Home Habari za Yanga WAKATI KIDONDA CHA TABORA HAKIJAKAUKA…SIMBA WAZIDISHA SIMANZI NA VILIO YANGA….

WAKATI KIDONDA CHA TABORA HAKIJAKAUKA…SIMBA WAZIDISHA SIMANZI NA VILIO YANGA….

Habari za Yanga SC

HUKU mashabiki wa Yanga wakiendelea kuugulia timu yao ya wanaume kuangukia kipigo mara mbili mfululizo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, timu ya Simba Queens, imepeleka kilio tena kwa wadada wao, Yanga Princess baada ya kuitandika bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara kwa Wanawake iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.

Yanga ilikubali kipigo kwenye Ligi Kuu msimu huu kwa mara ya kwanza ilipocheza na Azam FC na kulala kwa bao 1-0 na kisha kuchapwa 3-1 na Tabora United mechi zote zikipigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake jana, bao la kujifunga la Danai Bhobho, liliipa Simba Queens pointi tatu na kusababisha Yanga Princess kulala 1-0, katika Uwanja wa KMC Complex.

Tukio hilo linafanana na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, dabi ya wanaume, ambapo Kelvin Kijili wa Simba alijifunga mwenyewe na kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0, mechi iliyochezwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 19, mwaka huu.

Banai, kiungo mkabaji raia wa Zimbabwe aliyejiunga na Yanga Princess msimu huu akitokea Simba Queens, aliuweka mwenyewe mpira ndani ya wavu kwa mguu wa kushoto dakika tatu tu baada ya mapumziko, wakati akiokoa krosi iliyopigwa na Elizabeth Wambui ambayo ilikuwa inakwenda kumkuta Vivian Corazone.

Mchezaji huyo katika jitihada zake za kutaka kuuokoa mpira usimfikia kiungo mshambuliaji huyo raia wa Kenya, akaukwamisha wavuni.

Ushindi huo umeifanya Simba Queens kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya kutoka sare ya bao 1-1, mechi ikipigwa kwenye uwanja huo huo Oktoba 2, mwaka huu.

Yanga Princess walianza kufika kwenye lango la Simba Queens mapema tu sekunde 20 za mwanzo katika mchezo huo wa raundi ya nne ya Ligi Kuu, shambulizi lililofanywa na Ariet Udong, lakini shuti lake lilitoka nje.

Kama vile haitoshi, mchezaji huyo nusura aipatie timu yake bao dakika ya pili ya mchezo baada ya kupiga kichwa mpira wa faulo iliyopigwa na Danai, mpira ukatoka juu la lango.

Simba Queens ilijibu dakika ya nne kwa mpira wa faulo uliopigwa na Vivian, uliokwenda kutua kwenye kichwa cha Mkenya mwenzake, Jentrix Shikangwa, mpira ukatoka nje.

Katika kipindi chote cha kwanza, Simba Queens ilionekana kucheza pasi fupi fupi na kushambulia lango la Yanga Princess, ambao mabeki wake chini ya Diana Antwi walionekana kusimama imara kuokoa hatari zote.

Yanga Princess waliamua kukaa nyuma ya mpira, lakini walifanya mashambulizi ya kushtukiza kwa pasi ndefu kupitia kwa straika wao mwenye mbio, Ariet na mara kwa mara walikuwa hatari mno wanapofanya hivyo.

Kipa wa Yanga Princess, Rita Akarekor, alilazimika kufanya kazi ya ziada dakika ya 12, alipopangua shuti la Elizabent Wambui, na dakika moja baadaye alizima shambulizi lingine lililofanywa na Shikangwa.

Wema Richard angeweza kuipatia Yanga Princess bao dakika ya 20 baada ya krosi aliyopiga kukatika na kuonekana ikienda kujaa wavuni, lakini golikipa, Janeth Shija, aliruka juu na kwa ustadi aliupangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanga Princess ilifanya shambulio lingine kali dakika ya 36, lakini mabeki wa Simba Queens walikaa imara kuokoa.

Kipindi cha pili timu zilifanya mabadiliko, lakini mchezo ulionekana kupoa zaidi na wachezaji wa pande zote mbili walionekana kuchoka kadri muda ulivyozidi kusonga mbele.

Ni kipindi ambacho Simba Queens ilikosa mabao mengi ya wazi kuliko wapinzani wao.

Ushindi huo unaifanya Simba Queens kufikisha jumla ya pointi 12, ikishinda mechi zake zote nne ilizocheza, ikiendelea kukaa kileleni, huku Yanga Princess baada ya sare tatu, ikipoteza mchezo wa kwanza na kubaki na pointi tatu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUCHAGULIWA KUWA BOSI WA VILABU AFRIKA...MAJUKUMU YA HERSI HAYA HAPA...