KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi kuwa anataka kuona kikosi chake kinapata mabao ya ugenini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.
Simba, ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya CAF, wanatarajiwa kuondoka nchini Machi 28 kuelekea Misri kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Aprili 2.
Fadlu anaeleza kuwa Al Masry ni timu bora inayoshika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Misri, na hivyo ni wapinzani wenye uwezo mkubwa. Anasisitiza kuwa Simba italazimika kucheza kwa umakini mkubwa iwe na mpira au bila mpira.
“Tunapocheza ugenini, ni muhimu kufunga bao kwa sababu linasaidia sana katika mashindano haya. Tunakutana na changamoto kwa sababu tuna wachezaji vijana wasio na uzoefu wa hatua hii ya mashindano,” amesema Fadlu.
Kocha huyo alitumia mechi dhidi ya Al Ahly Tripoli katika hatua ya awali kama kipimo cha kikosi chake, alikiri kuwa hawakuwa imara kimwili na kiakili kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi na ujio wa wachezaji wapya, lakini walifanikiwa kupata sare ugenini kabla ya kushinda nyumbani.
“Mchezo ule ulinipa taarifa muhimu kuhusu wachezaji wangu na wapinzani wetu. Hilo lilitusaidia kuelewa namna ya kushindana katika hatua inayofuata,” ameongeza.
Fadlu anaamini kuwa mafanikio ya Simba hatua ya makundi yanaonyesha uimara wa timu licha ya kuwa na wachezaji wachanga.
Akikumbuka enzi zake akiwa Orlando Pirates, anasema walikuwa wakicheza kila baada ya siku tatu, na iliwagharimu kwenye ligi baada ya kushindwa fainali.
Simba inakabiliwa na majukumu makubwa msimu huu, ikihitaji kushindania mataji matatu, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB, na kufika mbali kwenye michuano ya CAF.
“Wachezaji wanapaswa kuelewa umuhimu wao kwenye timu. hatupaswi kutegemea mtu mmoja, bali nguvu ya pamoja ndiyo itatufanikisha,” amesema Fadlu.