Fanya mambo yote itakapotimia saa 1:00 usiku, kaa chini uangalie boli linavyotembea. Si tu kwamba Yanga itakuwa ikisaka heshima mbele CR Belouizdad ya Algeria, bali mpira wa kuvutia utakuwa unachezwa.
Ni mechi ambayo staa wa Yanga, Pacome Zouzoua anataka kuwapa heshima ya pekee mashabiki wa timu hiyo kwa ushindi muhimu kuwasogeza kwenye hatua ya robo fainali kutokea Kundi D.
Yanga inakutana na CR Belouizdad katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Mchezo huo umepewa jina la ‘Pacome Day’ ikijua inataka kupata matokeo, lakini ndani yake upigwe mpira mwingi kama ambavyo anavyofanya kiungo huyo fundi aliyeiongezea nguvu msimu huu akijua kufunga na kuchezesha timu ambaye alisajiliwa akitokea Asec Mimosas.
Tamu kuliko yote katika kuleta hamasa kwa wachezaji ili wapambane kwa jasho lote, matajiri wa Yanga jana usiku walikutana na wachezaji na kuwapa ahadi nzito ya fedha isiyopungua Sh500 milioni kwa ushindi, lakini kabla ya hapo kambini kwa wachezaji kumekuwa na mzuka mkubwa.
Yanga wamejidhatiti kuhakikisha safari hii wanacheza robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi ngazi ya klabu Afrika baada ya msimu uliopita kucheza fainali za Kombe la Shirikisho na kukosa ubingwa kikanuni.
Timu hiyo inataka pointi nane ambazo zitawaacha mbali Belouzdad wanaolingana nao, lakini matokeo ya kupoteza dhidi ya Waarabu hao kwenye mchezo wa kwanza ndio unaifanya kuwa nafasi ya tatu kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Lakini, hesabu za pili ni kwamba Yanga itakuwa na mtego wa kuhakikisha inashinda kuanzia bao nne ambazo zitaisaidia kuitofautisha huko mbele endapo timu hizo mbili zitalingana kila kitu, ambapo italazimika kuangaliwa kwa matokeo baina ya timu hizo mbili.
Yanga ilipoteza mechi ya kwanza ya makundi ugenini dhidi ya Belouizdad kwa mabao 3-0, ambapo ili waukwepe mtego huo watalazimika kushinda zaidi.
Timu hiyo katika mechi nne zilizopita za Ligi ya Mabingwa haijapishana sana na Belouizdad ikishinda moja nyumbani dhidi ya Medeama (3-0), lakini ikatoka sare mbili – kwanza nyumbani dhidi ya Ahly kisha Medeama ikifungana nao 1-1. Belouizdad imeshinda mchezo mmoja ilipoifunga Yanga, kisha ikatoka suluhu nyumbani na ugenini dhidi ya Ahly, lakini ikachapwa 2-1 na Medeama ugenini.
Staa ambaye Yanga itamtanguliza kama mwiba kwa Belouizdad ni Pacome huku Belouizdad ikimtegemea mshambuliaji Abderrahmane Meziane aliyewafunga Yanga zaidi akiwa na bao moja alilofunga kwenye mchezo wa kwanza msimu huu, lakini pia akiwa amewahi kuwafunga alipokuwa na USM Alger alipokutana nao kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.
Kando ya Meziane kuna kiungo Abdelraouf Benguit ambaye msimu huu amefunga mabao mawili katika mechi mbili, lakini kinara wa mabao kwenye ufungaji katika ligi akiwa mshambuliaji Lionel Wamba anayeshika nafasi ya tatu kwa ufungaji akiwa na mabao manane huku Yanga watatamba na fundi Stephanie Aziz KI mwenye mabao 10 katika ligi akiongoza kwa wapachika mabao.
Belouzdad ugenini msimu huu imefunga bao moja pekee ilipochapwa mabao 2-1 kwa bao la Benguit, ikiwa pia ukuta wake umeruhusu mabao mawili katika mechi nne inakutana na Yanga ambayo nyumbani imeshafunga mabao manne, ikishinda 3-0 dhidi ya Medeama na sare na Ahly ya bao 1-1 lakini ukuta wa Yanga utatakiwa kujiimarisha kwani umeruhusu mabao matano kwenye mechi nne.
Timu hizo hazijatofatiana sana zikiwa ligi ya nyumbani labda Yanga itaringa kwa kuwa ni vinara wa ligi ikiwa na pointi 43 wakati Belouizdad ikiwa ya pili na pointi 31 lakini zote kwenye mechi tano zilizopita kila timu ikishinda nne na sare moja.
Timu ya mwisho kuondoka na ushindi kimataifa ikikutana na Yanga nyumbani ilikuwa ni USM Alger, Mei 28,2023, Waarabu hao waliposhinda kwa mabao 2-1 kabla ya kwenda kuchapwa na baada ya hapo Yanga imekuwa na matokeo mazuri ikiwa kwake ikishinda mechi saba bila kupoteza.
MIKAKATI YA GAMONDI
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema wanakwenda kucheza mechi ambayo lazima washinde na hakuna tafsiri nyingine. “Hii ni mechi ngumu, lakini kwetu ni lazima kushinda. Tupo kwenye kundi gumu, tunakutana na timu yenye uzoefu mkubwa lakini Yanga tuko vizuri pia. Tumetoka kucheza mechi ngumu za ligi, sisi na wachezaji wangu tutafanya kila linalowezekana tuwafurahishe mashabiki wetu. Tutacheza kwa nidhamu kubwa tutakapokuwa tunashambulia tunajua wapinzani wetu watasubiri makosa yetu wakati tunashambulia,” alisema Gamondi.
MASTAA VICHWANI
Baada ya Yanga kuupa mchezo huo jina la ‘Pacome Day’ na tangu juzi vichwa vya baadhi ya mastaa wake, vigogo na hata mashabiki vimekuwa na rangi kila mmoja akiweka ‘blichi’ ambayo ndio rangi ya nywele zinazomtambulisha kiungo huyo.
Mchezo huo utaamuliwa na mwamuzi Boubou Traore kutoka Mali aliyezaliwa miaka 34 iliyopita akiwa anachezesha mechi ya kwanza ya Yanga akisaidiwa na Sydou Tiama wa Burkina Faso na Nodibo Samake kutoka Mali, huku mwamuzi wa akiba akiwa Ousmane Diakite wote kutoka Mali.
FAIDA YA JOTO LA DAR
Yanga itauanza mchezo huo kwa presha kubwa kusaka mabao ikitaka kuwachosha Belouzdad ambao bado walikuwa wanalia na joto kali la jijini Dar es Salaam mpango ambao umeanzia kwenye mazoezi, lakini pia makocha wa timu hiyo wamekuwa wakali ili kuhakikisha umakini wa kutumia nafasi unaongezeka ushindi upatikane.
Nchini Algeria kwa sasa hali ya hewa inasoma nyuzi joto 14 kukiwa na mvua kubwa inayoambatana na baridi, ikitua jijini Dar es Salaam ambako nyuzi joto kwasasa ni 32 kukiwa na joto kali bila mvua, hali ambayo ni wazi endapo Yanga itawakimbiza Waarabu hao watakutana na wakati mgumu.
Kocha wa Belouizdad, Marcos Paqueta amesema wamejiandaa kucheza mechi ngumu dhidi ya Yanga wakijua wanakutana na timu bora yenye wachezaji wazoefu, lakini wamejipanga kupata ushindi mazuri ambayo yatawarahisishia kufuzu robo fainali.
“Itakuwa mechi ngumu na nzuri. Yanga ni timu nzuri inapenda kucheza mpira kama sisi (Belouizdad). Naamini itakuwa mechi ambayo wote watakaoishuhudia wataifurahia. Kundi hili ni gumu nililiona kuanzia mwanzo. Tunafahamu tuliwafunga (Yanga) mwanzo lakini hii itakuwa mechi tofauti. Wasiwasi wangu ni hali ya hewa inaweza kutuathiri,” alisema Paqueta.