Home Habari za Yanga Leo MKWARA WA GAMONDI YANGA…WAKOLEZWA MOTO NA INJ HERSI

MKWARA WA GAMONDI YANGA…WAKOLEZWA MOTO NA INJ HERSI

Habari za Yanga leo

MASHABIKI wa Yanga wanatamba wanavyotaka, hata salamu zao tu zimekaa kwa kejeli wakitambia mwanzo wa msimu wakianza kwa kuchukua mataji wakiwachapa vigogo Simba na Azam lakini kuna kauli ameitoa kocha wao, Miguel Gamondi inazishtua timu pinzani.

Kocha Gamondi ametamka kwamba wala hana presha ikitokea timu yake imetangulia kuruhusu bao kwa kuwa hata wachezaji wake wanafanya makosa lakini kitu anajivunia kuwa na kikosi imara kinachoweza kukabiliana na ugumu wowote huku akisisitiza kwamba bado wataendelea kupambana kufikia malengo waliyojiwekea.

Malengo ya Yanga msimu huu ni kushinda mataji ya ndani wakianza na Ngao ya Jamii, pia wanataka kutetea Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, huku pia wakifika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali.

Gamondi amesema kuwa mechi mbili ambazo wamecheza kuwania Ngao ya jamii wakizifunga Simba (1-0) kisha Fainali wakiichapa Azam (4-1) tena wakitokea nyuma, zinathibitisha ubora walionao wakati wakisubiri kuanza msimu mpya.

“Ukitaka kujua ubora wako unatakiwa kuzishinda timu kubwa utakazoshindana nazo au zile za juu yako, nadhani matokeo ya hizi mechi mbili yametupa majibu sahihi tuko wapi, tumecheza vizuri na kupata matokeo,” alisema Gamondi na kuongeza.

“Unaposhinda mechi kubwa kama hizi hasa ukiwa unatokea nyuma ni kuonenyesha mna ubora, aina ya makosa ambayo tumefanya kwenye mchezo wa leo(juzi) tukaruhusu bao tunatakiwa kijirekebisha, tutalifanyia kazi hilo lakini kitu Bora ni namna wachezaji wanavyoweza kucheza kwa ukomavu.

“Nadhani sasa tupo tayari kuanza mashindano, tuna kazi kubwa mbele lakini kwa aina ya kikosi tulichonacho tunaweza kusimamia malengo yetu vizuri, tuna timu inayoweza kufunga kutengeneza na hata kuzuia.” Kwa upande mwingine Gamondi amemsifia beki wa kushoto wa timu hiyo, Chadrack Boka ambaye alisababisha bao la pili kutokana na krosi yake kumkuta beki wa Azam, Yoro Diaby aliyejifunga.

Gamondi amesema Boka ni mchezaji ambaye amekuwa akijituma zaidi kuanzia mazoezini ambapo huwa anawahi na kuanza mwenyewe mazoezi kabla ya pamoja, lakini pia juhudi zake hizo anazionyesha pia kwenye mechi huku akimsifia kwa kuwa na nidhamu ya mchezo.

Wakati huohuo, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, kwa upande wake ameonekana kuridhishwa na namna timu hiyo inavyocheza huku akisema ubora ulioonyeshwa katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii ndiyo unaotakiwa ndani ya Yanga.

Hersi amebainisha kwamba, katika kipindi cha usajili ambacho kinaelekea ukingoni, wameshusha wachezaji ambao wamekuwa na msaada mkubwa kikosini hapo akiwemo Chadrack Boka ambaye amekuja kuchukua nafasi ya Joyce Lomalisa aliyeondoka.

“Tumekuwa na mabadiliko mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na tija kikosini, hii inatufanya sisi viongozi kufurahia mafanikio ambayo tunaendelea kuyapata ingawa tunatambua bado tuna safari ndefu katika michuano ya kimataifa.”

Hersi aliongeza kwamba, msimu uliopita malengo yao makubwa yalikuwa ni kufika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kutofika hapo kwa muda mrefu, ingawa wanashukuru kwani waliweza kuvuka hapo na kufikia robo fainali ya mashindano hayo.

SOMA NA HII  GAMONDI WALA HANA HOFU NA KOSI LAKE.