Home Habari za michezo TATIZO LA SIMBA MSIMU HUU HILI HAPA….WAKISHINDA KUTATUA WATALIA SANA TU….

TATIZO LA SIMBA MSIMU HUU HILI HAPA….WAKISHINDA KUTATUA WATALIA SANA TU….

Habari za Simba leo

Ligi Kuu Tanzania Bara ndio nguzo kuu ya pembeni ambayo kwa sasa Simba imeiegemea licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa watetezi wa taji Yanga inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 52 na Azam FC iliyoonekana msimu huu imekuja tofauti katika ligi hiyo.

Simba ilianza kutolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa nyumbani bao 1-0 kisha kulala ugenini kwa mabao 2-0 mbele ya Al Ahly ya Misri. Iliporejea katika mashindano ya ndani, mambo yaliwaendea tena kombo katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA).

Katika hatua hiyo, Simba ilijikutaka ikitolewa kwa mikwaju ya penalti 6-5 na Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma baada ya dakika 90 za pambano hilo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Matokeo ya mchezo huo ni kama yamekoleza moto kutokana na kile ambacho kinaendelea katika klabu hiyo kiasi kwa sasa kuwa na presha kubwa mbele yao katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ni shindano pekee lililosalia mbele yao kabla ya kumalizika kwa msimu.

Hivi ni vikwazo vitano ambavyo Simba wanapaswa kukabiliana navyo kwa haraka ili kuendelea kupigania ubingwa wa ligi vinginevyo wanaweza kumaliza msimu ikiwa na Ngao ya Jamii tu iliyolibeba mapema Agosti mwaka jana, jijini Tanga kutokana na kasi waliyonayo wapinzani wake.

WANACHAMA/MASHABIKI

Hili ni moja ya maeneo muhimu katika timu. Washabiki, wananchama na wadau wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mpira, hamasa huchochea wachezaji kupambania matokeo na vile ambavyo wanajitokeza viwanjani huchangia mapato ambayo husaidia katika shughuli mbalimbali za uendeshaji.

Hali ilivyo kwa sasa mashabiki wa Simba wamekatishwa tamaa na timu yao, wengi wamekuwa wakiwanyooshea vidole viongozi wao kwa shutuma mbalimbali ikiwemo maamuzi waliyoyafanya ya kuachana na Jean Baleke na kumtoa kwa mkopo Moses Phiri huku wakisajili Pa Omar Jobe, raia wa Gambia na Freddy Michael Koublan ambao mpaka sasa wameshindwa kuonyesha makali yao.

Mategemeo ya mashabiki hao ilikuwa ni kuona viongozi wakileta washambuliaji wa maana zaidi ya wale walioondoka lakini imekuwa tofauti.

Baadhi ya viongozi wa zamani wa timu hiyo, wameanza kuwatuliza wanachama kwa kuandika jumbe mbalimbali, huku wakiahidi Simba imara inakuja, miongoni mwa watu hao ni pamoja na Mtendaji mkuu wa zamani, Crescentius Magori.

Hakuna namna mashabiki wanatakiwa kuwa nyuma ya timu yao kwa kutoa sapoti kwa wachezaji wao ili kuendelea na mapambano katika ligi kwani bado kimahesabu wana nafasi ya kutwaa ubingwa kulingana na idadi ya michezo iliyosalia mbele yao, bado wanamchezo dhidi ya Yanga na Azam FC.

VIONGOZI

Huu ni wakati wa viongozi wa Simba kuondoa makandokando waliyonayo kwani inaelezwa baina yao kuna makundi yanayochochea kuwepo kwa mpasuko ambao matokeo yake hayaonekani kuwa na afya kwa maendeleo ya timu.

Mpasuko huo unatajwa kuwepo kwa viongozi wa juu, upo upande mmoja ambao unautegea mwingine ili kuona ukiharibikiwa, viongozi wote hao wanatajwa kuwa na nguvu kwenye klabu hiyo, hivyo huu ni wakati wa kuondoa tofauti zao na kusimama kila mmoja kwa nafasi yake kwa ajili ya timu.

Kama kila mmoja ataendelea kushupaza shingo yake huku akimtupia mwenzake lawama kwa kutumia wapambe ambao wamekuwa wakitumia vyombo vya habari ni wazi huenda Simba ikashindwa kufua dafu mbele ya Yanga na Azam.

Kama Simba itashindwa kumaliza msimu katika nafasi mbili za juu huenda msimu ujao mashindano ya kimataifa wakawawatazamaji wakati wanajenga upya kikosi chao. Kila mmoja anatakiwa kusimamia kauli yao mbinu ya ‘Simba nguvu moja’ kusiwepo mtu au watu kujiona wao ni bora kuliko wengine.

FOMU YA TIMU

Simba haijafanya vizuri katika michezo yake mitatu iliyopita katika mashindano yote huo ni mwenendo mbaya ambao wanatakiwa kuubadilisha na kurejea katika wimbi la ushindi ambalo litarejesha hali ya kujiamini ya mchezaji mmoja mmoja na timu kwa jumla.

Kwa kubadili upepo huo wa mambo ‘fomu’ ni wazi kuwa Simba itakuwa na nafasi ya kupigania ubingwa wa ligi ambao mara yao ya mwisho kutwaa ilikuwa 2020/21.

Bahati nzuri hata baadhi ya wachezaji wamelitambua hilo akiwamo Fabrice Ngoma aliyewakumbusha wachezaji wenzake, kujituma kwa asilimia 80-100 kusaidia kubadilisha upepo wa matokeo, kwani bado wana nafasi ya kufanya makubwa kwa mechi zilizosalia zinazoweza kuwapa taji pekee kubwa msimu huu.

MOTISHA

Muda mwingine motisha husaidia wachezaji kujituma hivyo viongozi wa Simba wanatakiwa kutolea macho eneo hili na kama kuna madeni kama inavyoelezwa na baadhi ya wadau basi ni vyema kuwalipa ili kuchochea morali za nyota wao.

Motisha zina nafasi yake katika soka na kwa kutambua umuhimu wake ndio maana rais wa nchi, Samia Suluhu Hassan alikuwa akitoa zawadi ya fedha kwa kila bao litakalofungwa na Simba na Yanga michuano ya kimataifa tangu msimu uliopita wa 2022/23.

Matokeo yake tuliona namna ambavyo vikosi hivyo vilikuwa vikipambana na kufanya vizuri katika michuano hiyo, hili ni eneo muhimu viongozi wa Simba wanatakiwa kulitazama ili kuokoa jahazi.

BENCHIKHA

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anatakiwa kutafuta namna nzuri ya kuwajenga wachezaji wake kimwili na kiakili na kutafuta mbinu bora zaidi za kiufundi ambazo zitawasaidia kufanya vizuri katika michezo iliyosalia. Kwa mujibu wa ratiba michezo 10 kwa Simba iliyosalia ni dhidi ya Yanga, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Namungo, Tabora United, Azam FC, Kagera Sugar, Geita Gold, KMC na JKT Tanzania.

Benchikha ni kocha mwenye misimamo na asiyependa kufeli, hii ikiwa na maana akikomaa na wachezaji wana nafasi ya kutuliza hali ya mambo, kwani kwa sasa mashabiki wanachotaka ni kuona timu inapata matokeo mazuri bila kujali matokeo hayo yanaopatikana vipi mbele ya wapinzani wao.

WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohammed Badru, anaamini hiki ndio kipindi ambacho wadau, mashabiki na viongozi wa Simba wanatakiwa kuwa pamoja ili kuhakikisha timu inamaliza vizuri msimu.

“Matatizo mengine yanatakiwa kuangalia baada ya msimu kumalizika, hiki sio kipindi cha kuanza kumuona fulani mbaya, waendelee kushikamana kwa sababu mpasuka kati yao unaweza kuathiri zaidi mwenendo wa timu,” alisema.

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr ambaye aliishuhudia timu hiyo katika michezo yake miwili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, amewataka viongozi wa timu hiyo kuingia gharama kwa kufanya maboresho ya nguvu ambayo yataongeza nguvu ya kikosi.

“Sio kwamba Simba ina kikosi kibaya sana hapana, lakini wanatakiwa kuongeza watu wengine wa nguvu katika maeneo muhimu ikiwemo ushambuliaji ili kuongeza ufanisi wa timu, unataka kufanya vizuri Afrika lazima uwe na wachezaji wa daraja la juu,” alisema kocha huyo.

SOMA NA HII  LWANGA, ONYANGO WAREJEA KAZINI