Home Habari za michezo ‘KIBESI’ CHA ALLY SALUM KWA KINA CHE MALONE KINAVYOMPA SHAVU LA UHAKIKA...

‘KIBESI’ CHA ALLY SALUM KWA KINA CHE MALONE KINAVYOMPA SHAVU LA UHAKIKA SIMBA….

Habari za Simba Leo

Haikuwa kazi nyepesi kwa kipa wa Simba, Ally Salim (23) kuanza kuaminiwa kupewa nafasi katika baadhi ya mechi za mashindano, kwani alizungukwa na makipa wazoefu.

Wakati anapandishwa kutoka kikosi cha vijana, kikosi cha wakubwa kilikuwa na Aishi Manula, Said Mohamed ‘Nduda, Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao wakaondoka baadaye akaja Beno Kakolanya, hivyo haikuwa kazi nyepesi kwake kupata nafasi mbele ya kaka zake.

Uvumilivu wake, ukaanza kumlipa mwishoni mwa msimu uliopita baada ya Manula kuumia, wengi walitegemea mechi dhidi ya Ihefu FC, waliyoshinda mabao 2-0 angedaka Kakolanya, lakini kocha Oliveira Roberto ‘Robertinho’ akampanga Salim.

Mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Yanga, kocha Robertinho bado aliendelea kumpa nafasi Salim na walishinda mabao 2-0 mbali na Ligi Kuu, bali alidaka mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad.

Mchezo dhidi ya Wydad, Simba ikiwa ugenini ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0 huku kipa huyo akiwa langoni, mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, Mnyama aliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ujio wa kocha mpya ndani ya kikosi hicho, Abdelhak Benchikha ambaye alikuwa anatoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha kiwango chake, uliibua ufundi mwingine wa Salim, kujua ni fundi wa kudaka penalti.

PENALTI ZIMEMPA UMAARUFU

Nyuma ya penalti anazozidaka wakati wa mechi za mashindano, anafanya mazoezi ya kutosha, kitu kinachomjengea kujiamini, akibakia na mpigaji anaona ni jambo la kawaida.

“Tunafanya mazoezi ya kudaka penalti na makipa wenzangu, ndio maana unakuta siyo muoga inapotokea hilo kwenye mechi za mashindano nalichukulia kama jambo la kawaida,” anasema na kuongeza;

“Ukichunguza vizuri makipa wote wa Simba tuna uwezo wa kudaka penalti, kuanzia kwa kaka yangu Manula, Ayoub na Abel, yote hayo ni matunda ya mazoezi ambayo tunayafanya na kocha kutuongezea mbinu.

“Ukiachana na hilo, kuna wakati naonekana kuwagombeza mabeki, ile inakuwa ni kuwakumbusha, unakuta umeongea nao jambo zaidi ya mara mbili, na wao wanakuwa kwenye presha ya mchezo, hivyo lazima niwaambie ili tumalize dakika 90 salama.”

Kipa anayemfunza vitu vingi kwa kumuangalia anachofanya mazoezini na kwenye mechi, anamtaja Manula alivyojasiri akisimama golini, nidhamu ya kazi na mbinu zake uwanjani.

“Ukiondoa changamoto za majeraha ya hapa na pale aliyoyapitia, Manula kwangu ni kipa bora, nina bahati kucheza naye timu moja, amekuwa akinishauri vitu vya kufanya ili niwe bora,” anasema.

KUPANDISHWA

Tangu apandishwe timu ya wakubwa akitokea Simba B mwaka 2018-2024 timu hiyo. imechukua mataji manne ya Ligi Kuu Bara, msimu wa 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21.

“Nilifurahia kuvaa medali za ubingwa, kwani siyo kitu rahisi, kuna wachezaji hawajawahi kupata bahati hiyo na wanatamani kwenye maisha yao waweke historia ya kuvaa medali za ubingwa,” anasema.

BENO, DIDA WATOA NENO

Beno ambaye kwa sasa anacheza Singida Fountain Gate, anamuelezea Salimu kwamba nafasi anayopewa ya kuaminiwa ni wakati wake wa kutoka, anapaswa kuipambania ili isimponyoke.

“Nafasi yake ina ushindani, ukiachana na Manula, kuna mgeni Ayoub Lakred na Hussein Abel ambaye hajaanza kupata nafasi ila ni kipa mzuri,”anasema.

Wakati Dida anayecheza Namungo, anasema “Uvumilivu ndio umemfanya Salim aonekane bora kwa sasa, anatakiwa kuendelea kumshawishi kocha kwamba ni bora, kwani nafasi yake ina ushindani mkubwa.”

MAKOCHA NAO

Kocha wa zamani wa makipa wa timu hiyo, Idd Pazi anasema ni kipa mzuri anayehitaji kujifunza utulivu na kutuliza wengine kwenye mechi za presha.

“Uzuri wa nafasi ya kipa kadri unavyocheza ndivyo unavyozidi kuwa bora, ajitume kwa bidii, naamini atafanya makubwa,” anasema na kuongeza;

Ukiachana na Pazi, kocha wa makipa wa Singida Fountain Gate,Peter Manyika Sr anasema “Kadri ninavyoendelea kumuona Salim kiwango chake kinakuwa bora, aendelee kujifunza utulivu ambao utawafanya awatulize wengine mechi ikiwa kwenye presha.”

Credit:- Mwanaspoti

SOMA NA HII  MBADALA WA AUCHO WAPATIKANA YANGA...KUMBE KAGOMA ALIVUNJA MKATABA...ISHU NZIMA IKO HIVI