Home Habari za michezo FT: YANGA 2-0 SIMBA…..BUNDI ATUA MSIMBAZI…MASTAA JAGWANI KUJAZWA MINOTI….

FT: YANGA 2-0 SIMBA…..BUNDI ATUA MSIMBAZI…MASTAA JAGWANI KUJAZWA MINOTI….

Habari za Yanga leo

Pacome Zouzoua na Clement Mzize wamekuwa mashujaa wa Yanga leo hii baada ya kuiongoza timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yaliyoihakikisha timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Matokeo hayo yameifanya Yanga imalize ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi na pointi 82 huku Simba ilimaliza katika nafasi ya pili na pointi 78.

Zouzoua alitangulia kuifungia Yanga katika dakika ya 66 kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na refa Mohamed Amin baada ya kipa Moussa Camara kumfanyia faulo kiungo huyo wa Yanga katika eneo la hatari.

Wakati Simba ikipambana kusaka bao la kusawazisha, Mzize ambaye aliingia uwanjani akitokea benchi, aliipatia Yanga bao lililozika rasmi matumaini ya Simba kupata ushindi na kutwaa ubingwa akimalizia vyema pasi ya Pacome.

Ushindi huo haukupatikana kwa kubahatisha kwa Yanga kwani ilionekana kutawala muda mwingi wa mechi ikitengeneza nafasi nyingi tofauti na Simba ambayo ilifanya hivyo mara chache huku ikitengeneza idadi ndogo ya nafasi.

Yanga ingeweza kuimaliza mechi katika kipindi cha kwanza lakini ilishindwa kutumia vyema nafasi ambazo ilitengeneza.

Mfano ni dakika ya 12 baada ya Mudathir Yahya kufanya kazi nzuri ya kumtoka Chamou Karaboue na kupiga pasi iliyoenda kwa Pacome Zouzoua ambaye akiwa analitaza lango, alipaisha mpira huo.

Dakika sita baadaye Chadrack Boka alipokea pasi nzuri ya Israel Mwenda lakini wakati wengi wakiamini angeweka mpira huo kimiani, beki huyo alipiga shuti lililotoka nje.

Simba walijibu shambulizi hilo katika dakika ya 27 baada ya Shomary Kapombe kupiga krosi nzuri kuielekeza kwa Steven Mukwala lakini kipa Djigui Diarra wa Yanga aliwahi kuokoa mpira huo.

Hadi filimbi ya refa Amin ilipopulizwa kuashiria muda wa mapumziko, timu hizo zilienda vyumbani zikiwa hazijafungana.

Hata hivyo mambo yalikuwa magumu kwa Simba katika kipindi cha pili ambacho licha ya kujaribu kufunguka kusaka mabao, ilijikuta ikiruhusu mabao hayo mawili ambayo yamefanya taji la Ligi Kuu msimu huu kwenda kwa watani wao Yanga.

Katika mchezo huo, Yanga ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Prince Dube, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya ambao nafasi zao zilichukuliwa na Clatous Chama, Salum Abubakar, Jonathan Ikangalombo na Mzize.

Simba iliwatoa Steven Mukwala, Shomari Kapombe, Yusuph Kagoma, Joshua Mutale na Fabrice Ngoma ambao nafasi zao zilichukuliwa na Leonel Ateba, Awesu Awesu, Abdulrazack Hamza, Valentine Nouma na Kibu Denis.

Yanga imetwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 82 huku Simba ikimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 78.

Hilo ni taji la 31 la Ligi Kuu kwa Yanga huku watani zao Simba wakiwa wametwaa mara 22.

Matokeo hayo yameifanya Yanga iwe imepata ushindi katika mechi tano mfululizo za mashindano tofauti dhidi ya Simba.

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilichoanza kiliundwa na Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Abdullah, Khalid Aucho, Duke Abuya, Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli.

Simba ilianzisha kikosi kilichokuwa na Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Fondoh Malone, Chamou Karaboue, Yusuph Kagoma, Joshua Mutale, Fabrice Ngoma, Steven Mukwala, Jean Ahoua na Elie Mpanzu.

SOMA NA HII  NDOA YA AZIZI KI NA YANGA SHAKANI....ENG HERSI ASALIMU AMRI ....MAYELE ATAJWA....