Home Habari za michezo YANGA IWE JUA IWE MVUA MPAKA KIELEWEKE NA STRAIKA HUYU WA ASEC

YANGA IWE JUA IWE MVUA MPAKA KIELEWEKE NA STRAIKA HUYU WA ASEC

Kikosi cha Yanga kimerudi mazoezini kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana utakaopigwa keshokutwa, Jumatano, ikitoka kuiliza Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu kwa mabao 4-1, huku mabosi wa klabu hiyo wakishusha kifaa cha kwanza kutoka Zanzibar, Shekhan Ibrahim, kisha wakamgeukia straika mkali.

Mabosi wa Yanga kwa sasa wanapambana kuhakikisha wanamleta straika huyo kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast, Sankara Karamoko kabla ya kuuaga mwaka 2023 kwa lengo la kuimarisha eneo la ushambuliaji ambalo limekosa mtu wa mwisho wa kutupia nyavuni, japo timu imekuwa ikifunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu.

Licha ya Yanga kuhitaji mshambuliaji ambaye hajacheza mashindano ya Afrika msimu huu, mabosi wa klabu hiyo wala hawajali wanapigania saini ya staa huyo anayejua kufunga mabao kutoka Asec ili kumtumias hata kwenye michuano ya ndani ikiwa na kazi ya kutetea taji la Ligi Kuu Bara na lile la ASFC.

Mkataba wa Sankara na ASEC unaisha mwisho wa msimu huu na Mwanaspoti linafahamu, mshambuliaji huyo ameshaingia rada za Yanga akiwa ameanza kuweka ngumu kuelekea Ulaya kwa timu moja ya Daraja la Pili.

Mabosi wa Yanga, wameamua kuwatumia kikamilifu mastaa wa timu hiyo waliopita Asec ili kumshawishi Sankara ajiunge na timu hiyo na mwenyewe akakubali akiona jamaa wako timu salama.

Yanga inataka kukamilisha dili hilo kabla ya mwaka huu kufikia tamati Desemba 31 na Mwanaspoti linafahamu Sankara anapambana kumalizana na Asec ili awahi usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Jumamosi na kutarajiwa kufungwa Januari 16 mwakani.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ndiye masta aliye mbele ya vita hiyo ya kumshawishi Sankara ambaye anaweza kuwa staa wa nne kutoka Asec kutua, kwani tayari inao Stephanie Aziz KI, Pacome Zouzoua, Yao Kouassi ambao wote walisajiliwa na timu hiyo kwa nyakati tofauti.

Bosi mmoja wa Yanga ameliambia Mwanaspoti, kama kuna mshambuliaji anawaumiza kichwa basi ni Sankara na kwamba katika usajili wao huu wa dirisha dogo jamaa ni chaguo la kwanza.

Bosi huyo aliongeza mbali na Sankara pia wanaisubiri Medeama ya Ghana kuangalia namna ya kumalizia mazungumzo juu ya kumchukua pia Jonathan Sowah ambaye ni mshambuliaji wa timu hiyo.

“Sankara ndio chaguo letu namba moja tukimpata huyo tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya usajili wetu, ni kijana mdogo ambaye analijua goli,” alisema bosi huyo na kuongeza;

“Chaguo la pili ni yule Sowah (Jonathan) tunataka kumuona hapa pia atakavyocheza ugenini akitushawishi tutatafuta akili ya kumalizana naye, tunaweza hata kusajili washambuliaji wawili dirisha hili.”

Yanga inahaha kusaka mshambuliaji wa kati kwani tangu Fiston Mayele aondoke kwenda Pyramids ya Misri, haijapata mbadala wake licha ya kumsajili Hafiz Konkoni kutoka Ghana na kikosini ikiwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize ambao wameshindwa kufanya maajabu na kuwapasua kichwa mabosi hadi sasa.

Licha ya kwamba Yanga haina mshambuliaji wa kati tegemeo wa kuamua mechi, lakini ni moja ya timu yenye mabao mengi katika Ligi Kuu ikifunga 30 katika mechi 10 tu, ikitanguliwa na Azam yenye 31 kupitia mechi 12, huku Aziz KI akiongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao tisa akifuatiwa na Maxi Nzengeli mwenye saba.

Aziz KI na Maxi kama ilivyo kwa Pacome Zouzoua mwenye mabao manne ni viungo washambuliaji, huku mshambuliaji wa kati, Musonda amefunga mabao matatu, wakati Mzize na Hafiz kila mmoja ana bao moja.

SOMA NA HII  KWANI LIGI INAANZA LINI, YANGA YAMNASA STRAIKA MPYA, YAMTAMBULISHA USIKU