Home Habari za michezo SHOW ZA MNYAMA ZNZ LEO KAMA KAWA…MUDA NI ULE ULE WA MAANGAMIZI….

SHOW ZA MNYAMA ZNZ LEO KAMA KAWA…MUDA NI ULE ULE WA MAANGAMIZI….

Habari za Simba leo

MUDA ni ule ule na mahali ni pale pale, wakati Mnyama Simba akirudi uwanjani kukamilisha ratiba ya mechi za makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 kwa kukabiliana na APR ya Rwanda, huku ikiwa tayari imeshakata tiketi ya robo fainali.

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja huku Simba ikiwa kinara wa Kundi B ikilingana pointi sita na Singida Fountain Gate iliyomaliza mechi huku zikitofautishwa na mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba ilitinga hatua hiyo ikiungana na Yanga, Azam, Singida Fountain Gate na KVZ baada ya kushinda mechi ya pili mfululizo kwenye Kundi B dhidi ya Singida, huku leo ikisaka heshima tu ya kumaliza kama kinara wa kundi hilo, huku APR ikitaka kupata ushindi kuungana vigogo hivyo katika robo fainali.

APR ina pointi tatu kwa sasa baada ya kucheza mechi mbili ikipoteza moja na kushinda moja, huku ikisifika kwa kutandaza soka tamu, kitu kinachofanya mchezo wa leo kuwa mtamu zaidi kwani Simba nayo imerudi kwenye lile soka burudani lililozoeleka.

Simba ikiwa chini ya kocha Abdelhak Benchikha juzi ilitandaza soka tamu huku baadhi ya nyota wake wakitoa burudani kwa mashabiki akiwamo Fabrice Ngoma, Luis Miquissone na Willy Onana wakati timu hiyo ikishinda 2-0 mbele ya Singida, japo leo itakuwa na kazi ya kukabiliana na nyota wa APR wenye kasi na vipaji.

Juzi kocha Benchikha alisifia wachezaji walivyocheza vizuri, huku Ngoma akichaguliwa nyota wa mchezo na kuvuta Sh 500,000 akiwa mchezaji wa pili wa timu hiyo baada ya awali beki Fondoh Che Malone kuchaguliwa siku ya mechi dhidi ya JKU na kushinda mabao 3-1.

Kabla ya mechi hiyo mapema saa 10:15 jioni, Jamhuri itavaana na Jamus kwenye mchezo wa Kundi C, huku timu hizi zikipambana kusaka kumaliza katika nafasi ya pili au kupata tiketi ya ‘best looser’ ili icheze robo fainali zinazotarajiwa kuanza keshokutwa Jumapili.

SOMA NA HII  DIAMOND : NAJUA NINI KILITOKEA MPAKA HAJI MANARA AKAWA YANGA...MUNGU MKUBWA KULIKO FITINA ZA BINADAMU...