Home Habari za michezo KUHUSU UNDANI WA STARS KUTOKA SARE NA ZAMBIA JANA….UKWELI USIOSEMWA HUU HAPA…

KUHUSU UNDANI WA STARS KUTOKA SARE NA ZAMBIA JANA….UKWELI USIOSEMWA HUU HAPA…

Taifa Stars
Tanzania's midfielder #6 Feisal Salum (C) fights for the ball with Zambia's midfielder #15 Kelvin Kapumbu (R) during the Africa Cup of Nations (CAN) 2024 group F football match between Zambia and Tanzania at Stade Laurent Pokou in San Pedro on January 21, 2024. (Photo by SIA KAMBOU / AFP)

BAADA ya Stars kurudia historia ya 1980 dhidi ya Zambia juzi katika Uwanja wa Laurent Pokou, Ivory Coast kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambako ilitoka sare ya bao 1-1, makocha wameeleza sababu za kukwama kwa timu hiyo.

Hii ni mara ya tatu kwa Stars kushiriki michuano hiyo, ambapo sare ya kwanza ilipatikana kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa mjini Lagos, Nigeria mwaka 1980 na bao la Tanzania lilifungwa na Hayati Juma Mkami.

Lakini sasa sasa imejirudia tena katika mechi ya juzi dhidi ya Zambia kwa bao lililofungwa na Saimon Msuva katika dakika ya 10 likiwa ni bao lake la pili katika michuano hiyo, kwani lingine alifunga mwaka 2019 dhidi ya Uganda katika fainali zilizofanyika Misri.

Juzi, Stars iliingia uwanjani katika mchezo huo ikiwa haina kocha mkuu, baada ya Adel Amrouche kutimuliwa ilipotoka kwenye mchezo dhidi ya Morocco ambao ilichezea kichapo cha mabao 3-0.

Hiyo ni mechi ya pili kwa Stars katika kundi F ililopo na timu za Morocco, Zambia na DR Congo huku Stars ikifunga na kupata sare iliyoifanya kupata pointi moja.

Licha ya sare hiyo mashabiki wengi hapa nchini walilalamikia kutokuwepo kwa umakini upande wa Stars kwani tayari ilikuwa imemiliki mchezo kipindi cha kwanza, lakini shida ikaanza iliporejea katika kipindi cha pili.

Kipindi cha pili baada ya Stars kuamini imemaliza mechi, kocha wa Zambia, Avram Gran aliwaingiza Kennedy Musonda anayeitumikia Yanga na Clatous Chama wa Simba na ndio waliobadili mchezo na kuhamishia mashambuzi langoni mwa Tanzania.

Mchezo huo ulibadilika baada ya Chama kuanza kuwasumbua viungo wa Stars na dakika chache kusababisha kona aliyopiga haraka na kusababisha bao la kusawazisha kuingia. Kufuatia matokeo hayo, baadhi ya makocha wamezungumzia kilichoiponza timu ya Taifa.

Kocha wa zamani wa Yanga ambaye sasa ni wa Tabora United, Goran Kapinovic, amesema licha ya mchezo kumalizika kwa sare, lakini angalau Stars ilicheza vizuri.

Amesema uchaguzi wa kikosi cha kwanza ulikuwa sahihi na timu ilicheza kwa umoja na kujituma, lakini kilichoiponza ni kuanza kupunguza kasi iliyoanza nayo baada ya kupata bao.

“Hakukuwa na mpango mkubwa wa kutafuta mabao, pia dakika 10 za mwisho wachezaji hawakuongeza umakini jambo ambalo lilisababishwa kufungwa, bila kusahau uwezo mdogo wa mazoezi ya viungo waliyo nayo,” amesema.

“(Stars) katika haya mashindano ya Afcon inaponzwa wachezaji wake wengi wanazichezea timu za kawaida tofauti na wapinzani wao Morocco, Zambia na hata DR Congo.

“Samata pekee ndiye anacheza Ulaya tena klabu kubwa, ila wengine wote ni kawaida. Hilo ndilo lililoiumiza Stars kwani ilikosa viwango bora na sasa ijipange kuzalisha vipaji ili viende kucheza soka la ushindani zaidi.”

Kocha wa zamani wa Yanga na Azam, George Lwandamina amesema Tanzania itajilaumu kwa kushindwa kutawala mchezo katika kipindi cha pili na kusababisha makosa ambayo yaliwarudisha Zambia mchezoni.

Lwandamina ambaye ni kocha Zesco, amesema kuanzia eneo la ushambuliaji lilishindwa kuwa na ubunifu na kutengeneza hatari katika lango la Zambia na pia lile la kiungo lilipokosa ubunifu wa kutengeneza pasi za hatari na kuulinda mpira.

Amesema amebaini kosa jingine ni lile la mabeki waliofanya makosa ya kupoteza mipira kirahisi.

“Nafikiri Tanzania walicheza vizuri dakika arobaini na tano za kwanza. Kipindi cha pili walishindwa kabisa kuushika mchezo, kwani kuna makosa ambayo yalitusaidia Zambia,” amesema.

“Mnapocheza watu kumi uwanjani dhidi ya wenzenu waliokamilika wale waliokamilika kama watashindwa kutengeneza (nafasi) tofauti ya kimbinu ni rahisi (kwa) wale wachache kuamka kama nao wako sawasawa.

“Nadhani hiki ndicho kilichotokea jana (juzi). Wachezaji wetu Zambia walitumia ukomavu wao kulazimisha kubadilisha kitu wakati Tanzania wakiwa chini.

“Nadhani pia Tanzania inatakiwa kutengeneza wachezaji wenye uwezo wa kufanya mambo makubwa jana walikuwa kawaida sana. Huoni kama ni timu inayotaka kutafuta ushindi au ushindi mkubwa zaidi. Kkuna wakati walikuwa wanacheza kama timu ambayo imeshafuzu.”

Kocha mkongwe nchini, Abdul Mingange amesema kama Stars itaendelea na makosa iliyofanya dhidi ya Zambia inaweza kupoteza mchezo ujao ambao ni muhimu na ndio uliosalia.

“Tusiwalaumu sana kwani kwenye mpira wa miguu kuna kuzidiana na ukitazama kiwango cha wapinzani kilikuwa juu zaidi, hata maarifa nayo walizidiwa ukiachana na uwezo mkubwa walionao kutokana na mazoezi ya viungo,” amesema Mingange.

“Natoa asilimia 40 ya Stars kushinda (dhidi ya DR Congo) kwani shida ni moja – wanaocheza nao wameshazoea kushiriki ligi ngumu zenye ushindani tofauti na kikosi chetu wengi wametoka Ligi Kuu Bara ambapo washindani wao ndio Simba ambayo nayo haina makali ya kimataifa.”

SOMA NA HII  METACHA MNATA AZUA YA KUZUA ....POLISI TANZANIA WAIBUKA NA KUMNG'ANG'ANIA BAADA YA KUSAINI TIMU INGINE...