Home Habari za michezo OKELLO ANA MZUKA YANGA, AANZA KAZI GYM

OKELLO ANA MZUKA YANGA, AANZA KAZI GYM

17
0

HAKUNA kulala, hilo ndilo neno linaloelezea mwanzo wa safari ya mshambuliaji mpya wa Yanga, Allan Okello, ambaye tayari ameanza rasmi mazoezi na kujiunga na wachezaji wenzake katika Gym mara baada ya kukamilisha usajili wake.

Okello ameonekana akiwa na hamasa kubwa na ari ya hali ya juu wakati wa mazoezi, akionesha wazi kuwa yupo tayari kukabiliana na changamoto mpya ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuipigania nafasi yake ndani ya kikosi cha Wananchi.

Mshambuliaji huyo amesajiliwa akitokea klabu ya Vipers SC ya Uganda, akiwa na uzoefu mpana wa soka la Afrika Mashariki pamoja na mashindano ya kimataifa, jambo linaloongeza matumaini kwa benchi la ufundi la Yanga.

Ujio wake unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Wananchi, huku kocha akiamini kuwa kasi, ufundi na uwezo wake wa kufumania nyavu vitakuwa silaha muhimu kwa timu msimu huu.

Okello pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, na anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliowahi kung’ara katika Ligi Kuu ya Uganda pamoja na michuano ya klabu barani Afrika.

Mashabiki wa Yanga tayari wameanza kuweka matumaini makubwa kwake, wakitarajia kumuona akitoa mchango mkubwa katika jitihada za kutetea ubingwa wa ligi na kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu.