Home Azam FC TAMU NA CHUNGU WANAZOPITIA MASTAA WAPYA WA AZAM HIZI HAPA….SIMBA MTAPIGIKA….

TAMU NA CHUNGU WANAZOPITIA MASTAA WAPYA WA AZAM HIZI HAPA….SIMBA MTAPIGIKA….

Habari za Michezo

Fowadi mpya wa Azam FC, Franklin Navarro aliyesajiliwa kutoka Amerika ya Kusini, amesema yupo tayari kuanza mikiki ya Ligi Kuu Bara, licha ya kukiri kukabiliana na changamoto ya lugha, vyakula na mazingira.

Navarro ambaye alikuwa akiichezea Inter Palmira ya kwao Colombia, anaamini kadiri ambavyo siku zitakuwa zikisogea mambo yataendelea kumnyokea akiwa na Mcolombia mwenzake, Yeison Fuentes (21) aliyetokea Leones FC.

“Kucheza Afrika ni jambo jema kwa ajili ya kupata uzoefu mwingine kwenye maisha yangu ya soka, kiukweli nasubiri kwa hamu kuanza kucheza mechi za ligi ya Tanzania, nimekuwa nikipewa ushirikiano wa kutosha kutoka kwenye benchi la ufundi na hata wachezaji wenzangu japo muda mwingine mawasiliano ni changamoto,” alisema na kuendelea;

“Imetubidi kuanza kujifunza Kiswahili na kwa bahati nzuri kwa sasa tunajua namna ya kusalimia, tukiwa uwanjani ambacho kinaongea huwa ni miguu na ninashukuru kuona wachezaji wenzangu wakijitahidi kutusoma na sisi tumekuwa tukiwasoma na kujua namna ya kucheza nao.”

Navarro na Fuentes wanaongea Kihispania, hivyo imekuwa changamoto kwa upande wao kufanya mazungumzo ya kina na wachezaji wenzao japo wamekuwa wakipenda kucheza na kufurahi na wenzao kwenye kikosi hicho kukiwa na jambo la ndani zaidi yupo kiongozi ambaye amekuwa akielewana nao.

Wacolombia hao wamekuwa wakijituma katika mazoezi ambayo yanaendelea, Azam Complex, Chamazi huku Navarro akionyesha kuwa na uchu na nyavu, hivyo mabeki wa Ligi Kuu wanapaswa kujiandaa naye kwani ni mshambuliaji mwenye kasi na maarifa kama ilivyo wachezaji wengi kutoka Amerika ya Kusini.

Kwa upande wake kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo alishaweka wazi mapema hawatawapa presha wachezaji hao hivyo huenda wakaanza kupewa nafasi taratibu kwa kupewa dakika chache za kucheza kwenye kikosi hicho ili kuzoea mikiki ya Ligi Kuu Bara ambayo imerejea baada ya kusimama kwa wiki chache kufuatia ushiriki wa Taifa Stars kwenye fainali za Afcon huko Ivory Coast.

Februari 9, Azam itakuwa ugenini kucheza mchezo wa kiporo utakaokuwa wa 14 kwa msimu huu katika Ligi Kuu dhidi ya Simba kama Navarro na Fuentes watapata nafasi ya kucheza watakuwa wachezaji wa kwanza kutoka Colombia kucheza ligi hiyo inayoshika nafasi ya sita Afrika kwa ubora kulingana na Shirikisho la Soka la Kimataifa la historia na Takwimu (IFFHS), ikiwa imeporomoka kwa nafasi moja kutoka nafasi ya tano iliyokuwa inaishikilia tangu mwaka juzi.

SOMA NA HII  KOCHA WA KAIZER CHIEFS MBIONI KUPEWA KIBARUA SIMBA...KIGOGO WA NDANI KABISA AFUNGUKA A-Z MCHAKATO ULIVYO...