Home Habari za michezo YANGA YAJIPANGA NA MIPANGO HATARI

YANGA YAJIPANGA NA MIPANGO HATARI

85
0

OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema kikosi cha timu hiyo kimemaliza salama mchezo wao dhidi ya Al Ahly bila kupata majeruhi wowote, jambo ambalo ni faraja kubwa kwa benchi la ufundi kuelekea michezo ijayo ya hatua ya makundi.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kamwe amesema Al Ahly wamefanikiwa kupata matokeo mazuri wakiwa nyumbani kwao, huku wakikiri kuwa timu hiyo imekuwa ikipata changamoto inapocheza mechi za ugenini katika mashindano hayo.

Ameeleza kuwa hatua ya makundi ni ngumu na inahitaji hesabu kubwa, huku kila timu ikipambana kuhakikisha inakusanya pointi muhimu ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kamwe amesema ushindi wa Al Ahly ni jambo la kawaida kwao wanapocheza nyumbani, na amesisitiza kuwa Yanga haina sababu ya kukata tamaa kwani bado nafasi ya kufanya vizuri ipo wazi.

Ameongeza kuwa Yanga nayo ina kila sababu ya kufurahi itakapocheza nyumbani Januari 31, ambapo mashabiki wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kuipa timu hiyo sapoti kubwa katika mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu.

“Tunajua utakuwa mchezo mgumu, lakini tunaenda kujipanga vizuri ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri nyumbani. Tuna imani na kikosi chetu,” amesema Kamwe.