Home Uncategorized MZEE YANGA NA UMRI WAKE WA MIAKA 85 LAKINI MAISHA YA KIJANA...

MZEE YANGA NA UMRI WAKE WA MIAKA 85 LAKINI MAISHA YA KIJANA WA SEKONDARI!

Na Saleh Ally
JANA ilikuwa siku muhimu na maalum kwa wanachama na mashabiki wote wanaoiiunga mkono klabu ya Yanga.

Rangi mbili maarufu, njano na kijani na ile ya tatu nyeusi, zinakamilisha muonekano halisia wa klabu hiyo kongwe zaidi kwa zile za soka ambayo ilianzishwa mwaka 1935.

Kwa mwanadamu kama utafikisha miaka 85, hakika ni mtu mzima, mzee hasa ambaye utakuwa ukisubiri majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Kwa maana kama muda wa kupambana kutafuta maisha utakuwa umepita. Wakati huo utakuwa ukimalizia kula matunda yako kama ulifanya juhudi kutafuta maisha kwa kila namna.

Wakati ukiwa unakula matunda, pia utakuwa ni nafasi ya kutadhmini kile ulichokifanya kuwa kilikuwa sahihi au la. Ulipambana kweli au ulikuwa mzembe.

Si vibaya ukisema wakati huo unakuwa ni ule wa mavuno.
Yanga ni taasisi, itaendelea kuishi zaidi ya miaka mingine 100. Lakini hii 85 nayo inapaswa kuwa kipimo kwa “Mzee Yanga” kujipima kutokana na alichokifanya kwa muda wote huo.

Nimeona wengi wakisherekea miaka hiyo ya Yanga jambo ambalo ni sahihi na wanapaswa kujiuliza kuwa, miaka hiyo 85 wakati wanaisherekea, imekuwa na faida kiasi gani ndani ya klabu hiyo ambayo bado inaweza kujivunia ukongwe.

Kujivunia ukongwe ukiwa hauna kitu ni sawa na mzee aliyefikisha umri wa miaka 85 halafu anakuwa anaishi maisha ya shida. Hana sehemu ya uhakika ya kuishi, fedha za kulipa matumizi yake ni shida na bado ni tegemezi.

Mzee akiwa na umri huo, akawa anakosa vitu hivyo, tutasema aliutumia ujana wake vibaya. Tunasema hivyo kwa kuwa tunaona kuwa uzeeni, maisha yamekuwa bado ya kubangaiza kwa kuwa hakuwa amejiweka sawa wakati wa ujana wake.

Yanga leo hii, inaweza ikawa ni Mzee Yanga ambaye kuna sehemu alicheza sana na maisha, ndiyo maana unaona pamoja na mwonekano wake wa nje, yaani anapokuwa barabarani kuonekana anang’ara, bado hana makazi mazuri, hajajitegemea sahihi kwa kuwa ni tegemezi na hana mali za kutosha.

Hapa makazi, najaribu kukuonyesha jengo la makao makuu ya Yanga pale Kaunda jijini Dar es Salaam, ni kitega uchumi ambacho hakitumiki sawasawa na kimekuwa kama gofu, hakina faida kubwa kwa Yanga.
Angalia Uwanja wa Kaunda ambao ulijengwa na wazee wa Yanga miaka hiyo zaidi ya 30 iliyopita, leo hata kuutunza au kuhakikisha upo imeshindikana. Bado makazi yake na sehemu ya kufanyia kazi ni za kubahatisha au kubabia licha ya kuwa na miaka 85.

Nimesema ni tegemezi, leo Yanga sidhani kwenye akaunti hata kama wana Sh milioni 500 ambazo zinakuwa ni sehemu ya akiba ya baadaye. Lakini pia hawana vitega uchumi vinavyoweza kuwafanya kutulia katika umri huu wa miaka 85.

Yanga bado inatangatanga kwa sasa, lazima ihangaike kulipa mishahara, ihangaike kwa shida kwelikweli kulipa fedha za wafanyakazi wake na kadhalika.

Hakuna ubishi, hali ya sasa ya Yanga ikiwa inatimiza miaka 85, inaonyesha huko nyuma au miaka ya katikati hakukuwa na umakini na mambo yalikwenda shaghalabaghala. Mambo yalikuwa katika yanapelekwa ndivyo sivyo kwa maana ya nidhamu na nia njema ya kuiendeleza Yanga.


Hapa nazungumzia kukosa viongozi sahihi ambao walikuwa na malengo wa kuifanya Yanga iwe bora baadaye na huenda hawakuamini kuwa kila siku zinavyokwenda, miaka inahesabika.

Nimeanza kuandika kuhusu Yanga miaka 20 ilivyopita, ninaamini wengi sana wakati huo hawakuwa wameanza kuifuatilia au kuijua hasa kwa vijana wengi walio katika shule za msingi na sekondari katika kipindi hiki. Lakini niwaibie tu kidogo, viongozi wengi walikuwa Yanga kwa ajili ya matumbo yao na hili limeendelea hadi wakati wa kizazi hiki.

Ndio maana tunaiona Yanga inayokwenda mwendo wa kinyonga hadi leo. Inayoonekana ina umri mkubwa lakini inakosa mambo mengi yanayoweza kuipa sura ya “Mzee aliyejituma wakati wa ujana wake.”

Miaka 85 ya Yanga iwe chachu ya kujitathmini na kuangalia miaka hiyo yote kama ilitumika vibaya, basi kuanzia mwaka wa 86, mambo yaende kisayansi zaidi kwa kuwa baadaye Yanga itakuwa na miaka 90 na tathmini itarudi katika kile walichofanya.

Kuendelea kulipua mambo, ni kuendelea kuifanya Yanga iwe kubwa kwa umri lakini maendeleo ya kitoto. Na kwa bahati mbaya, Yanga yenyewe haizungumzi na wanaoiwakilisha ni watu hivyo, mafanikio na kufeli kwake kunawahusisha watu ambao ni wanachama na mashabiki, wanaoongozwa na viongozi na watumishi kama vile wachezaji.
SOMA NA HII  HIVI NDIVYO USAJILI WA SIMBA UTAKAVYOKUWA