BENCHI la ufundi la Simba linaloongozwa na Kocha Mkuu, Steve Barker, limeanza kwa umakini mkubwa maandalizi ya kiufundi kuelekea mchezo muhimu dhidi ya Esperance Sportive de Tunis.
Hatua hiyo ikilenga kuboresha ubora wa timu na kuwachunga kwa karibu wachezaji hatari wa wapinzani wao.
Simba kwa sasa ipo nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi, Januari 24.
Mchezo huo unatajwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia na uzoefu wa Esperance katika michuano ya kimataifa.
Katika maandalizi hayo, Barker kwa kushirikiana na wasaidizi wake, Selemani Matola pamoja na mtaalamu wa video wa klabu hiyo, Prinil Deean, wametumia muda mwingi kuisoma Esperance kwa kina, wakichambua mifumo yao ya uchezaji, mbinu na nguvu walizonazo katika kila eneo la uwanja.
Taarifa zinaeleza kuwa benchi hilo la ufundi limejikita zaidi katika uchambuzi wa video za mechi za awali za Esperance, ili kubaini mapungufu yao na kutengeneza mkakati sahihi utakaoiwezesha Simba kupambana vyema katika mchezo huo mgumu.
Hata wakati wa safari ya kuelekea Tunisia, Barker na wasaidizi wake hawakuacha kazi, ambapo walionekana wakiendelea na majadiliano ya kiufundi ndani ya ndege, hususan katika safari ya kutoka Istanbul, Uturuki, kuelekea Tunis, Tunisia.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Simba kuingia uwanjani ikiwa imejiandaa kikamilifu, huku mashabiki wa wekundu wa Msimbazi wakitarajia kuona timu yao ikionesha nidhamu ya hali ya juu na matokeo chanya dhidi ya Esperance.