Home Habari za michezo KUTOKA TP MAZEMBE MPAKA SINGIDA KAMA UTANI

KUTOKA TP MAZEMBE MPAKA SINGIDA KAMA UTANI

Klabu ya Singida Fountain Gate inatajwa kuwa ipo kwenye mazungumzo ya kina na aliyekuwa kiungo wa TP Mazembe ya DR Congo, Miche Mika anayekipiga katika kikosi cha FC Saint Eloi Lupopo kwa sasa.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kwamba, mabosi wa Singida wameanza mazungumzo na FC Lupopo kuangalia namna watakavyoweza kupata huduma ya mchezaji huyo kumchukua moja kwa moja akiwa huru.

Kiungo huyo alijiunga na Lupopo, Januari 14, 2022 na mkataba wake unamalizika Januari Mosi mwakani ikiwa ni siku chache tu kuanzia sasa.

Mika kiungo mkabaji na ushambuliaji anatumia mguu wa kulia katika kuifanya kazi yake kwa usahihi ndani ya uwanja.

Kiungo huyo 27, ni mzoefu wa mashindano ya kimataifa kwani alicheza Fainali ya Super Cup dhidi ya Wydad AC akiwa na kikosi cha Mazembe na kupoteza 1-0 Februari 24, 2018 katika Uwanja wa Mohamed V.

Pia, mabosi wa Singida wapo kwenye rada za kumchukua kiungo Sydney Linyama kutoka timu hiyo hiyo kama tu dili la Mika litakuwa gumu kutokana na wote ni wachezaji tegemeo kwenye kikosi chao.

Mabosi hao tayari wametupa ndoano kwenda Jwaneng Galaxy kwa beki Benson Bolasie Mangolo 24, (anacheza kushoto), kwa lengo la kuboresha eneo hilo ambalo kwa sasa anacheza Gadiel Michael.

Mangolo ameonyesha kiwango bora kwenye Ligi ya Mabingwa na mkataba wake unamalizika mwishoni mwa Desemba na amekataa kuongeza mpya.

Kupitia Mtandao wa FAR Post wa Botswana umeripoti nyota huyo licha ya kuwindwa na Singida, timu za Sekhukhune United, Chippa United, Amazulu na Esperance zinahitaji saini yake.

Chanzo kilisema mabosi wa Singida wanaangalia kuitengeneza timu hiyo kuwa na ushindani ndani na nje msimu ujao kucheza tena mashindano ya kimataifa kwa kiwango kikubwa.

Mtendaji Mkuu wa Singida, Olebile Sikwane alisema bado ni timu ndogo lakini kuhusishwa na wachezaji wazuri barani Afrika ni jambo zuri na wakiwapata watakuwa na timu bora zaidi ya sasa.

“Kuhusishwa na mchezaji kama Benson (Mangolo) ni jambo zuri kwa sababu kwa Afrika anatajwa kuwa kwenye kiwango kizuri lakini tunaheshimu mkataba wake kwa sasa na Jwaneng;

“Wote hao ni wazuri, mfano nani hataki kumleta Sydney kwenye timu yake? lakini swali je tutaweza kushindana na wale wenye kisu kikali zaidi?”

Singida imefungiwa kusajili na FIFA kutokana na mashtaka kutoka kwa wachezaji mbalimbali, Sikwane alisema suala hilo linatafutiwa ufumbuzi.

SOMA NA HII  ACHANA NA ISHU YA BONGO UNAAMBIWA SIMBA IMEFUNIKA AFRIKA NZIMA YAWEKA REKODI HII