Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, 30, ameeleza mikakati yake wakati akitua Jamhuri ya Iraq huko Asia Magharibi kwa ajili ya kujiunga timu yake mpya, Al Talaba SC iliyomsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Msuva ambaye alikuwa nchini kwa zaidi ya miezi mitatu tangu kumalizika kwa msimu uliopita ambao alikuwa akiichezea Al-Najma ya Saudi Arabia, amesema hii ni fursa nyingine tena kwake kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi.
“Nina uzoefu wa kutosha kwa hiyo nahitaji kuendeleza kile ambacho nimekuwa nikikifanya kwa miaka mingi, Al Talaba SC walinitafuta baada ya mkataba wangu kumalizika kule Saudia na nikawaeleza mahitaji yangu na kwa bahati nzuri walikuwa tayari kunipa nilichohitaji,” anasema na kuongeza;
“Kilichobaki kwa sasa ni mimi tu kuwafanyia kazi yao, binafsi sina shaka na uwezo wangu nipo tayari kuonyesha Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye vipaji vingi vya soka. Ninashauku kubwa ya kuanza maisha yangu mapya ya utafutaji Iraq, najua ni nchi nzuri kama ilivyo Saudia.”
Kulingana na programu za mazoezi ambazo alikuwa akitumiwa, Msuva anaamini zitamsaidia kuwa katika mstari mmoja na wachezaji wengine wa timu hiyo.
“Mbali na ratiba ya timu, nilikuwa nikijituma mwenyewe kila siku ili niwe bora zaidi na hilo limekuwa likinisaidia. Binafsi nimejiandaa kutumika katika nafasi yoyote ambayo benchi la ufundi itapenda kunitumia.”
Al Talaba SC itakuwa timu ya sita, Msuva kuichezea nje ya Tanzania, timu lake la kwanza lilikuwa Difaa El Jadida alilojiunga nayo Julai 2017, baada ya kuonyesha makali yake ndani ya miaka mitatu kwenye ligi ya Morocco, Wydad Casablanca ilivutiwa naye na kumsajili lakini hakudumu kwa vigogo hao kutokana na ishu za madai zilizowafanya kufikishana Fifa.
Baadaye Msuva aliibukia Saudi Arabia ambako alianza kwa kuichezea, Al-Qadsiah mkataba wake ulipomalizika alirejea Afrika kwa kujiunga na JS Kabylie ya Algeria lakini mambo hayakumwendea vizuri mkataba wake ulikatishwa na ndipo alipoamua kurejea tena Saudia kwa kujiunga Al-Najma aliyoichezea msimu uliopita.
LIGI YA MABINGWA
Msuva ana ndoto ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Asia ambayo timu ya Cristiano Ronaldo, Al Nassr ya Saudi Arabia ilishiriki na kuishia hatua ya robo fainali ambapo waliondolewa na Al Ain ya Falme za Kiarabu.
Jambo la kwanza natakiwa kwenda kupambana na wachezaji wenzangu ili tutwae ubingwa kwa kufanya hivyo tutakuwa tumejiweka katika nafasi ya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa, itakuwa ni nafasi nyingine nzuri kwangu,”
“Nimecheza ligi ya mabingwa Afrika na kufanya vizuri hivyo nahitaji kucheza michuano ya namna hiyo Asia, najua kwamba haitakuwa kazi nyepesi kwa sababu mpira wa Iraq unaushindani mkubwa kama ilivyo kwa Saudia,” anasema.
Msimu uliopita Al Talaba SC ilishika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi yenye timu 20 hivyo wanakibarua kizito mbele yao kuhakikisha wanaivua ubingwa Al Shorta.
[…] la kusajiliwa Peshmarga Sulaymaniya SC inayoshiriki Ligi daraja la kwanza nchini Iraq akiungana na Simon Msuva anayetumikia Al […]