Home Habari za michezo HIKI KIKOSI CHA SASA TAIFA STARS SIO POA

HIKI KIKOSI CHA SASA TAIFA STARS SIO POA

Taifa Stars leo

Muda wowote kuanzia sasa magari ya maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yatakuwa yanapishana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kuwapokea wachezaji wa kimataifa wa Tanzania ambao watakuwa wakitua kuripoti kambini tayari kuanza maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Tanzania ni kati ya mataifa 24 ambayo yatapigania ufalme wa Afrika huko Ivory Coast ambako fainali hizo zitafanyika Januari 13 hadi Februari 11 mwakani kwa mara ya 34 huku ikiwa mara ya pili kwa taifa hilo kuwa mwenyeji, mara yao ya kwanza ilikuwa 1984.

Tofauti na awamu zilizopita kikosi cha sasa cha Taifa Stars ambacho kinanolewa na Mualgeria, Adel Amrouche, kimeita wachezaji wa awali 53 wakiwamo idadi kubwa ya wachezaji wa Kitanzania ambao wanacheza soka la kulipwa katika mataifa yaliyoendelea zaidi.

Na bila ya shaka wachezaji wenye asili ya Tanzania wenye uraia wa nchi nyingine sasa wanavutika kuja kuchezea Taifa Stars kwa sababu hawalazimiki tena kuukana uraia wa mataifa wanakoishi kutokana na serikali kuwarahisishia mambo kwa hati maalum ya uraia pacha.

Haya ni maingizo mapya matano ambayo yanaweza kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Amrouche kulingana na kile ambacho wamekuwa wakikifanya kwenye klabu zao.

AMAHL PELLEGRINO

Huyu ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Norway ‘Eliteserien’, ambaye anaichezea Bodo/Glimt ya nchini humo ni miongoni mwa washambuliaji hatari mwenye wastani mzuri wa kutumia nafasi, anaweza kucheza kama winga wa kulia au kushoto na hata namba tisa au 10.

Pellegrino ambaye amezaliwa na kukulia Norway, alikuwa akipigiwa debe na wadau mbalimbali wa soka la Tanzania kufuatia kufanya kwake makubwa kuanzia kwenye ligi za ndani Norway hadi upande wa michuano ya Ulaya ambayo Bodo/Glimt imekuwa ikishiriki na kufanya vizuri.

Akiwa na Bodo/Glimt, msimu uliopita nyota huyo mwenye asili ya Zanzibar alikuwa mfungaji bora wa Eliteserien baada ya kumaliza msimu akiwa na mabao 24 ambayo yaliisaidia timu yake kuchukua ubingwa wa ligi. Pia ni kati ya wachezaji muhimu ambao wameifanya Bodo/Glimt kutinga mtoano wa Europa Conference League baada ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi.

ZION NA ROBERTO

Hawa ni wadogo zake nyota wa zamani wa Chelsea, Adam Nditi ambaye alipotea kwenye soka la ushindani kama utani licha ya kuwa kwenye nafasi ya kufanya makubwa. Mbali na hao ambao wameitwa kwenye kikosi cha Amrouche yupo mwingine mdogo wao wa mwisho ambaye naye ni mwanasoka anaitwa, Paulo (aliyezaliwa 2005).

Wadogo zake hao watatu walianza maisha yao ya soka katika akademi ya Reading kabla ya kila mmoja baada ya kukua kwenda kutafuta malisho sehemu nyingine, Roberto ambaye ni beki wa kulia anacheza soka la kulipwa Scotland akiwa na Forfar Athletic ambayo inashiriki ligi daraja la tatu nchini humo.

Zion naye ni beki wa kulia kama ilivyo kwa kaka yake, Roberto ila yeye aliamua kuendelea kukomaa England, ni kati ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Aldershot Town.

ADAM KASA

Ni beki wa kushoto mwenye uwezo mkubwa wa kupanda na kushuka, baada ya kuwa na shauku kwa kipindi kirefu kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars hatimaye ndoto yake hiyo imetimia na kilichosalia ni kuonyesha kuwa amestahili nafasi hiyo.

Adam anacheza soka la kulipwa Sweden akiwa na IFK Haninge na mara kwa mara amekuwa akizitumia likizo zake kuponda raha Tanzania kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya utalii na msimu uliopita alikuja nchini akiwa na marafiki zake.

Akiongelea fursa aliyoipata, beki huyo aliyezaliwa Februari 22, 1993 anasema, “Kwangu ni heshima iliyoje kwa sababu kwa miaka mingi nimekuwa nikitamani kupata nafasi ya kuichezea Tanzania lakini nashukuru sana TFF kwa juhudi ambazo wamefanya, nimekuwa na wakati mzuri wa kufanya mazungumzo na kocha ambaye ameonyesha kuwa na uhitaji na mimi.”

AYOUB BILALI

Ni kiungo mwenye uwezo wa kucheza kama mkabaji, mchezeshaji au mshambuliaji. Juni mwaka huu mkataba wake ulifikia ukomo wa kuichezea FK Gorazde ya Bosnia. Bilal ni mchezaji kijana ambaye ana uzoefu wa kucheza soka la kulipwa Ulaya, hivyo atatoa changamoto ya namba kwa wakongwe kwenye kikosi cha Stars.

KIKOSI CHA AWALI

Makipa: Beno Kakolanya (Singida Big Stars), Aishi Manula (Simba SC), Aboutwaleeb Mshery na Metacha Mnata (Yanga), Kwesi Kawawa (IFK Haninge).

Mabeki: Nickson Kibabage, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdallah (Yanga), Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Haji Mnoga na Zion Nditi (Aldershot Town), Abdi Banda (Richards Bay), Novatus Dismas (Shakhar Donetsk), Edwin Charles Balua (Prisons), Abdulmalik Zakaria (Namungo), Roberto Nditi (Forfar Athletic), Adam Kasa (IFK Haninge), Mohamed Hussein, Kennedy Juma na Israel Patrick (Simba SC), Elias Lawi (Coastal Union)

Viungo: Omar Abbas Mvungi (Nantes), Mzamiru Yassin (Simba SC), Feisal Salum na Sospeter Bajana (Azam), Baraka Majogoro (Chippa United), Mudathir Yahya (Yanga), Morice Abraham (RFK Novi Sad), Himid Mao (Talaea El Gish), Ladaki Juma (Mtibwa Sugar), Kokola Charles M’mombwa (Macarthur), Khleffin Hamdoun (Muscat), Adolf Bitegeko (Volsungur), Yusuph Kagoma (Singida Big Stars), Abdul Suleiman (Azam FC), Ben Starkie (Basford, Ayoub Bilali (FK Gorazde), Tarryn Allarakhia (Wealdstone), Miano Danilo (Telford United), Twariq Abdallah (Telford United), Mark Kwarteng (Kingston), Mohamed Ali omar (Borehamwood)

Wadhambuliaji: Mbwana Samatta (PAOK), Saimon Msuva (JS Kabylie), Kibu Denis (Simba SC), Matheo Antony (Mtibwa Sugar), Joshua Ibrahim (Tusker FC), Clement Mzize (Yanga SC), Adam Salamba (Ly stade club), Pellegrino Ahmal (Bodo), Said Khamis (FK Jedinstvo), Cyprian Kachwele (Vancouver Whitecaps FC 2).

SOMA NA HII  UNAAMBIWA SHABIKI AKIMBIA OFISI YAKE NA KUHAMA NYUMBA KISA GOLI TANO ZA YANGA