Home Habari za michezo YANGA YTANGAZA VITA POINT 18 ZATAJWA

YANGA YTANGAZA VITA POINT 18 ZATAJWA

Habari za Yanga

Klabu ya Yanga imesema Kocha wao Mkuu, Miguel Gamondi, atakuwa na kibarua kigumu zaidi mwezi huu, katika kuhakikisha timu hiyo inavuna pointi za kutosha kwenye jumla ya michezo sita ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya mwaka kupinduka.

Yanga katika mwezi huu watakuwa na michezo sita, mitano ya Ligi Kuu Bara wakianza kibarua hicho Jumamosi hii dhidi ya Mtibwa Sugar, kwenye dimba la Azam Complex na mmoja wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana Desemba 20, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati Yanga ikilia na ratiba ngumu, hali kama hiyo pia inaikumba Simba, ambayo nayo itakuwa na mechi sita kali za kuvuja jasho kupambania ushindi mwezi huu.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema mwezi huu maandalizi yake ni tofauti kwa sababu ukitazama ratiba ina michezo mingi na migumu.

Alisema kuna mechi iliyopo karibu dhidi ya Mtibwa Sugar, ambayo mbali na matatizo yao, lakini ni timu nzuri na hawataichukulia kama dhaifu kwa sababu wanaweza wakabadilika katika mchezo huo.

“Ukiangalia kalenda ya mwezi huu, ratiba imetubana sana kuna mechi nyingi ambazo ni ngumu sana, tunatakiwa kuvuna alama tatu dhidi ya Mtibwa Sugar, baadaye tunahitaji kushinda mbele ya Medeama katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tukimalizana na mechi hizo tunatakiwa kusafiri kwenda mikoani kwa ajili ya kucheza mechi zetu za ugenini, kuna Tabora United, Kagera Sugar na Tanzania Prisons na baadaye tunarudi nyumbani kukabiliana na Mashujaa FC,” alisema Kamwe.

Aliongeza kuwa Kocha Gamondi anatakiwa kuandaa programu zake za kuwavusha Yanga salama katika mwezi huo kwa kufanikiwa katika malengo yao ya kusaka ushindi.

“Hatufanyi maandalizi ya mechi moja, bali mechi zote za Desemba. Msimamo wa ligi hautufurahishi kwa sasa, kazi kubwa ni kwa benchi la ufundi na wachezaji kutakiwa kupambana katika hiki kibarua kigumu kusaka alama tatu muhimu dhidi ya Mtibwa Sugar na kurejea katika nafasi yetu ya juu,” alisema Kamwe.

Alisisitiza kuwa licha ya Mtibwa Sugar kuwa katika hali mbaya kimatokeo, wanatakiwa kucheza kwa kuwaheshimu kwa sababu ni timu yenye watu wenye uzoefu mkubwa kwenye ligi na wanaweza kubadili kwao.

Baada ya Mtibwa Sugar, kikosi cha Yanga kitarudi tena dimba Desemba 20, kurudiana na Medeama FC, kisha watakutana ugenini dhidi ya Tabora United mchezo wa Ligi Kuu, hiyo ikiwa ni kama bandika bandua.

Wananchi hao watakuwa na mawindoni tena Desemba 26, dhidi ya Kagera Sugar halafu Tanzania Prisons na baadaye watarejea nyumbani kuvaana na Mashujaa FC, kwenye dimba la Azam.

Kwa upande wa Simba, wao watashuka dimbani Ijumaa wiki hii kuikaribisha Kagera Sugar, kisha Jumanne ijayo watakuwa wenyeji wa Wydad Casablanca ya Morocco katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kisha watakuwa wageni wa KMC Desemba 23.

Baada ya mchezo huo watasafiri hadi Kigoma kuivaa Mashujaa FC Desemba 26 na kisha siku mbili kabla ya mwaka kupinduka wataifuta Tabora United.

SOMA NA HII  KISA RATIBA YA LIGI KUU...KOCHA MKUU SIMBA AIBUKA HILI JIPYA...AVUNJA UKIMYA KUHUSU MECHI NYINGI ZA 'HOME'....