HIVI karibuni kuna jambo kubwa kwenye soka linakwenda kutokea. Achana na ubingwa wa Yanga ambayo imetangaza leo, lakini kuna lingine ambalo linalomhusisha staa wa Simba, Mzambia Clatous Chama kusaini mkataba mpya katika moja ya timu kubwa Afrika, huku Stephane Aziz Ki akimvuta Jangwani Mwamba huyo wa Lusaka.
Chama yupo Dar es Salaam na anaishi kifahari huku simu yake ikiwa bize kuita namba za mabosi wa timu mbalimbali Afrika zinazotaka huduma yake kwa msimu ujao zikiwemo kutoka kwa mabosi wake wa sasa, Simba, sambamba na mabingwa wa ligi watarajiwa, Yanga.
Mkataba wa Chama na Simba unaisha mwishoni mwa msimu huu na tayari uongozi wa Wekundu wa Msimbazi hao umeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya mchezaji huyo ambaye ni kipenzi cha mashabiki lakini hadi sasa hawajakubaliana jambo na hajasaini mkataba mpya.
Simba inataka kumuongezea Chama mkataba wa mwaka mmoja ambao hautapishana sana na mkataba unaomalizika kwa maana ya mshahara na pesa ya usajili lakini Mwamba huyo ametaka mkataba wa miaka miwili utakaokua na maboresho zaidi jambo ambalo halijakubalika kwa baadhi ya vigogo wa timu hiyo na kuchelewesha dili la staa huyo kusaini mkataba mpya.
Katika Sekretarieti na Bodi ya Wakurugenzi wa Simba kuna makundi matatu kuhusu jambo la Chama. Kuna baadhi ya viongozi wanataka Chama abaki Simba kwa dau lolote lile, wapo wanaotaka abaki lakini timu isitumie pesa nyingi juu yake pia wapo ambao wanahitaji Kiungo huyo aondoke wakiamini muda wake umekwisha ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao.
Vikao vinaendelea juu ya hilo. Hata hivyo Chama hana presha na ameendelea kuponda maisha ndani ya Dar huku akiwa na ofa kutoka timu nyingine ikiwemo Yanga ambayo anaweza kutua muda wowote kama Simba haitafanya kile anachotaka.
Wakati hilo likiendelea, inafahamika kuwa Chama kwa sasa anaishi kishua zaidi na ilivyokuwa mwanzo huku Yanga ikitajwa kuwa Chanzo. Staa huyo wa timu ya taifa ya Zambia, amebadili gari alilokuwa akitembelea ambalo alipewa na Simba, lakini pia amehama eneo la kufanyia mazoezi binafsi ‘Gym’ na sasa anapiga tizi sehemu tofauti na ile ya mwanzo.
AZIZ KI AMVUTA YANGA
Staa wa Yanga Aziz Ki ni swahiba mkubwa wa Chama. Ndani na nje ya maisha ya soka ni marafiki wakubwa. Haijaishia hapo, wawili hao kwa mara kadhaa wamekuwa wakifanya mazoezi kwenye ‘gym’ moja iliyopo Mikocheni Dar es Salaam. Ni gym ambayo mastaa wengi hufanya mazoezi pale akiwemo Luis Miquissone wa Simba, Pacome Zouzoua na Koassi Yao wa Yanga.
Aziz Ki aliwahi kuumbia uongozi wa Yanga usajili wachezaji wenye uzoefu na mashindano ya kimataifa kama Chama ili timu hiyo itwae ubingwa wa Afrika kwa ngazi ya klabu. Ni jambo ambalo Yanga inalifanyika kazi kwa sasa na tayari imeanza mazungumzo ya kumpata Chama huku ikitajwa kumuwekea ofa kubwa mezani kwake licha ya kwamba bado hawajafika muafaka.
Aziz Ki anamkubali Chama na anaamini wakicheza kwa pamoja wanaweza kuleta mabadiliko na mafanikio makubwa ndani ya timu.
Jambo lingine ni mkataba wa Aziz KI na Yanga kuelekea mwisho na hadi Staa huyo kuwindwa na timu vigogo wa Afrika na nje ya Afrika jambo lililowafanya Yanga kuanza kutafuta mbadala wake kama tahadhari.
Yanga inajua fika Aziz Ki kwa sasa ana ofa kubwa ambazo kama ataamua kuondoka Yanga, hakuna wa kumzuia lakini timu hiyo imeendelea kufanya mazungumzo na Staa huyo kupitia kwa Rais wa timu hiyo, Hersi Said ili kuhakikisha inamshawishi staa huyo kubaki.
Wakati Yanga ikifanya hivyo pia iko sokoni kutafuta wachezaji watakaoziba mapengo ya wale watakaoondoka na lengo lao kubwa kwenye eneo la kiungo ni kumshusha Chama, Jangwani.
Chama ambaye kwa msimu huu hadi sasa amefunga mabao saba kwenye ligi alitua Simba kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa msimu wa 2018/2019 akitokea Lusaka Dynamos ya nchini kwao na kucheza kwakiwango kikubwa katika timu hiyo jambo lililopelekea mwaka 2021 kuuzwa kwa pesa ndefu, RS Berkane ya Morocco lakini baadae mwakaq 2022 alirejea Simba ambapo yupo hadi sasa na mkataba wake utatamatika mwezi ujao.
Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema Simba imewekeza nguvu kwenye mechi za ligi zilizobaki wakati huo huo ikifanya tathmini ya kikosi kizima kwa kuangalia ni wachezaji gani wanastahili kubaki ama kuondoka ndani ya timu hiyo.
“Pamoja na yote, tunalenga kujenga timu imara kwa msimu ujao. Kuna wachezaji tutaachana nao lakini pia wengine watabaki na tutasajili wengine. Tunataka kubaki na wachezaji wenye ari na Moyo wa kuipigania Simba na tayari mazungumzo yameanza na yanaendelea,” alisema Ahmed.
Credit:- Mwanaspoti