ACHANA na ubora wa kipa wa Simba, Ayoub Lakred aliouonyesha jana habari ya mjini ni mbinu za kijeshi za kocha wa timu hiyo Belhack Benchikha na ubora wa Willy Onana.
Simba ikiwa kwenye Uwanja wa Mkapa ilionyesha kiwango cha hali ya juu na kufanikiwa kuichapa Wydad Casablanca mabao 2-0, ukiwa ni ushindi wake wa kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi msimu huu.
Onana mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki wa Simba walikuwa wakilalama kila siku kuwa hawamuelewi, jana alieleweka baada ya kuweka mabao yote mawili kambani, la kwanza alifunga katika dakika ya 36 baada ya kupata pasi safi toka kwa Kibu Denis, dakika mbili baadaye akaweka bao la pili kwa ufundi wa hali ya juu kwa pasi safi toka kwa Mzamiru Yassin, ambaye alipata mpira toka kwa Clatous Chama.
Sasa Simba imefufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali, baada ya kufikisha pointi tano kwenye michezo mitatu iliyocheza, kabla ya mchezo wa jana kati ya Asec na Jwaneng ilikuwa nafasi ya pili nyuma ya Asec sasa inatakiwa kushinda michezo yake miwili iliyobaki, dhidi ya Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy ambapo itafikisha pointi 11 na kufuzu bila kutazama matokeo ya mwingine.
Mbinu za Kijeshi za Benchikha
Kwa mara ya kwanza kocha wa Simba Benchikha amewaonyesha mashabiki ni jinsi gani ana mbinu kali kwenye soka, kwanza ni jinsi Simba ilivyokuwa inacheza kwa umakini bila kupoteza mpira na hata walipokuwa wakipoteza walihaha haraka na kuupokonya, huku kila mchezaji akionekana kuwa na pumzi ya kutosha.
Lakini achana na hilo mbinu kali ya kijeshi ya Benchikha ilionekana kuanzia dakika ya 60 baada ya kumuingiza mshambuliaji John Bocco na kuwatoa wachezaji wengine wote wa eneo la ushambuliaji na kuanza kuingiza mabeki, ambapo dakika ya 77, timu yake ilicheza ikiwa na watu tisa wanaolinda, mshambuliaji mmoja na kipa pekee.
Benchikha alimtoa Chama nafasi yake ikachukuliwa na Israel Mwenda, akamtoa Kibu akaingia David Kameta, Abdallah Hamis aliingia kuchukua nafasi ya Mzamiru huku Baleke na kuingia Keneddy Juma.
Hii ni mara ya kwanza inaonekana kwenye timu ya Simba, Simba ikicheza na Fabrice Ngoma, Inonga, Che Malone, Israel Mwenda, Duchu, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Mohammed Kazi na kipa Ayoub. ikiwa ni mbinu pekee ya kulinda ushindi wake wa mabao mawili.
Baada ya kuingiza mabeki hao ambao wanne walikuwa wakicheza pembeni na wanne katikati, Wydad walifika langoni mwa Simba mara saba, lakini zote hakukuwa na madhara, huku mabeki wote wakifanya kazi kubwa ya kuokoa hatari, hata hivyo pamoja na kuwa na walinzi wengi Simba ndiyo walikosa nafasi ya wazi katika dakika ya 90 baada ya Inonga kushindwa kuuweka mpira kimiani ukatolewa na kuwa kona.
“Tunashukuru kwa kuwa tumepata ushindi napenda kuwapongeza wachezaji wangu wote kwa juhudi zao walizozionyesha, sasa tunajipanga kwa ajili ya michezo mingine,” alisema Benchikha baada ya mechi.
Ayoub Lakred, Onana mastaa
Pamoja na Onana kufunga mabao hayo mawili, lakini ni dhahiri kuwa kazi kubwa sana kwenye mchezo huo ilifanywa na kipa Ayoub Lakred ambaye kipindi cha kwanza tu alifanikiwa kuokoa michomo mitano ambayo kama siyo umakini wake basi Simba ingeenda mapumziko kwa majonzi.
Hata hivyo kwa upande wa Onana, alikuwa shujaa kwenye mchezo huo akiwa amefunga mabao yake ya kwanza akiwa na Simba, lakini akiwa mchezaji wa kwanza kwa timu hiyo kufunga mabao mawili kwenye hatua ya makundi katika Uwanja wa Mkapa, mbali na kufunga lakini alifanikiwa kuonyesha kiwango cha juu, huku akipiga mashuti manne kwa dakika alizokaa uwanjani, kikiwa ni kiwango tofauti na huko nyuma.