Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA JMOSI….MAXI, PACOME WAPIGWA KITI MOTO YANGA….MABOSI WAKOMAA NAO…

KUELEKEA MECHI YA JMOSI….MAXI, PACOME WAPIGWA KITI MOTO YANGA….MABOSI WAKOMAA NAO…

Habari za Yanga leo

KUMEKUWA na vikao vya hapa na pale vinavyofanywa na mabosi wa Yanga sambamba na wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo ili kuweka mambo sawa kuelekea mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi.

Unaambiwa vikao hivyo vinavyoendelea ndani ya Yanga, vilianza tangu kikosi hicho kilipokuwa Malawi kabla ya kurejea Dar es Salaam ambapo nyota mmoja wa kikosi hicho amefichua siri kwamba viongozi wamewaambia wachezaji wote akiwamo Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Clement Mzize, Djigui Diarra na kila mmoja kuhakikisha Jumamosi ushindi unapatikana na kufuzu hatua ya makundi.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Silver Strikers katika mechi ya marudiano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo, itakayochezwa Jumamosi Oktoba 25, 2025 kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga inayoingia uwanjani ikiwa imetoka kufungwa bao 1-0 ugenini nchini Malawi, inahitaji ushindi wa angalau tofauti ya mabao 2-0 ili kufuzu hatua ya makundi kwa msimu wa nne mfululizo kwenye mashindano ya CAF baada ya 2022-2023 kufanya hivyo upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, kisha 2023-2024 na 2024-2025 upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nyota mmoja wa kikosi cha kwanza ndani ya Yanga akicheza nafasi ya kiungo, amefichua kwamba, kabla ya kuanza safari ya kurudi Dar es Salaam Jumatatu wiki hii, kulifanyika kikao kifupi na uongozi wa juu wa timu hiyo ukawanyooshea maneno kuwa, kuna ulazima kwao wachezaji kubadilika.

Kwa mujibu wake, mabosi wa Yanga waliwaambia wachezaji hao kwamba, licha ya kumuondoa kocha Romain Folz, lakini hata wao wachezaji hawakucheza vizuri na mechi ya marudiano ipo kwenye mikono yao, lazima wafanye kweli wafuzu makundi.

“Huu mchezo upo kwenye mikono yetu, tuliyoambiwa kule Malawi sio maneno rahisi, ndio maana unaona tulivyofika tulikubaliana hakuna kuongea na yeyote, akili iwe kwenye mechi hii ya Jumamosi,” amesema kiungo huyo.

“Tumeambiwa tuamke, viongozi hawakufurahia tulivyocheza hata kama wamemuondoa kocha, uongozi hautaki kusikia tunatolewa na hawa jamaa.”

Naye beki wa timu hiyo licha ya kuthibitisha hilo, amesema umakini kwenye mechi ya marudiano utakuwa mkubwa hasa baada ya kuhakikishiwa kutakuwa na bonasi nzuri.

Beki huyo amesema, wao kama wachezaji wameendelea kusisitizana juu ya kupigania ushindi kwenye mechi hiyo iliyobeba hatma yao kimataifa msimu huu.

“Ni kweli hayo uliyosikia lakini tunajipanga, haitakuwa rahisi, lakini tutakuwa makini sana tunahamaishana sana huku kambini,” amesema.

Juzi Jumanne mchana Oktoba 21, 2025, kikosi cha Yanga kiliingia kambini ikiwa ni baada ya Jumatatu Oktoba 20, 2025 kuwasili nchini kikitokea Malawi kilikochapwa bao 1-0 na Silver Strikers.

Katika maandalizi ya mechi hiyo, kikosi cha Yanga hivi sasa kipo chini ya kocha Patrick Mabedi ambaye anakaimu nafasi ya Folz aliyeondoshwa muda mchache baada ya kupoteza mbele ya Silver Strikers.

Inafahamika kuwa, tangu kikosi hicho kiingie kambini, viongozi wamekuwa wakifanya vikao ikiwamo kujadili ujio wa kocha mpya na namna ya kukabiliana na Silver Strikers na kushinda Kwa Mkapa.

SOMA NA HII  KISA UJIO WA CHAMA...PABLO AVUNJA UKIMYA...AFUNGUKA MSIMAMO WAKE...ADAI HAKUTAKA KUWA KIKWAZO..