Home Habari za michezo JAMANI KUMBE GUARDIOLA NI MTU KAMA WATU WENGINE

JAMANI KUMBE GUARDIOLA NI MTU KAMA WATU WENGINE

Hakuna ubishi kwamba Pep Guardiola ni moja ya makocha bora kabisa kwenye historia ya mchezo wa mpira wa miguu, lakini si mara zote amekuwa akifahamu namna bora ya kupata huduma bora kutoka kwa wachezaji wake.

Mhispaniola huyo ameshinda mataji 38 katika maisha yake na bila shaka amekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha viwango vya wachezaji wadogo na wakubwa kwenye timu zote alizowahi kuzinoa Barcelona, Bayern Munich na Manchester City.

Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali zimethibitisha kwamba Guardiola naye ni mwanadamu, si wachezaji wote wanaokuwa kwenye timu yake amekuwa na uwezo wa kuwafanya kuwa bora ndani ya uwanja.

KALVIN PHILLIPS

Kwa kawaida imekuwa ikiwachukua wachezaji hadi miezi 12 kuwa sawa chini ya kocha Guardiola, lakini mwaka sasa umepita na Phillips hana maajabu huko Etihad tangu aliposajiliwa kwa Pauni 42 milioni kutoka Leeds United.

Phillips ameshindwa kumshawishi kocha Guardiola kwa maana ya kumfanya acheze kwenye kiwango kikubwa na matokeo yake amejikuta akiwekwa benchi na kiungo Rodri. Phillips amecheza dakika 645 tu chini ya Guardiola kwenye kikosi cha Man City.

MARIO GOTZE

Kiungo wa Kijerumani, Gotze alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Guardiola baada ya kutua huko Bayern Munich, akimnyakua kutoka Borussia Dortmund mwaka 2013. Staa huyo alibeba mataji saba akiwa na Bayern, lakini kocha Guardiola alishindwa kabisa kumfanya Gotze kucheza kwenye kiwango bora kabisa cha soka lake. Licha ya kwamba alifunga mabao 36 katika mechi 114 alizocheza chini ya Guardiola, Gotze alishindwa kuwa kwenye kiwango bora cha soka lake akiwa na Mhispaniola huyo

MEDHI BENATI

Guardiola alilipa karibu Pauni 22 milioni kumnasa Benatia kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi la mwaka 2014 na wawili hao walifanya kazi pamoja kwa miaka miwili huko Bayern Munich. Lakini, beki huyo wa Morocco alishindwa kuonyesha ubora wake alipokuwa kwenye kikosi cha Bayern na kujikuta akianzishwa mara 11 tu. Baadaye, Benatia alikiri kwenye moja ya mahojiano aliyofanya kwamba hakuwa kwenye uhusiano mzuri na kocha Guardiola na kudai kwamba Mhispaniola huyo hana utu kabisa.

ZLATAN IBRAHIMOVIC

Uhamisho wa mbwembwe nyingi wa Zlatan kutoka Inter Milan kwenda Barcelona ulifanyika mwaka 2009 na wengi waliamini staa huyo atakwenda kuwa moto zaidi chini ya kocha Guardiola. Kwa kipindi hicho, straika huyo wa Sweden alikuwa tishio kwelikweli Ulaya na kuwafanya wapinzani wa Barcelona kuingia uoga namna ya kuikabili timu hiyo. Lakini, Guardiola alishindwa kabisa kupata namna bora ya kumtumia Zlatan na hivyo, staa huyo aliondoka Nou Camp baada ya mwaka mmoja tu.

ALEXANDER HLEB

Baada ya kuonyesha kuwa ni bora akiwa na Stuttgart na Arsenal, Hleb alipata nafasi kwenda kuwa chini ya Guardiola huko Barcelona katika msimu wa 2008–09. Hata hivyo, mambo hayakuwa matamu kama alivyokuwa chini ya Felix Magath na Arsene Wenger, Guardiola alishindwa kabisa kupata huduma bora kutoka kwa fundi huyo wa mpira kutoka Belarus. Hleb alidumu kwa msimu mmoja tu chini ya Guardiola kabla ya kuamua kumtoa mkopo kwa muda wake wote uliobaki kwenye mkataba wa Barcelona.

DANILO

Beki huyo wa Kibrazili sawa huenda akapata sifa zake kwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu England akiwa na kocha Guardiola, lakini hakuna ubishi kwamba hakuwa kwenye kiwango bora sana kama ilivyotarajiwa alipokuwa chini ya Mhispaniola huyo.

Danilo alikuwa akiingia na kutoka kwenye kikosi cha kwanza cha Guardiola huko Man City na hakika Mhispaniola huyo alishindwa kabisa namna bora ya kumtumia beki huyo wa pembeni. Baadaye aliamua kumuuza Juventus, alikokwenda kuwa moto uwanjani.

DMYTRO CHYGRYNSKYI

Alisajiliwa kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2009, Guardiola alivutiwa sana na Chygrynskyi, na kutoa Pauni 22 milioni kunasa saini yake alipomsajili kutoka Shakhtar Donetsk. Licha ya Guardiola kulazimisha sana usajili wa beki huyo kutoka Ukraine, bado hakuweza kupata namba nzuri ya kumtumia na matokeo yake alidumu kwa msimu mmoja tu huko Nou Camp kabla ya kurudi zake Shakhtar. Ubora wote wa Guardiola wa kufahamu namna bora ya kutumia wachezaji, lakini hapo alishindwa.

SOMA NA HII  RAIS "HAKUNA WA KUIZUIA YANGA KUTWAA UBINGWA CAF...AMEFUNGUKA HAYA