Home Habari za Simba Leo SIMBA NDIO MTAIJUA LEO…WAARABU WAINGIA UBARIDI TAYARI

SIMBA NDIO MTAIJUA LEO…WAARABU WAINGIA UBARIDI TAYARI

HABARI ZA SIMBA

MNYAMA SIMBA inacheza mechi ya kwanza katika michuano Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ikiwa ugenini dhidi ya Al Ahli Tripoli leo na hakika sasa ndio mtawajua Wekundu wa Msimbazi.

Al Ahli ni klabu ya pili kwa mafanikio katika historia ya soka la Libya nyuma ya Al-Ittihad, ikishinda mataji 13 ya Ligi Kuu ya Libya, mataji 7 ya Kombe la Libya na mataji mawili ya Super Cup.

Hii ni klabu pekee kutoka Libya iliyowahi kufika fainali ya michuano ya Afrika ilipofanya hivyo katika Kombe la Washindi Afrika 1984, na kutakiwa kukutana na Al Ahly ya Misri lakini ikajitoa kwa sababu za kisiasa zilizotokana na uhusiano mbaya kati ya nchi hizo wakati huo.

Mafanikio makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni kufika hatua ta robo fainali mara moja tu mwaka 2017, wakati katika michuano hii ya Kombe la Shirikisho inakokutana na Simba leo, ilifika nusu fainali mwaka 2022.

Klabu hiyo inayovaa jezi za kijani na nyeupe ilianzishwa mwaka 1950 na vijana walioungana katika harakati za kupigania uhuru kutoka kwa majeshi ya Uingereza na ikapewa jina la Al Istiqlal, (linalomaanisha Uhuru), lakini baadaye likabadilishwa na kuwa Al Ahli Tripoli (linalomaanisha Familia).

Wakati Simba imeanzia hatua hii kutokana na ubora iliyonayo katika viwango vya CAF baada ya kuwa imecheza robo fainali tano za CAF katika miaka sita iliyopita, Al Ahli Tipoli ilianzia hatua ya awali ikiing’oa Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1.

Katika mechi ya kwanza Al Ahli Tripoli iliifunga Uhamiaji 2-0 na marudiano ikaifunga 3-1, shukrani kwa mabao ya Ahmed Krawa’a aliyeweka chuma mbili na Ammar Taifour. Mechi hizi zote zilichezwa Libya, baada ya timu hiyo ya Zanzibar kukubali udhamini uliojaa utata wa kwenda kucheza mechi zote huko, licha ya Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi kufanya jitihada kubwa kuboresha miundombinu ya michezo hasa viwanja.

Katika kuthibitisha kwamba ofa ya Uhamiaji ilijaa utata, klabu hiyo haijathubutu kuiomba Simba nayo ikacheze mechi zote kule Libya.

SIMBA NDIO HII SASA

Simba inashuka kwenye Uwanja wa June 11, mjini Tripoli, Libya ikiwa inatokea katika ligi iliyo juu ya Ligi ya Libya kwa ubora wa viwango vya CAF. Wakati Ligi ya Libya ikishika Na.10 CAF, Ligi Kuu Bara ni ya 6 kwa ubora Afrika.

Simba imekuwa na rekodi bora kutokana na kufika mbali Afrika ikicheza robo fainali tano za CAF, ambazo nne ni za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho.

Licha ya msimu uliopita kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, uongozi wa klabu hiyo chini ya mwekezaji bilionea Na.1 kijana Afrika, Mohamed Dewji, uliona inastahili kufika mbali zaidi, hivyo ukafanya mabadiliko makubwa ya kikosi, hasa baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika ligi na kuangukia michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako wengi wanaamini siko hadhi ya klabu hiyo kongwe.

Ikashusha mashine za kazi kibao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mara hii inafanya makubwa zaidi.

Ilimnasa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, Jean Charles Ahoua, beki Karaboue Chamou raia wa Ivory Coast, mshambuliaji wa Uganda, Stephen Mukwala, kiungo Mtanzania Yusuph Kagoma, beki Kelvin Kijili (Tanzania), kiungo Augustine Okejepha (Nigeria), Joshula Mutale (Zambia), beki Valentin Nouma (Burkina Faso) na kipa Mousa Camara wa timu ya taifa ya Guinea.

Pamoja na kumleta kocha mpya Fadlu Davids, Simba inatarajiwa kuwa na mtihani wa kuonyesha sasa zile rangi zake halisi licha ya kwamba nyota wengi wapya ndio wanazidi kuzoeana kutengeneza muunganiko.

Simba imeanza vyema msimu wa Ligi Kuu Bara kwa kushinda mechi mbili za kwanza kwa jumla ya mabao 7-0, ikiifunga Tabora United 3-0 na Fountain Gate 4-0, hivyo kuonyesha ubora katika maeneo yote ya uwanja – kwenye kushambulia na kujilinda.

Ahoua ameanza kuonyesha kwamba hakushinda kwa bahati mbali tuzo ya MVP kule Ivory Coast, kwa kuhusika moja kwa moja katika mabao manne kati ya 7 ambayo Simba imefunga, huku jingine moja la tano akimpa mpira mtu aliyetoa asisti ya bao. Amefunga mabao mawili na kutoa asisti mbili na tayari ameanza kuzi-run shoo za kikosi cha Fadlu.

Mashabiki wana matumaini makubwa sana na Ahoua na wengine kina Debora Mavambo, Mutale, Mukwala huku Camara akiwa imara langoni alikoonyesha ubora mkubwa wa kucheza mpira kwa miguu.

Simba inaweza kutumia udhaifu wa Tripoli wa kuwa na wachezaji wazee wengi na kuwakimbiza ili kuwachosha na kupata matokeo mazuri kuanzia leo ugenini na katika marudiano kwa Mkapa Jumapili ya Septemba 22.

Lakini mtihani ulio wazi ni kupambana na uzoefu walionao nyota wakongwe wa Tripoli, huku pia Simba ikitakiwa kuthibitisha hofu ya mashabiki kuhusu uwezo wa kikosi chao kushinda mechi kubwa.

Simba ilifungwa dhidi ya Yanga 1-0 katika Ngao ya Jamii, ikatoka sare ya 1-1 na Al Hilal ya Sudan katika mechi ya kirafiki.

Ushindi dhidi ya Tabora United na Fountain Gate katika ligi ulionyesha Simba mpya inavyokuja, lakini vikosi ilivyokabiliana navyo havikuwa kamili kutokana na nyota wakali wengi wapya wa timu hizo kukosa mechi hizo kwa vile walikuwa hawajatimiza taratibu za vibali.

Hivyo, kwa kuanzia na mechi hizi mbili dhidi ya Tripoli ndio tutaiona ile Simba ya ndoto za wengi.

UGENINI MAJANGA

Hata hivyo, Simba imekuwa haina historia nzuri kwa mechi za ugenini katika michuano tofauti ya Afrika na kudhihirisha hilo, mechi 10 zilizopita, imepata ushindi mara moja tu, kutoka sare nne na kupoteza tano, ikifunga mabao matano na kufungwa 11.

Ardhi ya Kaskazini mwa Afrika ndio imekuwa ngumu zaidi kwa Simba kwa uishia kupata sare na vichapo.

Katika mechi 10 zilizopita dhidi ya klabu za ukanda huo haijapata ushindi hata mmoja, ikitoka sare mbili na kupoteza nane mtawalia huku ikifunga mabao mawili tu na kufungwa 18.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONA MAMBO MAGUMU...KRAMO AOMBA KURUDI KWAO KUJIPANGA UPYA...