Home Uncategorized MUDA WA KUREJEA LIGI UPO KARIBUNI, WAKATI WA KILA MMOJA KUJIWEKA TAYARI

MUDA WA KUREJEA LIGI UPO KARIBUNI, WAKATI WA KILA MMOJA KUJIWEKA TAYARI


MAAGIZO ambayo yatatolewa na Serikali tusiyapuuzie iwapo  masuala ya michezo yatarudishwa hivi karibuni kwani tulikuwa tumekosa mambo mengi kwa upande wa michezo.
Sababu kubwa iliyofanya mambo kwenda kombo kwenye masuala ya michezo pamoja na shughuli nyingine ni kutokana na janga la Virusi vya Corona ambalo limeivuruga dunia linavyotaka.
Hilo lipo wazi kwani sio jambo la mtu mmoja pekee bali dunia nzima inapambana kuona namna gani inaweza kupata usalama na kuendelea na shughuli za maisha kama ilivyokuwa zamani.
Mzigo mzito upo kwa kila mmoja kufikiria hali ya maisha yake na namna anavyoweza kuwa salama kwa wakati huu wa mashaka ambao umezidi kuendelea kwa kila mmoja na dunia pia kiujumla.
Maradhi tupo nayo ni lazima tukubali kwamba Virusi vya Corona vipo na vinaenea kwa kasi lakini cha kujiuliza ni kwa namna gani tunachukua tahadhari wakati tunaendelea na maisha mengine ya kila siku.
Siku zinakwenda kasi sana hilo lipo wazi basi na akili za kupambana kwenye vita hii ni muhimu pia kuibadili na kufanya mambo kwa kuzingatia afya zetu ambazo ni utajiri namba moja.
Hofu imetanda kila kona ambapo kwenye mioyo ya watu wengi wanahofia kushindwa kuendelea kupambana na Virusi vya Corona hilo inabidi liondoke kwenye mioyo ya watu kwa sasa.
Uwezekano wa maisha kuendelea kama kawaida upo na kwa hatua ambayo tumefikia kwa sasa sio hatua mbaya kwani tayari tunaona kwamba kuna harakati ambazo zimeanza ili kuirejesha ligi.
Kikubwa tunachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuona kwamba kila mmoja anajitahidi kuzungumza na mwenzake ili awe balozi mzuri ili pale mambo yatakapoanza kwenda sawa kila mmoja awe ni mshindi katika hili.
Iwapo kila mmoja atakuwa balozi katika hili japo kwa muda mfupi itaokoa wengine ambao wao ni wepesi wa kupuuzia mambo na kuyafanya yaende kwa namna ambavyo wanafikiria.
Kikubwa ni kila mmoja kuchukua tahadhari ajilinde yeye na wenzake jambo litakalofanya kila mtu aendelee na maisha yake kwa amani.
Mabadiliko yanazidi kutokea kila iitwapo leo ambapo tunaona kwamba nchi za wenzetu wameshaanza kukiwasha ndani ya uwanja jambo ambalo linapaswa liwe mfano kwetu pia.
Ujerumani wao tayari wameanza kushuhudia burudani ambapo ligi yao maarufu kama Bundesliga kwa sasa inachanja mbunga.
Mwezi Machi nao walisimamisha ligi yao kutokana na janga la Corona ambalo linawapasua kichwa wataalamu kutafuta dawa ili maisha yaendelee kwenda.
Kama wao wameanza basi ni sawa na nina amini wanasimamia kile ambacho wanakiamini lakini bado kuna namna ambayo wanaweza kufanya ili wazidi kuwa bora na kutoa somo kwa wengine ambao bado hawajaanza ligi.
Kitu pekee ambacho kinatakiwa kwa sasa ni wao wenyewe wachezaji kukubali hali halisi kwanza kisha kujipanga upya kwa ajili ya kubadili staili yao ya maisha.
Maisha ya mpira kwa wakati ujao pale ambapo ligi itarudi yana changamoto nyingi lakini ni bora iwe hivyo kuliko kukosa kabisa ile burudani ambayo tulikuwa tumeizoea.
Wachezaji wanatakiwa watambue kwamba kitakachowaokoa kwa sasa ni umakini wao pamoja na dua bila kukoma itawasaidia kuwa kwenye ubora wao na kuikabili changamoto mpya ya viwango vyao kushuka.
Inabidi watambue kwamba mechi zote zitachezwa bila mashabiki hivyo ni lazima wajiaandae kisaikolojia kupambana na hilo kwani ni jambo la kuzingatia.
Ikiwa muda wa mapumziko haya ya lazima  walishindwa kufanya mazoezi itakuwa ngumu kurejea kwenye ubora wao na kuwafanya wawe kwenye uwezo wa chini kuendelea na maisha ya kwenye soka.
Ni muhimu kufuata utaratibu na kanuni ambazo zimewekwa na Serikali pamoja na Wizara ya afya wakati wa mazoezi itawasiaidia kuwa bora.
Matumaini yameanza kuonekana kidogo kwamba ligi inaweza kurejea maana hii ni mara ya pili Serikali inazungumza kuhusu kurejea kwa ligi ili kushuhudia burudani.
Kila mwanafamilia ya soka anapenda kuona wachezaji wakiwa kwenye ubora na wanafanya kazi bila mashaka yoyote ndani ya uwanja pindi ligi itakaporejea na ndio dua zilizopo kwa sasa.
Kwa kuwa kila mmoja anapenda kushuhudia burudani basi wachezaji nao wasiwaangushe mashabiki wao licha ya kwamba watacheza bila kuwa na mashabiki.
SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA NYUMA GAZETI LA CHAMPIONI IJUMAA