Home Azam FC YAO HATARINI MIKONONI MWA PEDRO

YAO HATARINI MIKONONI MWA PEDRO

36
0

Hatma ya beki wa Yanga, Attohoula Yao, kuendelea kusalia ndani ya kikosi cha Wananchi ipo mikononi mwa Kocha Mkuu, Pedro Gocalves, ambaye ndiye ataamua mustakabali wa nyota huyo baada ya tathmini ya afya na kiwango chake kukamilika.

Yao, bado ana mkataba na klabu hiyo, aliondolewa kwenye usajili wa msimu huu kutokana na majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu,

Licha ya kuwa ni sehemu ya wachezaji wanaolipwa na klabu hiyo kila mwezi. Hatua hiyo ilichukuliwa ili kumpa nafasi ya kutekeleza programu ya matibabu na kurejea kwenye ubora wake wa awali.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amefafanua kuwa kwa sasa wanaisubiri ripoti ya idara ya utimamu wa mwili ambayo itabainisha kama Yao atakuwa fiti ifikapo Januari au Februari.

Ripoti hiyo itakuwa msingi wa kocha kufanya uchambuzi kama bado anamhitaji kwenye eneo lake la ulinzi.

Kamwe amesema katika nafasi anayoicheza Yao, tayari kuna wachezaji wengine wawili; Israeli Mwenda na Kibwana Shomari , hivyo uamuzi wa kumrudisha kwenye usajili au la utategemea mahitaji ya benchi la ufundi na mkakati wa timu kuelekea mzunguko ujao.

“Kocha Pedro atafanya uchunguzi wake binafsi mara tu Yao atakapothibitishwa kuwa fiti kwa asilimia 100, ili kubaini kama kiwango chake kimerudi katika hali inayokidhi mahitaji ya kikosi.

Baada ya tathmini hiyo, kocha atawasilisha ripoti yake kwa uongozi, ikieleza kama anamuhitaji beki huyo ili arejeshwe kwenye usajili, aendelee kufanya mazoezi ndani ya timu au atolewe kwa mkopo ili apate muda wa kucheza mara kwa mara,” amesema.