Home Habari za michezo WINGA SIMBA AMPELEKA MORRISON JESHINI…..

WINGA SIMBA AMPELEKA MORRISON JESHINI…..

Habari za Michezo

Winga wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa anakipiga JKT Tanzania, Shiza Kichuya, ameweka wazi kutamani kucheza na Bernard Morrison katika kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo JKT Tanzania na timu nyingine zinazomilikiwa na majeshi, hazina ruhusa ya kusajili wageni kwa sasa mpaka pale sheria zitakapobadilishwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kichuya, alisema angependa kuona nyota huyo raia wa Ghana anasajiliwa katika timu hiyo kutokana na uwezo aliokuwa nao na anaamini atawasaidia kufanya vyema kwenye msimu mpya.

Kichuya alisema nyota huyo wa zamani wa Simba na Yanga anaijua vyema Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo uwepo wake utaongeza ubora wa timu yao.

“Akisajiliwa JKT Tanzania nitafurahi sana kwa sababu ni mchezaji mkubwa, ana uzoefu, ni mchezaji wa kimataifa, ana vitu vingi, ana kipaji kikubwa, anajua muda huu nini timu inatakiwa kufanya, na wakati wa kuibeba timu mgongoni mwake kwa kutumia uwezo na kipaji alichonacho, nadhani kila mtu anafahamu ni vitu gani alikuwa anavifanya akiwa Simba na Yanga,” alisema Kichuya.

Morrison alionekana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, unaomilikiwa na Maafande hao katika mchezo wa ‘play off’, kati ya JKT Tanzania dhidi ya Tabora United uliomalizika kwa suluhu.

Baada ya mechi hiyo kumalizika, Kichuya na Said Ndemla, ambao waliwahi kuichezea Simba, walionekana kufurahi kumwona Morrison na kuzungumza kwa muda mrefu.

Kwa sasa Morrison ni mchezaji wa FAR Rabat ya Morocco, lakini inadaiwa yuko nchini kwa ajili ya kupata matibabu baada ya kuumia akiwa na timu hiyo.

Mbali na nyota huyo, wachezaji wengine wa kigeni waliowahi kuzitumikia Simba, Yanga na Azam wapo nchini kwa kile kinachoelezwa kusaka timu.

SOMA NA HII  ILE ISHU YA MWAKINYO KUZICHAPA MAREKANI KUMBE IKO HIVI BANA...APOROMOKA UBORA WA VIWANGO...