.

Aidha, Gamondi amesema atatumia mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar kusaka pointi tatu pamoja na kuwapa mbinu wachezaji wake kwa ajili ya kuwinda alama sita zitakazofufua matumaini yao ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi cha Yanga kimereje nchini tayari kujiandaa kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumamosi wiki hii kabla ya Jumatano ya wiki ijayo kuikaribisha Medeama FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo uliopita, Yanga ililazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Waghana hao, hivyo kufikisha pointi mbili, matokeo ambayo yanaifanya kuburuza mkia kwenye Kundi D, linaloongozwa na Al Ahly ya Misri ikiwa na alama tano ikifuatiwa na Medeama na Belouizdad ya Algeria ambazo kila moja ina pointi nne.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Gamondi alisema licha ya kuwapo kwa mchezo mgumu kutafuta alama tatu muhimu, lakini hawawezi kusahau mechi ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo ni muhimu kushinda kwa ajili ya kufikia malengo yao mama kwa msimu huu.

Alisema anatambua umuhimu wa kila mchezo, baada ya mechi yao dhidi ya Medeama FC, wamerejea kujiandaa dhidi ya Mtibwa Sugar lakini wakitarajia kutumia mechi hiyo kama maandalizi ya mchezo huo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunatambua tuna mechi mbili nyumbani na tunahitaji kuvuna alama zote sita, dhidi ya Medeama FC na CR Belouizdad, kabla ya mchezo huo tunakibarua kigumu mbele yetu dhidi ya Mtibwa Sugar, tunatakiwa kushinda kabla ya kucheza michezo miwili ya kimataifa.

“Kabla ya kuanza kutafuta alama sita Ligi ya Mabingwa Afrika, lazima tuhakikishe tunafanya vizuri mechi iliyopo mbele yetu ya ligi, wachezaji wanatakiwa kufikiria kilichopo mbele yetu ambayo Mtibwa Sugar, mchezo huu unatusaidia kujiandaa dhidi ya Medeama FC nyumbani kuvuna alama tatu muhimu,” alisema.

Wakati huo huo wachezaji wa Yanga walisema wamerejea nyumbani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo ujao kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia malengo ambayo yanatarajiwa ikiwamo kwenye ligi na michuano ya kimataifa.

Kiungo wa timu hiyo, Khalid Aucho, alisema mechi ilikuwa ya ushindani na benchi la ufundi litafanyia kazi mapungufu yao na anaimani katika mechi iliyopo mbele yao ya ligi wataitumia kama sehemu ya maandalizi dhidi ya Medeama.

“Tumerudi kujiandaa na mchezo wetu huo, bado haijafika mwisho hadi iwe mwisho, nafasi ya kucheza robo fainali ipo wazi kwa sababu tuna mechi mbili nyumbani ambazo tunaweza kusaka alama sita na kuvuka kwenye hatua hiyo,” alisema Aucho.

Aliongeza kuwa watahakikisha wanapambana hadi mwisho ili kupata matokeo mazuri na kuwaomba mashabiki kujitokeza uwanjani kuendelea kuwapa sapoti katika kila hali wanayopitia hasa michuano ya kimataifa.

SOMA NA HII  RASMI...AL AHLY WAILAINISHIA SIMBA KWA MIQUISSONE...MABOSI MSIMBAZI WAPAGAWA NA MSHAHARA WAKE...