Kwa miaka ishirini na tano, Vodacom Tanzania PLC imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuchochea maendeleo endelevu katika jamii. Msafara wa Twende Butiama wa mwaka 2025 kwa mara nyingine unadhaminiwa na Vodacom na litahusisha msafara wa umbali wa karibu kilomita 1,500 likipita katika mikoa 11 kuanzia tarehe 3 hadi 13 mwezi Julai, na kumalizika kwa kishindo katika kijiji cha Butiama mkoani Mara – mahali alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumzia kuhusu msafara huo, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania na Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Zuweina Farah, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika harakati za maendeleo nchini.
“Tunaamini katika kuunganisha Watanzania kwa mustakabali bora, na Twende Butiama ni moja ya njia tunayoitumia kutimiza dira hiyo. Iwe ni ujumuishaji wa kidijitali, upatikanaji wa elimu, huduma bure za afya au utunzaji wa mazingira, kampeni hii inaonesha nguvu ya ushirikiano na dhamira ya kweli,” alisema Zuweina.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Twende Butiama imeboresha maisha ya maelfu ya Watanzania. Zaidi ya watu 150,000 wamenufaika na huduma za afya bure, zaidi ya miti 100,000 imepandwa katika shule mbalimbali nchini na kuhamasisha uelewa wa mazingira na kuboresha mazingira ya kujifunzia, zaidi ya madawati 1,900 yamegawiwa kwa shule za msingi 34 ili kupunguza idadi ya wanafunzi kukaa chini, na baiskeli 50 zimesambazwa kwa wanafunzi wa vijijini ili kuwapunguzia muda wa kufika shuleni na kuongeza mahudhurio.
