Home Habari za Simba Leo FADLU BADO ANALISUKA JESHI LA SIMBA…MSIKIE MOGELLA.

FADLU BADO ANALISUKA JESHI LA SIMBA…MSIKIE MOGELLA.

Habari za Simba- Fadlu

Licha ya kupiga tizi la maana ni kwamba hadi sasa Kocha wa Simba Fadlu Davids bado hajakipata kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Hadi sasa ni wachezaji wachache pekee wana uhakika kiasi wakiwemo mabeki wawili Che Malone Fondoh, Karaboue Chamou na viungo Jean Ahoua na Joshua Mutale huku wengine wakiendelea kuchuana na kupishana.

Fadlu anaendelea kuwasoma zaidi wachezaji hao na wikiendi hii watashuka uwanjani kucheza mechi nyingine mbili kabla ya kujiandaa kurejea nchini mapema wiki ijayo kujiandaa na Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 3.

Kisha kujipanga kwa mechi mbili za Ngao ya Jamii ikiwamo ile ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga itakayopigwa Agosti 8 kuanzia saa 1:00 usiku Kwa Mkapa.

Katika mechi za msimu uliopita za michuano hiyo, Simba ilianza kwa kuitambia Singida Fountain Gate kwa penalti kisha kucheza fainali na Yanga iliyokuwa imeifunga Azam kwa mabao 2-0 na dakika 120 ziliisha kwa timu hizo kutofungana na kulazimika kupigiana penalti na Mnyama akapata 3-1 na kurejesha tuzo hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Wananchi kwa misimu miwili mfululizo nyuma.

ZAMOYONI MOGELLA AFUNGUKA.

Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ amekisifia kikosi kipya cha Simba, lakini akatoa angalizo kwa kusema ni ngumu kwa timu yenye idadi kubwa ya wachezaji wapya kufanya vizuri ndani ya kipindi kifupi, hivyo ni vyema mashabiki wa Msimbazi kutambua hilo wakati kocha wao, Fadlu Davids akiendelea kukisuka upya.

“Ninachokiona kwa sasa kocha anapambana kupata muunganiko, hili ni jambo ambalo huwa linahitaji muda, kama ikitokea wakielewana kwa haraka hiyo itakuwa bahati, natamani mashabiki wa Simba waonyeshe ukomavu kwa kuwa nyuma ya timu yao hasa kipindi hiki ambacho inajengwa,” alisema Mogella aliyewahi kuwika na timu kadhaa ikiwamo Yanga na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amewataja Steven Mukwala na Jean Charles Ahoua kama maingizo mapya katika kikosi cha Simba ambayo yanaweza kurahisisha kazi kwa kocha Fadlu kutokana na ubora ambao ameona kutoka kwao, amekuwa akivutiwa nao.

“Makocha tumekuwa wafuatiliaji, nipo Ghana lakini huwa nafuatilia ligi za nchi mbalimbali, najua kuwa Simba kwa sasa wanajaribu kukijenga upya kikosi chao, wamefanya usajili mzuri mfano Mukwala amefanya vizuri hapa (Ghana) ni kati ya washambuliaji hatari, namtabiria mazuri,” alisema Hans aliyewahi kuzinoa Singida United na Azam aliyeongeza;

“Ahoua naye amefanya vizuri Ivory Coast, jambo ambalo linaweza kuwa changamoto kwa Fadlu ni moja tu ambalo ni kupata kile kilichobora kwa kila mchezaji, kuwa na wachezaji wazuri ni moja lakini kupata kilichobora kwa wachezaji katika muundo wa timu vile anataka icheze ni jambo jingine, akifaulu hapo huenda Simba ikarejea katika makali yake.”

SOMA NA HII  WAKATI SAKHO HAJAPOA BADO...OKRAH ATABIRIWA UFALME SIMBA SC...KAPOMBE AFUNGUKA WANAVYOSHINDANA KUMKABILI...