Home Habari za Simba Leo BEKI SIMBA ATANGAZA VITA…AWEKA WAZI KILA KITU

BEKI SIMBA ATANGAZA VITA…AWEKA WAZI KILA KITU

HABARI ZA SIMBA- HAMZA

Beki wa kati wa Simba, Abdulrazack Hamza amesema, anajisikia vizuri ndani ya kikosi hicho tangu ajiunge nacho msimu huu akitokea SuperSport United ya Afrika Kusini, huku akiweka wazi hahofii ushindani wa namba uliopo na kwamba amekuja kupambana na sio kuuza sura Msimbazi.

Nyota huyo aliyewahi kutamba na timu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Mbeya City, KMC na Namungo kabla ya kwenda Afrika Kusini, amekuwa beki tegemeo ndani ya Simba chini ya kocha Fadlu Davids akishirikiana na Mcameroon, Che Fondoh Malone.

Hamza alisema, unapocheza timu kubwa kama Simba ni lazima ujiandae na ushindani wa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hivyo anachukulia changamoto ya kuzidi kumuimarisha zaidi.

“Sio rahisi kuaminiwa na kupata nafasi ya kucheza kwa sababu ushindani ni mkubwa na ukiangalia kuna mabeki wengi wazuri ambao wanastahili pia, jambo kubwa kwangu ninalozingatia ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi kwa ufasaha,” alisema Hamza.

Hamza aliongeza, kupata kwake nafasi sio kwa sababu ya kuumia kwa beki mpya wa kikosi hicho, Chamou Karaboue aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Racing Club d’Abidjan ya kwao Ivory Coast, ila anachokiamini ni kujituma kwake.

“Simba ni timu yenye malengo makubwa na ndio maana kila mchezaji anayesajiliwa ni lazima aonyeshe ushindani mkubwa ili kutimiza hayo, binafsi najivunia uwapo wangu hapa na siogopi kushindana kwa sababu napenda kupata changamoto kila siku.”

Tangu Karaboue apate majeraha ya misuli ya paja (hamstring) katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii Agosti 8, mwaka huu ambao Simba ilichapwa bao 1-0 na Yanga, Hamza amecheza mechi tatu mfululizo na kuonyesha ubora mkubwa kikosini akiiwezesha timu kutoruhusu bao.

Akicheza na Malone, Smba ilimaliza nafasi ya tatu ya Ngao kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, kisha kushinda mechi mbili za Ligi Kuu kwa mabao 3-0 na 4-0 dhidi ya Tabora United na Fountain Gate mtawalia.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids alikaririwa akieleza, licha ya nyota wengi kikosini ni wapya ila taratibu wanazidi kuzoena kwa maana ya kiuchezaji, hivyo itawachukua muda kidogo kukaa vizuri japo kwa sasa wanaangalia ushindi kwanza.

SOMA NA HII  BAADA YA OKRAHA KUTANGAZWA KUSEPA ...MGUNDA AVUNJA UKIMYA SIMBA...ABAINISHA KINACHOFUATA..