UONGOZI wa Klabu ya Simba unaendelea kuimarisha kikosi chao hii ni baada ya kukamilisha usajili wa kinda kutoka timu ya vijana chini ya miaka 20 (U-20) ya Azam FC, Mohamoud Haji.
Wakati Haji akiwa na timu ya vijana ya Azam FC, kwenye mechi 19 alizocheza amefunga mabao 11 kati ya hayo ana hat-trick moja ana ametoa pasi tatu za mwisho zilizozaa mabao.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa wana imani kubwa na kinda huyo kutokana na kuwa na jicho la kuona goli huku kikiweka wazi kuwa watamtumia kwenye kikosi cha timu ya vijana.
“Ni kweli tumekamilisha usajili wa mshambuliaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili lakini nafikiri ataanzia timu ya vijana kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa lakini ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuona goli,” kilisema chanzo hicho.
KIJIRI ATAMBULISHWA
Wakati huohuo aliyekuwa beki wa Singida Fountain Gate, Kelvin Kijiri ambaye gazeti hili liliripoti kuwa atatua kikosini humu ametambulishwa.
Kijiri amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba ataungana na Shomari Kapombe mkongwe ambaye ni panga pangua katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Itakumbukwa kwamba Simba walikuwa wanaitaka saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum Abdallah FEI Toto, lakini Uongozi wa klabu yake wameendelea kuweka ngumu katika usajili huo. Ila kwa upande wa mchezaji mwenyewe yuko tayari kuichezea Simba inaelezwa.
SOMA NA HII KUELEKEA MECHI YA KESHO DHIDI YA YANGA....KOCHA MAKI AMNYOONYESHA KIDOLE HABIB KYOMBO...