Home Habari za michezo KUELEKEA ‘KARIAKOO DABI’….MIUJIZA YA MWEZI ‘APRIL’ KUENDELEA KUIBEBA SIMBA MBELE YA YANGA..?

KUELEKEA ‘KARIAKOO DABI’….MIUJIZA YA MWEZI ‘APRIL’ KUENDELEA KUIBEBA SIMBA MBELE YA YANGA..?

Habari za Michezo leo

Wakati ratiba ya mechi ya kiporo baina ya timu Simba na Yanga ‘Kariakoo Derby’ kuwa itapigwa Aprili 20 mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa, mwezi huu umeonekana kuwa wa bahati kwa Simba.

Mchezo huo namba 180, awali hakupangiwa ratiba katika maboresho yaliyofanywa na kutangazwa Februari 2024, na sasa utapigwa mwezi huu, yaani siku 12 kutoka leo Aprili 8, 2024.

TPBL imetangaza tayari klabu za Simba na Yanga pamoja na wadau wengine wa Ligi Kuu wamepatiwa taarifa zote kuhusiana na mchezo huo na maandalizi yake yanaanza mara moja ili kuhakikisha unafanyika katika kiwango cha juu kinachoendana na hadhi ya michezo mikubwa ya ligi ya sita kwa ubora Afrika.

Ofisa habari wa Yanga Ally Kamwe, amethibitisha kupokea ratiba hiyo na timu yao ipo tayari kwa mechi lakini amewaomba TPBL kuhakikisha kunakuwa na VAR uwanjani hapo ili kutenda haki.

“Tumepokea na tayari tumeanza maandalizi na mechi hiyo. Simba wanakumbuka tulichowafanya na sasa tunakwenda kuendeleza pale pale,” alisema Kamwe na kuongeza;

“Ninachosisitiza kwa TPLB ni kuhakikisha VAR inakuwepo uwanjani pale siku ya mechi kwani tumejipanga kufanya makubwa lisije kutokea la kutokea ikawa tabu baadaye, hili ni ombi kama wanaweza kulifanyia kazi itakuwa vizuri.”

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema ni mechi ya kisasi kwao.

“Tulipoteza mechi ya kwanza hivyo hii ya sasa ni kisasi kwetu. Hatutaki kufungwa mara mbili na Yanga hivyo tunajipanga kuhakikisha tunashinda mchezo huo,” alisema Ahmed ambaye timu yake imerejea jana kutoka Misri.

Katika mchezo huo, Yanga ndio itakuwa mwenyeji baada ya Simba kuhodhi mechi ya duru ya kwanza na kuchapwa 5-1 kwa mabao ya Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili huku lile la kufutia machozi kwa Simba likiwekwa nyavuni na Kibu Denis ambaye hajafunga tena kwenye ligi hadi sasa.

APRILI YA SIMBA

Tangu mwaka 2010, rekodi zinaonesha timu hizo mbili zimekutana katika mwezi Aprili mara nne na Simba kuwa mbabe zaidi kwenye mwezi huo.

Katika mechi hizo nne Simba imeshinda mbili na kutoa sare mbili huku Yanga ikiwa haijashinda mechi hata moja.

Mchezo wa kwanza ulipigwa Aprili 19, 2014 na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ambapo Simba ilitangulia kufunga kupitia Haruna Chanongo dakika ya 75 na Yanga kuchomoa dakika ya 86 kupita kwa Simon Msuva wachezaji ambao kwa sasa hawapo na timu hizo.

Mechi nyingine ilikuwa msimu wa 2017/2018, ikipigwa Aprili 29, 2018 na Simba kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Erasto Nyoni dakika ya 37.

Mechi nyingine iliyowakutanisha wakali hao wa Dar es Salaam mwezi April ilikuwa April 30, 2022 na kumalizika kwa suluhu wakati huo kocha wa Yanga alikuwa Cedric Kaze huku Simba ikiwa chini ya Pablo Franco.

Mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo mwezi huu ilipigwa Aprili 16, 2023 na Simba kushinda 2-0, ikipata bao la kwanza kupitia kwa Henock Inonga kwa kichwa dakika ya kwanza ya mchezo kabla ya Kibu Denis kushindilia msumari wa pili dakika 32 na nyota wote hao bado wapo Msimbazi.

Hata hivyo, mechi hiyo haitakuwa kinyonge kwani kutokana na rekodi za timu hizo hivi karibuni kwani mechi tano za mwisho walipokutana, Simba ilishinda mbili, Yanga ikashinda moja na mbili kumalizika kwa sare.

Simba na Yanga zote kwa sasa zipo kwenye mbio za ubingwa, Yanga ikiongoza ligi na alama 52 baada ya mechi 20, huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na alama 45 ilizovuna baada ya michezo 19, Azam yenye pointi 47 baada ya mechi 21 ipo nafasi ya pili.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUICHAPA DODOMA JIJI....UNAAMBIWA FADLU HUKO SIMBA KAKASIRIKA BALAA...