Home Habari za michezo MTANANGE SIMBA,YANGA MILIONI 100 MAPINDUZI CUP

MTANANGE SIMBA,YANGA MILIONI 100 MAPINDUZI CUP

Habari za michezo

Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2024 imetangaza zawadi za washindi wa msimu huu kwa kuweka bayana bingwa ataondoka na kitita cha Sh100 milioni, huku wa pili akizoa Sh70 milioni kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu za Visiwani Zanziabar, Tanzania Bara zikiwamo Simba na Yanga na baadhi kutoka nje ya nchi.

Zawadi hiyo ni mara mbili na ile ya msimu uliopita na bingwa alipata Sh50 milioni, hii ni kutokana na ukubwa wa michuano hiyo ikiakisi Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbarouk Othman alisema mbali na fedha hizo zawadi nyingine pia zitakuwepo ikiwamo ya mchezaji bora, kipa bora na nyinginezo ambazo zimo kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Kamati hiyo pia imetoa taarifa ya kujitoa kwa timu za Bandari ya Kenya na URA ya Uganda kutokana na changamoto ambazo zipo nje ya uwezo wao na nafasi zao zitachukuliwa na JKU ya Zanzibar na Jamus FC kutoka Sudan Kusini.

Kujitoa kwa timu hizo kumebadilisha makundi ya awali na sasa kundi A litaundwa na timu za Azam FC, Vital’O, Chipukizi United na Mlandege FC, huku kundi B likiwa na timu za JKU, Simba, APR na Singida Fountain Gate, wakati Kundi C litakuwa na timu za Jamus FC, Yanga, KVZ na Jamhuri, mfumo wa mashindano hayo utabaki ule ule.

Katibu wa Kamati ya michuano hiyo, Nasra Juma Mohammed alisema waliumiza kichwa sana kutafuta timu ambazo zitaziba nafasi hizo na kwa bahati nzuri wamezipata JKU na Jamus FC na kuanika viingilio akisema cha juu kikiwa Sh10,000 wakati cha chini ni Sh3,000 kwenye Uwanja wa Amaan unaotumika kwa mechi hizo.

SOMA NA HII  GAMONDI AMEKUNA KICHWA KUHUSU KONKONI KISHA ASEMA HAYA