Home Habari za michezo MSUVA AIKATAA YANGA BAADA YA KUTUA BONGO

MSUVA AIKATAA YANGA BAADA YA KUTUA BONGO

Mshambuliaji Simon Msuva yupo nchini tayari baada ya kutua tangu majuzi kimyakimya, kuwahi kambi ya timu ya taifa inayojiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), lakini akianzia kambi ya timu ya Kilimanjaro Stars ya Bara inayocheza leo na Zanzibar Heroes katika mechi maalumu ya kirafiki mjini Unguja.

Msuva ametua, huku mabosi wa Yanga wakiendelea na mazungumzo naye ili kumsainisha, lakini hapohapo mabosi wa klabu hiyo wakalazimika kufumua mahesabu yao ndani ya dili hilo.

Yanga inaamini kama itamepata Msuva, aliyeachana na JS Kabylie ya Algeria utakuwa usajili muhimu ndani ya kikosi hicho wakitafakari juu ya ubora alionao mshambuliaji huyo wa zamani wa timu hiyo.

Msuva tayari ameonyesha kuingia kwenye laini ya Yanga akiwataka kusubiri atue nchini ili aongee na familia yake kwanza kwa kina kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho ya kurejea Jangwani ikiwa ni baada ya kuondoka mwaka 2017 kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi akianzia Morocco kisha Saudia Arabia halafu Algeria.

Yanga imemuwekea fedha ya kufuru mezani ambayo imemfanya ajiulize mara mbili kabla ya kuamua wapi atue, ingawa mshambuliaji huyo akili yake ikitamani kuendelea kucheza nje.

Kama Yanga ikimnasa Msuva klabu hiyo inaona ni bora isajili mshambuliaji mmoja pekee wa kigeni na badala yake wahamishie nguvu eneo lingine wakitaka kumshusha winga wa maana.

Rekodi za Msuva zimekubalika pia kwa Kocha Miguel Gamondi akiwaambia kwa kifupi mabosi wa klabu hiyo kwa kuwaambia; “Nileteeni tu, atatufaa hapa.” maneno ambayo ni kama yamewafanya viongozi kuingiza gia kubwa kukimbizana na usajili huo.

Yanga haitaki kufanya makosa kwa Msuva apande ndege ya kwenda Ivory Coast na kikosi cha Taifa Stars kabla ya kumaliza dili hilo.

“Unajua hii ni mara ya pili kama sio ya tatu tunarudi kwake, kwa namna hawa Waarabu walivyomfanyia ni bora sasa akarudi kwanza kutuliza akili hapa kwetu, kwa kuwa ameshafika acha tusubiri kuona nini ataamua na familia yake,” alisema bosi mmoja wa juu.

Mbali na Msuva, Yanga inahusishwa na mastraika Jonathan Sowah wa Medeama ya Ghana, Ranga Chivaviro wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Sankara Karamoko wa Ivory Coast. Pia, inamzengea Moses Phiri anayedaiwa kuandika barua yakutaka kuondoka Msimbazi.

SOMA NA HII  KUTOKA KWENYE SIMULIZI ZA KNUD, MPAKA KWENYE USHINDI MKUBWA MERIDIANBET.....!