Klabu ya Yanga imemfuta kazi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi leo Ijumaa Novemba 15, 2024.
Taarifa ya kufutwa kazi kwa makocha hao imetolewa na Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Yanga ikisema: “Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutarifu umma kuwa umevunja mkataba na Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Angel Miguel Gamondi.
“Vilevile, Uongozi wa Young Africans Sports Club, umesitisha mkataba wa Kocha Msaidizi wa Kikosi cha Kwanza, Moussa Ndaw.”
Aidha, taarifa hiyo imesema uongozi wa Young Africans Sports Club unawashukuru makocha hao kwa mchango wao ndani ya Klabu yetu na unawatakia kila la kheri katika majukumu yao mapya.
“Tayari mchakato wa haraka wa kutafuta Makocha wapya wa kikosi chetu cha kwanza umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde,”imeongeza taarifa hiyo.
Taarifa zanasema kuwa sababu ya Gamondi kufutwa kazi ni pamoja na kushindwa kuipa makali Yanga kama ilivyokuwa msimu uliopita, huku sababu ya ubabe na kiburi vikitajwa.
Aidha duru za ndani zaidi zinadai kuwa msimu huu kocha huyo ameshindwa kusimamia nidhani ya wachezaji hali iliyopelekea wachezaji wengi kupoteza viwango na kushindwa kuisaidia timu.
Inaarifiwa kuwa, sababu nyingine ni kuweka matabaka na kushindwa kuishi na wachezaji vizuri, hatua iliyopelekea baadhi ya wachezaji kushindwa kupewa nafasi hasa wale walioonekana hawako karibu naye ili hali wanauwezo wa kucheza.