Home Habari za Simba Leo AL AHLI YAMWAGA PESA KUIMALIZA SIMBA.

AL AHLI YAMWAGA PESA KUIMALIZA SIMBA.

HABARI ZA SIMBA-AL AHL TRIPOLI

Al Ahli Tripoli ni timu inayotumia pesa nyingi katika kujiendesha. Katika kujiandaa na msimu mpya ikiwamo kuiwaza Simba, imemwaga mkwanja wa maana katika kusajili nyota tisa wapya, lakini watano kati yao wana umri wa miaka 30+.

Agosti 13, 2024 ilimsajili mshambuliaji wa kati Mabululu (32), ambaye jina lake halisi ni Agostinho Cristovao Paciencia, kutoka klabu ya Ittihad Alexandria ya Ligi Kuu ya Misri kwa ada ya uhamisho ya Euro 1.5 milioni (sawa na Sh4.4 bilioni za Tanzania).

Huyu Mabululu analipwa mshahara wa dola 50,000 (sawa na Sh136 milioni za Tanzania) kwa mwezi.

Straika huyu msimu uliopita alicheza mechi 25, akapiga mashuti 63 huku ni 20 tu kati ya hayo yakilenga lango. Akafunga mabao 11, lakini matano ni ya penalti, zote alipiga kulia kwa kipa.

Imemsajili pia winga wa kushoto, Hamdou El Houni (30) kutoka Wydad kwa ada ya uhamisho ya Euro 1 milioni (sawa na Sh3 bilioni). Lakini huyu msimu uliopita, alikuwa ovyo licha ya kusajiliwa kwa pesa nyingi, kwani alicheza mechi 19, alipiga mashuti 17 tu yaliyolenga lango na hakufunga bao hata moja hadi alipouzwa kwa Tripoli.

Ilimsajili pia kiungo wa kati, Ghaylen Chaalali (30) kutoka Esperance kwa Euro milioni 1 (sawa na Sh3 bilioni). Nyota huyu alicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Mei 25, 2024 ambayo Esperance ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa mara 12 wa Afrika, Al Ahly ya Misri.

Wengine waliosajiliwa ni beki wa kushoto Bakhit Khamis (30), kutoka Al-Merrikh SC, pia amesajiliwa kiungo wa kushoto, Al-Gozoli Nooh (21), winga wa kushoto Malek Al-Andalusi (21) kutoka Libyan SC, winga wa kushoto Tarek Bshara (24) kutoka Al-Olympique SC Zawiya.

LIGI HAINA PESA

Licha ya Al Ahli Tripoli kutumia pesa nyingi katika kujiendesha, Ligi Kuu ya nchi hiyo ambayo inashika nafasi ya 10 kwa ubora barani Afrika, haina udhamini wa kutosha kugharamia usafiri wa timu kwenda kwenye vituo vyao vya mechi.

Hivyo kulazimika kuingia msimu wa nne huu ikichezwa kwa makundi mawili ya timu 10+ kila moja na kisha timu tatu kutoka kila kundi zinakutana katika ligi ya jumla na kila timu kucheza mechi tano tu kumpata bingwa wa jumla.

Msimu uliopita, Al Ahli Tripoli iliongoza kundi ikipata pointi 48 baada ya kucheza mechi 20, ikishinda 15 sare 3 na vipigo 2, ikifunga mabao 29 na kuruhusu 7. Na ilipoingia katika ligi ya jumla ikashika nafasi ya tatu kwa pointi 7, ikishinda mechi 2, vipigo 2 na sare 1, ikifunga mabao 6 na kuruhusu mabao 6. Mabingwa wa jumla walikuwa Al Nasr waliomaliza na pointi 15, wakifuatiwa na Al Ahly Benghazi iliyomaliza na pointi 8.

SOMA NA HII  INSHU YA LAMECK LAWI NA KAGOMA NDANI YA SIMBA,YANGA TFF IKO HIVI