Home Habari za michezo KASI YA BENCHIKHA YAWASHITUA MAKOCHA

KASI YA BENCHIKHA YAWASHITUA MAKOCHA

Habari za Simba

Mechi nne alizokaa benchi kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha zimetuliza upepo ndani ya timu hiyo na mashabiki kuanza kufurahia kinachoonyeshwa na mastaa wao uwanjani, huku makocha na wadau mbalimbali wakimwagia sifa kocha huyo Mualgeria.

Katika mechi hizo Benchikha, ameiongoza Simba kushinda mbili, kafungwa mmoja na sare moja, ikianza suluhu na Jwaneng Galaxy ya Botswana, kisha kulala 1-0 kwa Wydad ya Morocco iliyoipasua 2-0 majuzi ziliporudiana zote zikiwa ni mechi za Kundi B za Ligi ya Mabingwa, huku ikishinda 3-0 katika Ligi Kuu mbele ya Mtibwa Sugar.

Matokeo hayo yamewafanya wanasimba kwa sasa kupumua baada ya kukosa amani tangu walipoishuhudia timu hiyo ikifumuliwa mabao 5-1 na Yanga katika Ligi Kuu na kumfurusha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na jambo hilo limewaibua wadau kadhaa wa soka wakiwamo mastaa wa zamani na makocha waliotoa maoni yao.

Kocha Abdul Mingange, ambaye ni Meja Mstaafu wa Jeshi, alisema Simba ni ile ile, mashabiki ni wale wale na viongozi ni wale wale, alichokifanya Benchikha ni kutibu akili ya wachezaji kuirejesha mchezoni na kuonyesha mbinu zake.

“Simba haikuanza vibaya kwenye Ligi Kuu, kufungwa na Yanga ndiko kulichangia morali ya watu kushuka chini na kuona wana timu mbovu, Benchikha ni kocha mwenye CV kubwa anajua anachokifanya na ndio maana alitumia akili kubwa kuwafunga Waarabu wenzake wa Wydad, kwani hakutaka mpira wa shoo badala yake alitaka matokeo,” alisema Mingange na kuongeza;

“Ili kikosi chake kiwe hatari zaidi, asajili straika wa kujitegemea na wa uhakika, Jean Baleke anapenda mashambulizi ya kushitukiza sasa yasipokuwepo inakuaje, pia wasajili namba nane mbunifu, japokuwa wakati mwingine wanamtumia Sadio Kanoute ambaye mara nyingi anapata kadi, wampata atakayejilinda na kulinda wengine na pia wasajili beki mwingine upande wa Tshabalala.”

Kwa upande wa staa wa zamani wa timu hiyo, Steven Mapunda ‘Garrincha’ alisema Benchikha anakiangalia kikosi chake ajue maeneo ya kuyaongezea nguvu, jambo la msingi zaidi anaona timu imeanza kucheza kimbinu.

“Mabadiliko mengine kocha anajua kupanga kikosi, maana unaweza ukawa na wachezaji wazuri halafu ukashindwa kuwatumia, mfano mzuri Willy Onana anaanza kumrejesha kwenye mstari, morali inarejea, mbinu zake zinaonekana,” alisema Garrincha, huku beki wa zamani wa Simba na Nyota Nyekundu, Frank Kasanga ‘Bwalya’ aliongeza kuwa Simba imechangamka chini ya Benchikha.

“Tangu kocha Benchikha aanze kuinoa Simba naona wachezaji wamechangamka, wanacheza kwa kasi na ndivyo soka la kisasa linavyotakiwa,” alisema Bwalya.

SOMA NA HII  ROBERTINHO ALALAMIKA HUKU AKIWAPA ONYO YANGA!!! NOMA KWELI