Home Uncategorized FEDHA ZISIMPOTEZE BAKARI MWAMNYETO AKAJEGA URAFIKI NA BENCHI

FEDHA ZISIMPOTEZE BAKARI MWAMNYETO AKAJEGA URAFIKI NA BENCHI


UNAAMBIWA kwenye maisha ya kila siku ambayo tunaishi wewe poteza kila kitu ulichonacho ila usipoteze matumaini yatakusaidia kurejesha yale ambayo umepoteza.
Ndivyo ilivyo kwenye maisha ya soka ambapo huku unaambiwa mchezaji poteza kila kitu ulichonacho ila sio nafasi yako kwenye kikosi cha kwanza.
Nimeanza kusema hivyo kutokana na sarakasi ambazo zinaendelea kwa sasa kwa beki chipukizi anayekipiga ndani ya Coastal Union, Bakari Mwamnyeto kuwa lulu ambapo kila timu inamtazama.
Ni wakati wake kuwa sokoni kwa sasa kutokana na ubora wake ambao anaonyesha ndani ya uwanja na nje ya uwanja yupo vizuri kijana.
Ukizungumzia kuta matata ambazo ni lazima mshambuliaji ujipange kuzipita kwa wakati huu kabla ya ligi kusimamishwa huwezi kuacha kuitaja ile ya Coastal Union iliyo chini ya Mwamnyeto.
Mbali na kuwa ni beki pia amepewa majukumu ya kuwa nahodha hapo unaona ni mzigo mzito ambao anao kijana lazima apambane.
Timu yake ikiwa imecheza mechi  28 imeruhusu kufungwa mabao 19 inaonyesha ipo vizuri kwani kuta namba moja kwa uimara ni ile ya Simba imefungwa mabao 15 baada ya kucheza mechi 27.
Hesabu zinarudi kwa Mwamnyeto tena tangu msimu uliopita ilielezwa kuwa anakwenda Simba ghafla upepo umebadilika anataka milioni 100 atue Yanga ni maisha ya soka ila kuna umuhimu kwake kufanya tathimini mara mbilimbili.
Nilipata muda wa kuzungumza na Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru aliweka bayana kwamba timu hizi kubwa zina wakati wao zikijiskia kuchukua wachezaji zinabeba ila akishindwa kuwapa kile walichokitarajia basi asifikirie atapewa thamani aliyokuwa anaifikiria.
Orodha ya majina ya wachezaji ambaao walisajiliwa kwenye timu kubwa na wakaachwa bila kujua hatma yao aliyonitajia ni kubwa ila mfano mdogo tu alinipa majina mawili ya Abdulhaman Humud na Hassan Dilunga ambao kwa sasa wapo kwenye ubora.
Tuachane na hayo narudi kwa Mwamnyeto danadana hizi zinazopigwa zina maana ni wakati mwingine tena wanaomshauri kijana huyu kumpa darasa makini iwapo anahitaji kusepa ndani ya utawala wake ambao umeanza kujipa wakati huu.
Inakuwa ngumu sana kuendeleza pale ulipoishia iwapo utakwenda nje ya ule mfumo ambao umeouzoea hasa kwa wachezaji wazawa bado sijajua tatizo limejificha wapi.
Wazawa wengi huwa inakuwa ni maji kupwa maji kujaa mfano mzuri ni Ibrahim Ajibu ambaye alisepa Yanga akiwa kwenye ubora wake na ufalme wake ulikuwa mkubwa ila alipoibukia Simba mambo yamebuma.
Pasi zake 17 na mabao sita akiwa Yanga kwa sasa bado zinampasua kichwa kwani hajafikia hata nusu ya vyote viwili, ana pasi nne za mabao na bao amefunga moja na nafasi yake kwenye timu ni finyu.
Kuna jambo la kujifunza kwa wachezaji wetu wazawa kabla ya kuondoka haina maana kwamba wanapaswa wabaki hapo walipo hapana ni lazima wafanye tathimini sahihi itakayowachuja na kuwapa picha ya kesho itakavyokuwa.
Achana na hao waliojiunga na Simba pamoja na Yanga hebu jikumbushe, Abdulkalim Kassim, anayekipiga ndani ya Azam FC utawala wake uliyeyuka ghafla baada ya kuibukia hapo msimu wa 2018/19 akitokea Kagera Sugar ambapo alikuwa ni chaguo la kwanza ila kwa sasa amejenga ushkaji na benchi.
Ninaamini kwamba kila mchezaji ana ndoto zake basi wakati wa kutimiza ndoto ni muhimu kutazama matumaini ya kuwa kikosi cha kwanza kuliko matumaini ya kupokea mkwanja mrefu kisha ukajenga ushkaji na benchi inauma kweli.

SOMA NA HII  SABABU YA BERNARD MORRISON KUACHWA BONGO IPO HIVI