Home Habari za Simba Leo KOCHA WA SIMBA ASOTA RUMANDE…SIKU 609

KOCHA WA SIMBA ASOTA RUMANDE…SIKU 609

Habari za Simba-Muharami Simba

Aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultani (40) na wenzake wanaendelea kusota rumande kwa siku 609 sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilka.

Muharami na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, Novemba 21, 2022 na kusomewa mashtaka.

Hata hivyo, tangu wafikishwe mahakamani hapo siku hiyo hadi leo Julai 23, 2024, washtakiwa hao wamefikisha siku 609 sawa na mwaka mmoja na miezi minane na siku nne wakiwa rumande kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Licha ya upelelezi wa kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 71/2022 kutokamilika, pia washtakiwa wanaendelea kusota rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria. Pia mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, leo wakili wa Serikali Frank Rimoy aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo Serikali inaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mkazi Mkuu anayesikiliza shauri hilo, Aaron Lyamuya aliahirisha shauri hilo hadi Agost 5, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana.

Washtakiwa hao wanatetewa na wakili Daudi Mzeri na kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.

Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko mkazi Magole; Maulid Mzungu maarufu mbonde (54) mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na Muharami.

Wengine ni John John maarufu Chipanda (40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.

Awali washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano, lakini Septemba 23, 2023 Mkurugenzi wa mashtaka nchini( DPP) aliwabadilishia hati ya mashtaka kwa kuwaongezea mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha na kisha kuwasomea upya mashtaka yao.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabiliwa watu wote ambapo Inadaiwa  tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti  na ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.

Shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja  walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 27.10.

Vile vile,  Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa  wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa Kilo 7.79.

Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina  ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Katika shtaka la nane inadaiwa kuwa Aprili 20,2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies LTD akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

SOMA NA HII  RAISI WA SIMBA MO DEWJI...KILA SIKU UNALALAMIKA HASARA... KAMA UMEOCHOKA ACHIA TIMU